Sambaza....

Nahodha wa kikosi cha KMC, Yusuph Ndikumana, ameitaja mechi dhidi ya Azam FC kama mechi muhimu zaidi kwao kwa sasa, hasa ukiangalia nafasi ambayo wapo na uhitaji wao alama tatu muhimu Ili kujinasua sehemu ambayo wapo.

Ndikumana, mchezaji wa zamani LLB Academy ya Burundi na Mbao FC ya Mwanza amesema wanatambua ugumu wa mchezo huo kutokana na ubora wa timu zote mbili lakini watajitahidi kadri wawezavyo Ili kupata matokeo chanya ya alama tatu.

“Ni mwendelezo wa ligi, nafikiri ni mechi muhimu kwetu ukizingatia nafasi ambayo tupo tunahitaji matokeo na tumejiandaa vizuri, Azam ni timu nzuri timu ambayo ipo nafasi nzuri na sisi ni timu nzuri vile vile, na bado tunandoto ya kufanya mambo mazuri, tulipata hizo pointi zitatuweka kwenye nafasi nzuri zaidi,” Ndikumana amesema.

Mpaka sasa KMC imefungwa michezo mitatu na kutoka sare katika michezo nane Hali inayoonesha bado safu ya ulinzi inafanya kazi nzuri, hivyo Ndikumana ameahidi kuendelea kuiongoza vyema safu hiyo kwa kuhakikisha wanawazuia wachezaji bora wa Azam kama Obrey Chirwa na wengineo.

“Cha muhimu kwanza ni kuwaheshimu, Baada ya hapo kila kitu kitakuwa sawa, hatuwezi kuwachukilia Poa kwa sababu Sio wachezaji wa level ya chini, ni wachezaji Wakubwa, wachezaji wazuri, nafikiri tahadhali yetu itatusaidia kuweza kucheza nao kwa umakini sana na kuweza kuwadhibiti,” amesema.

KMC itashuka dimbani Jumatatu ijayo ya Disemba 10 kucheza mchezo wao wa 15 dhidi ya Azam huku kwa sasa wakiwa katika nafasi ya 11 na alama zao 17.

Sambaza....