Sambaza....

Klabu ya soka ya Biashara United ya mkoani Mara imeonesha haina utani kabisa pale linapokuja suala la maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu soka Tanzania Bara, kwani mpaka sasa imewaruhusu wachezaji watatu kutoka nchi za Ivory Coast, Ghana na Nigeria kufanya majaribio.

Meneja wa klabu hiyo Amani Josiah amesema itakuwa mapema sana kuwataja kwa majina wachezaji hao, lakini amesema itoshe kueleweka kuwa wapo na wachezaji ho katika kambi inayoendelea mkoani Mara kujiandaa na msimu ujao wa ligi.

Josiah amesema wachezaji hao wameonesha kiwango kikubwa katika mazoezi yao na wanatarajia kuwa watawasaidia kufanya vizuri msimu ujao kama wataingia nao mkataba wa kuitumikia timu hiyo ngeni kunako ligi kuu.

Tumeanza kambi kwa takribani majuma matatu sasa, tupo na wachezaji wengi waliotusaidia kupanda ligi, tumewaacha wachezaji sita tu, na jambo zuri ni kuwa tupo na wachezaji kutoka Afrika Magharibi ambao tunaangalia uwezo wao, wanamaendeleo mazuri pengine tutawasajili kwa ajili ya msimu ujao, nimeambiwa mmoja ni mdogo wake na Didier Drogba” Josiah amesema.

Vilevile Josiah amesema wanachotaka kufanya ni kuhakikisha wanasajili wachezaji ambao watawasaidi katika msimu ujao wa ligi, na hawataangalia majina makubwa bali uwezo wake anapokuwa uwanjani.

“Hatutaka kusema ni wachezaji gani mpaka sasa tumepanga kuwasajili, lakini tayari tumeanza mazungumzo na wachezaji ambao tuliwaangalia msimu huu, lengo letu ni kuwa na kikosi ambacho wachezaji watakuwa wanaelewana, unaweza kusema tutamsajili mchezaji huyu ukawaaminisha mashabiki na ushindwe kufanya hivyo, ndio maana nashindwa kusema ni nani ambaye tutamsajili kwa sasa, tusubiri,” amesema.

Biashara United ni miongoni mwa timu sita ambazo zitacheza ligi kuu soka Tanzania Bara msimu ujao, nyingine ni pamoja na Alliance School ya Mwanza, Coastal Union ya Tanga, KMC, JKT Tanzania na African Lyon zote za Dar es Salaam.

Sambaza....