Sambaza....

Macho yangu yalikuwa makini sana tulipokuwa kwenye dimba la Nambole. Dimba ambalo ni gumu sana. Nilijaribu kuiweka presha pembeni na kuamua kuwatazama vizuri Taifa Stars.

Na ikizingatia ilikuwa mechi ya kwanza ya kocha kutoka Nigeria Emmanuel Amunike, nilitamani kumuona anawezaje kucheza katika mechi za ugenini.

Mechi ambazo hana mashabiki wengi, hana uzoefu na uwanja husika. Nashukuru Mungu nilimwelewa sana kocha Emmanuel Amunike katika mechi ile kwa sababu alijielezea vizuri sana namna ambavyo anaweza akacheza mechi za ugenini.

Alitumia mfumo wa 3-4-3. Mfumo ambao ulimlazimu atumie wachezaji saba wenye asili ya kujilinda ndani ya kikosi chake. Aliweka mabeki watatu wa kati (Abdi Banda, Agrey Morris na Mwantika).

Huku akitumia Wingbacks, upande wa kulia akimtumia Hassan Kessy na upande wa kushoto akimtumia Gadiel Michael na akatumia viungo wawili wa kati wenye asili kubwa ya kujilinda, ambao ni Mudathir Yahaya na Frank Domayo.

Kujaza wachezaji saba wenye asili ya kujilinda ilikuwa na maana kuwa alikuwa ameenda Uganda kwa ajili ya kujilinda ili asifungwe. Hivo matokeo ya sare au kushinda kwa kutumia mashambulizi ya kushtukiza ndicho kitu ambacho alikuwa anakitaka.

Nilimwelewa kwa asilimia kubwa na alifanikiwa kwa kiwango kikubwa. Nikamsubiri kwenye mechi dhidi ya Cape Verde. Nilitamani pia atajioneshaje kwenye mechi hii.

Alichokifanya Uganda ndicho alichokifanya Cape Verde. Alijaza tena wachezaji saba wenye asili ya kujilinda. Kikosi kilikuwa kile kile kwa asilimia kubwa. Tulishuhudia ingizo jipya la Himid Mao eneo la Frank Domayo.

Nilijua kitu ambacho anakitafuta ndicho kile ambacho alikipata katika mechi dhidi ya Uganda. Alitaka matokeo chanya, hakutaka kufunguka sana kwa sababu alikuwa ugenini.

Alitaka timu yake iwe chini kwa muda mrefu sana huku akifanya mashambulizi ya kushtukiza na hii ni kwa sababu alikuwa katika uwanja wa ugenini. Hivo ilikuwa lazima ajihami ndiyo maana hata katika orodha ya wachezaji wa akiba hakukuwepo kiungo. Wengi walikuwa mabeki.

Alifanikiwa kwenye mechi dhidi ya Uganda, lakini hakuweza kujifunza kitu kimoja muhimu sana katika mchezo. Nacho ni njia mbadala, siku zote timu huenda na njia mbadala katika mchezo husika.

Ni ngumu kwa kocha kuruhusu timu iende na njia moja tu ya kupata matokeo, je njia hiyo isipofanikiwa kukupa matokeo unayoyataka?. Na hiki ndicho kitu ambacho kilitokea kwa Emmanuel Amunike, njia yake ya kwanza haikumwezesha yeye kupata matokeo.

Na kibaya zaidi orodha ya wachezaji wake wa akiba ilikuwa inaonesha dhahiri kuwa hakuwa na njia mbadala kwa sababu hakukuwepo na wachezaji wa kubadili mbinu.

Wachezaji wengi walikuwa wana asili ya kujilinda tu. Tangu mechi dhidi ya Uganda, wachezaji wa mbele (Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Simon Msuva) walikuwa wanashuka chini katikati kuchukua mipira.

Hawakuwa na viungo wa kuwachezesha kwa sababu asilimia kubwa ya viungo walikuwa wanakaa chini kujilinda. Hivo ilikuwa inawalazimu kina Mbwana Samatta kushuka chini katikati kuchukua mpira.

Kwa kifupi kulikuwa na uwazi mkubwa kati ya eneo letu la kiungo mchezeshaji na eneo la ushambuliaji. Nilitegemea hiki kilionekana kwenye mechi dhidi ya Uganda. Nikawa nategemea kitafanyiwa kazi kwenye mechi dhidi ya Cape Verde, lakini ikawa tofauti na mategemeo yangu.

Na ndiyo maana tulipofungwa na Cape Verde hatukuwa na njia mbadala kwetu sisi kusawazisha goli kwa sababu tulikuwa na aina ya wachezaji ambao wasingeweza kubadili mbinu ya mchezo husika.

Tulikuwa na wachezaji ambao walikuwa wanakaa chini muda mrefu sana na kibaya zaidi hatukuwa na kiungo tena katika orodha ya wachezaji wa akiba. Hivo mechi iliisha kwetu baada ya kufungwa zile goli mbili.

Tusingekuwa na uwezo tena wa kufanya chochote kwa sababu hatukuwa na kiungo mchezeshaji ndani ya timu. Kiungo ambaye angetengeneza nafasi nyingi ndani ya uwanja na ikiwezekana kuhusika katika ufungaji wa magoli.

Hapo ndipo umuhimu wa Ibrahim Ajib na Shiza Ramadhan Kichuya ulipokuja. Hawa ndiyo watu ambao wangeweza kuleta utofauti katika mechi hii.

Tunaweza kuwatupia lawama kina Thomas Ulimwengu kwa kutotupa magoli lakini tujiulizeni ni nani ambaye angeweza kuwa mtengezaji wa nafasi hizi?, kwangu mimi nadhani hata kama angeingizwa John Bocco acheze mbele ya Kina Himid Mao na Mudhathir Yahaya ilikuwa kazi bure tu.

Tulitakiwa kuwa na wachezeshaji haswaa, wenye ubunifu katika kutengeneza nafasi za kufunga pamoja na uwezo wa wao kufunga wenyewe. Hawa watu hawapo katika orodha ya wachezaji wa timu ya taifa.

Na tunaenda kucheza dhidi ya Cape Verde tukiwa hatuna hawa watu kabisa, tunajiwekea mazingira magumu sana ya kushinda hii mechi. Hata kama tutashinda, ushindi wetu utakuwa ushindi wa kuhangaika sana kwa sababu hatuna wapishi wazuri wa kutupikia magoli ambayo tunayahitaji katika mchezo huo.

Ndiyo maana nafsi yangu inatamani sana kusikia leo kocha Emmanuel Amunike amewaongeza Ibrahim Ajib au Shiza Ramadhani Kichuya katika kikosi chetu kwa sababu hawa wanauwezo wa kufanya kazi ambayo inahitajika kufanywa siku ya jumanne.

Wanauwezo wa kutengeneza nafasi za magoli, wanauwezo wa kuongeza nguvu kubwa sana wakati timu ikiwa inashambulia. Na kwa sababu katika mechi zote mbili zilizopita tulikuwa na uwazi kuanzia eneo la kiungo wa kati na eneo la mbele, hawa wawili, mmoja wao anaweza akapunguza uwazi huo na akawa anatengeza nafasi za kufunga pamoja na kufunga yeye.

Na hii itawasaidia kina Mbwana Samatta kutokuwa wanashuka chini katikati kuchukua mipira na kutowaka uhuru mabeki wa timu pinzani kuanzisha mahsmbulizi wakiwa huru bila bugudha.

Sambaza....