Mataifa Afrika

Pamoja na ushindi, huu ulikuwa udhaifu wa Taifa Stars

Sambaza kwa marafiki....

Baada ya miaka 39, kwa mara ya kwanza Jana Tanzania tumefanikiwa kufuzu kwenda Afcon.

Hii ilikuwa ni furaha kubwa sana katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, kwa sababu tu tulikuwa na hamu ya kuona hiki kitu kikitokea.

Ni mfumo gani ambao mwalimu Emmanuel Amunike aliingia nao Jana ?

Kwenye mechi ya Jana Tanzania walikuwa wanacheza 4-4-2 lakini yenye umbo la DIAMOND. Kwa sababu wachezaji wa pembeni walikuwa wanashuka katikati ya uwanja kuongeza idadi ya viungo wa kati ndani ya uwanja.

Kuna wakati Fareed Mussa alikuwa anakaa pembeni na kushuka katikati ya uwanja kuungana na kina Mudathir Yahaya na Erasto Nyoni katika eneo la katikati.

Pia, Mbwana Ally Samatta naye alikuwa anashuka katikati, kwa hiyo wakati wakiwa wanakuwa katikati walikuwa wanatengeneza Diamond shape kwenye mfumo wa Emmanuel Amunike.

Upi ulikuwa ubora wa Tanzania ?

Taifa Stars ilikuwa inategemea eneo la pembeni mwa uwanja kwa ajili ya kufanya mashambulizi kwenye mechi ya Jana.

Na ukitazama magoli yote yalitokea pembeni. Goli la kwanza, Gadiel Michael katoka pembeni akapiga krosi ambayo ilizaa goli.

Goli la pili, Mbwana Ally Samatta katokea pembeni mwa uwanja na kusababisha penati ambayo ilizalisha goli la pili.

Goli la tatu nalo, John Bocco katoa krosi akiwa pembeni mwa uwanja na kusababisha goli la tatu.

Alifanyaje Emmanuel Amunike mpaka ikawa hivi ?

Kwanza, wachezaji wote wa mbele hawakutakiwa kucheza eneo moja tu la karibu na kumi na nane, wote walikuwa hawakai muda mrefu eneo hilo.

Simon Msuva alikuwa anakuja kulia pembeni, ambapo alikuwa anaongozewa nguvu na John Bocco ambaye naye alikuwa anatokea kulia.

Mbwana Ally Samatta alikuwa anatokea pembeni kushoto, huku alikuwa akisaidizana na Fareed Mussa.

Samatta akifanya yake

Kwa hiyo, wakati upande mmoja ukiwa na mpira. Mfano, upande wa kulia ulipokuwa na mpira, labda John Bocco alipokuwa na mpira, kina Simon Msuva, Mbwana Ally Samatta walikuwa wanawahi haraka eneo la kumi na nane.

Pia mabeki wa pembeni, Gadiel Michael na Hassan Kessy walikuwa wanasukuma vizuri mashambulizi kwenye hii mechi.

Kwa hiyo ubora wa Taifa Stars katika mechi ya jana ulikuwa pembeni, na hiki ndicho kilichosababisha Taifa Stars kushinda (kiufundi).

Upi ulikuwa udhaifu wa Taifa Stars?

Emmanuel Amunike amekuwa muumini wa dhehebu la kujizuia. Huwezi kumbadilisha. Na siyo dhambi kwenye hilo.

Jana alikuwa na viungo wawili ambao wana asili ya kujizuia (Erasto Nyoni na Mudathir Yahaya). Kitu ambacho kilisababisha timu icheze mipira mirefu.

Timu ilikuwa inacheza mipira mirefu kwa kuipeleka pembeni , sehemu ambayo ndiko kulikuwa ubora wa timu.

Nyoni akitetema!

Sasa kama Uganda wangeamua kuhakikisha pembeni pawe pagumu kwetu sisi kupita bila shaka tungekuwa na asilimia ndogo sana ya kushinda.

Kwa sababu hatukuwa na njia mbadala ya kuzalisha mashambulizi zaidi ya kutegemea eneo la katikati mwa uwanja.

Kama kungekuwepo na kiungo wa ushambuliaji katika mechi hii kungekuwa na uwezekano mkubwa kuwepo na njia mbili za kutengeneza nafasi za magoli (pembeni na katikati ya uwanja).

Mwisho.

Dakika alizoingia Faisal Fei Toto zilikuwa na maana kubwa sana. Timu ilibadilika, mipira ikawa inapita katikati mwa uwanja kwenda mbele, ile mipira mirefu haikuwepo tena.

Na Faisal Fei Toto alicheza kiungo cha juu, huku nyuma kukiwa na Erasto Nyoni, Mudathir Yahaya yeye akiwa mbele yao.

Kuna funzo hapa. Faisal anaweza kuingizwa na timu ikawa na njia mbili za kupata magoli (katikati na pembeni), huku mbele ya Faisal wakicheza kaka zao watatu Bocco , Samatta na Msuva.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.