Sambaza....

Miaka kumi imepita, miaka ambayo ilitawaliwa na wafalme wawili wa mpira duniani.

Wafalme ambao wametufanya tujivunie kufuatilia mpira. Wafalme ambao wameleta ladha tamu kwenye mpira wetu.

Ladha ambayo imechagizwa kwa kiasi kikubwa na ushindani wao.

Wamefanikiwa kuigawa dunia mara mbili, upande mmoja wa dunia ni wa Lionel Messi na upande mwingine wa dunia ni wa Cristiano Ronaldo.

Hizi ndizo dini mbili ambazo mashabiki wote wa mpira duniani huabudu, nusu ya mashabiki huabudu Jumamosi kwa Lionel Messi na nusu ya mashabiki waliobaki huabudu kwa Cristiano Ronaldo.

Hii ni kwa sababu walitumia muda wa miaka kumi kuweka alama zenye kuheshimika, alama ambazo zina nguvu sana kwenye mpira wetu.

Ndiyo maana hata tunzo ya Ballon D’or wamekuwa wakibadilishana wao kwa muda wa miaka kumi.

Miaka mitano kachukua Lionel Messi na miaka mitano iliyobaki kachukua Cristiano Ronaldo.

Tangu waichukue kutoka kwa Ricardo Kaka hakuna mchezaji ambaye kafanikiwa kuichukua zaidi ya hawa miamba wawili.

Wamevunja rekodi nyingi sana na wameweka rekodi nyingi sana, rekodi ambazo zinaweza kuwa mzigo mzito kwa kizazi kijacho kuja kuzivunja.

Kwa kifupi hawa ndiyo nembo ya mpira duniani kwa sasa, ni ngumu kutaja neno mpira wa miguu bila majina haya mawili kuja kichwani mwako.

Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ndiyo mpira, na mpira ndiyo Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Ni ngumu kuikataa hii kauli kwa sababu wamecheza miaka kumi mfululizo bila kushuka kiwango.

Wamefanikiwa kuvishikilia viwango vyao, kila uchwao wanaonekana wapya, wana njaa na hawajifikiria kushiba mafanikio ambayo wameyapata.

Upya wao huonekana kila jua linapochomoza, kuna wakati mwingine tulitamani kuona mchezaji mwingine ambaye angeingia katikati ili kutoa upinzani.

Tulihisi Xavi na Iniesta wangeweza kusimama katikati yao na kuichukua Ballon D’or lakini ilikuwa tofauti na matamanio yetu.

Xavi na Iniesta wameshaondoka, hawatarudi tena kwenye soka la ushindani ni ngumu tena kuweka matamanio yetu juu yao.

Hata Antoinne Griezmann naye tulimuona anaweza kuifanya kazi ambayo Frank Ribbery alishindwa.

Umri unaweza ukawa unamhukumu kwa sasa Frank Ribbery, ila huyu alikuwa na nafasi ya kuingia katikati lakini ikawa bahati mbaya.

Tunaweza kumtegemea Antoinne Griezmann? Au tumsubiri Mbappe, au bado tuwe na imani kuwa Neymar ndiye mtu sahihi kutoa upinzani kwa hawa watu wawili?

Alikimbia kivuli cha Lionel Messi pale Barcelona, sehemu ambayo ilikuwa inampa nafasi kubwa kwake yeye kubeba Ballon D’or.

Akaenda PSG, sehemu ambayo inatoa tafasri halisi ya neno “pesa ina nguvu kubwa”.

Tulitegemea huku atakuwa huru na anaweza kucheza katika kiwango kikubwa ambacho kinaweza kumweka katikati ushindani wa Ballon D’or.

Moja ya kitu ambacho kimewabeba sana Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kwa miaka kumi iliyopita ni ukomavu wa maamuzi ndani ya uwanja.

Wanajua kutumia ipasavyo nafasi ambazo wanazipata, ndiyo maana huwa tegemeo katika timu zao katika nyakati ngumu.

Kipindi ambacho timu zao zimebanwa wao (Cristiano Ronaldo na Lionel Messi) huibuka kama wakombozi kwa sababu ya ukomavu wa maamuzi kwenye miguu yao.

Ni ngumu kubeba Ballon D’or kama huna uwezo wa kuibeba timu yako katika nyakati ngumu.

Lazima uibuke shujaa, uwe tofauti na wenzako, uwe sababu ya kuitwa mhimili wa timu.

Hapa ndipo Neymar anakwama. Mechi ya mwisho kwake yeye kucheza katika michuano ya klabu bingwa ulaya ilikuwa mechi kati ya PSG na Realmadrid kabla ya jana kucheza dhidi ya Liverpool.

Mechi dhidi ya Realmadrid alionesha utoto mwingi wakati akiwa na mpira, hakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yenye manufaa ndani ya timu.

Mara nyingi alikuwa mbinafsi anajiangalia yeye badala ya kuiangalia timu.

Hakuwa chanzo cha timu kufanya vizuri. Ila alishiriki kuigandamiza timu kutokana na maamuzi yake ambayo hayajakomaa.

Heshima ya mchezaji mara nyingi hupatikana kwenye mechi kubwa. Hapa ndipo ushujaa unapopatikana kwa sababu mchezaji anakuwa anapambana na mashujaa.

Jana kwenye mechi kati ya Liverpool na PSG , Neymar hakuweza kuwa shujaa na huu ni mwendelezo wake wa kutokufanya vizuri kwenye michuano mikubwa na mechi kubwa kama hizi.

Hapa ndipo tofauti yake na kina Cristiano Ronaldo na Lionel Messi inapoonekana.

Wao huwa wakomavu kiakili na kwenye miguu lakini Neymar hana ukomavu kwenye miguu na kwenye akili.

Ni ngumu sana kachukua Ballon D’or kama huna ukomavu wa kimaamuzi ndani ya uwanja.

Kukosa kwa maamuzi chanya ndani ya uwanja hasa hasa kwenye mechi kubwa kunanifanya nimuone Neymar akipiga hatua moja nyuma kuiogopa Ballon D’or.

Hana njaa tena ya kachukua Ballon D’or kama kipindi kile anakuja Barcelona. Kwa sasa anaikimbia Ballon D’or badala ya kuikimbilia.

Ameshasahau kabisa kuwa moja ya ndoto yake ambayo alikuwa akiiota kwa kipindi kirefu na bado hajaitimiza mpaka sasa ni yeye kubeba Ballon D’or.

Sambaza....