Blog

Moro Lamine wa juzi, jana na leo

Sambaza kwa marafiki....

MORO Lamine. Pande moja la baba katika ukuta wa Yanga. Ndiye anayeficha aibu za wachezaji wenzake pale nyuma. Ni mwanaume wa shoka.

Kwanza mchezaji, pili ana kimo, tatu anazungumza na kutoa maelekezo jinsi kazi ya ulinzi inavyotakiwa kufanywa kiufanisi. Bonge la beki.

Stori yake kuja Dar es Salaam mara ya kwanza imejaa mikasa ya kusisimua. Miezi sita iliyopita alikuja jijini kama kuku mgeni aliyekuwa na kamba yake mguuni. Hukupata shida kumtambua kama ni mtu mpya jijini. Alikuwa mkimya aliyependa kuinamisha chini shingo yake. Hakukuwa na mtu anayemjua, aliujua mpira na kujijua mwenyewe tu.

Lamine Moro (mwenye jezi nyekundu) katikati akipiga mpira mbele ya mchezaji wa Afc Leopard

Ni Simba waliomleta Moro mbele ya mboni zetu katika michuano ya SportPesa. Nasikia walimleta kwa majaribio. Sijui kilichotokea mbeleni. Moro akaamua kukusanya kilicho chake na kuondoka.

Moro aliondoka nchini nyuma akiacha mjadala mzito vinywani mwa mashabiki wa Simba na viongozi wao katika korido za jengo la Msimbazi. Kila mmoja alikuja na tathimini juu yake. Ni kama alipita bundi hivi, ghafla akatoweka vinywani mwao. Hakuzungumziwa tena. Stori yake na Simba ikaishia hapo. Huyo ni Moro wa juzi. Bado wa jana na leo.

Ligi yetu ikaisha Simba wakawa mabingwa. Usajili ukafunguliwa. Tetesi za Moro kusajiliwa Yanga zikaanza. Stori zilianzia mitandaoni, zikahamia kwenye blogs, mwishoni magazeti yetu yakaja kututhibitishia. Hatimaye picha zake Uwanja wa Ndege kutua Yanga zikazagaa kila pembe ya nchi.

 

Alipita katika mlango ule ule alioupita mara ya kwanza alipokanyaga ardhi ya Tanzania. Pembeni ya mlango huo kulikuwa na mlango mwingine uliosomeka In. Trip hii ule wa mlango wa In aliupa kisogo. Alienda katika mlango ulioandikwa Exit. Hatimaye Moro ndani ya Dar es Salaam.

Safari hii hakuonekana tena kuwa mgeni kwa baadhi ya mambo kiwanjani pale. Aliwajua wenyeji wake. Aliwafuata waliko wakapakiana katika gari wakaondoka. Rasmi akaanza maisha na Yanga.

Akasaini mkataba. Timu ikaenda zake kambini Morogoro. Mara nyingi kambini kunakuwa sehemu tulivu katika maandalizi. Hakuna presha. Ni huko Moro alikoanza kuonyesha yeye ni mchezaji wa daraja gani. Alifanya mazoezi chini ya msaidizi wa Zahera, Mwandila. Pole pole akaanza kukonga.

Aliwateka akawateka na kuwateka. Yanga wakaanza nyodo. Zilipokuja zile mazoezi mechi, Moro alikuwa kivutio. Yanga ikarudi zake Dar es Salaam kucheza na Kariobang Sharks. Hapa Moro alicheza karibu zaidi na watu Yanga Tanzania nzima kutokana na mechi kurushwa na Azam Tv. Ndani ya Uwanja Taifa, Moro aliuwasha kisawa sawa.

Kutokea hapo anabadilishiwa mtu wa kucheza nae. Kuna siku atacheza na Ally Sonso, siku nyingine Kelvin Yondani. Ni Sonso na Yondani wanaobadilishana nafasi ya kucheza nae. Moro yuko kama alivyo. Huyu ni Moro wa jana. Bado leo.

Rejea kutazama pambano la Yanga na Township Rollers kule ugenini Botswana. Moro ni Defender wa kileo. Washambuliaji wa Township walicheza jinsi alivyotaka yeye. Aliwatuliza kuanzia chini mpaka juu. Alikuwa akimtuma Yondani kazi zote nyepesi, kazi zote ngumu ungemuona mwenyewe.

Mechi inaisha Yanga imeshinda 1-0. Hii ni mechi waliyofanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Walitaka kukaba wasifungwe wakafanikiwa na walitaka kufunga bao wakafunga. Hii ni kazi ngumu inayofanywa na watu wachache. Haiwezi kufanywa na kila mtu.

Kama Simba wasingekuwa na miluzi mingi kwake inawezekana ndio angekuwa muarobaini wao katika ulinzi hivi sasa. Tena wangempata kiunafuu. Leo timu yao imebaki kufungwa mabao yale yale. Hawafungwi mabao mapya. Ulinzi wa kati ni tatizo kubwa Simba. Lakini nani anayejali?

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.