Sambaza....

Ukiulizwa ni nani alimuua Goliath? Jibu sahihi litakuwa ni Daudi. Zamani sana hata kizazi cha sasa hakikuwepo bali ni simulizi zilizopo katika vitabu vitukufu lengo ni kutufunza kuwa “ tusiwe na dharau” kwa watu tusiowajua hata kama mionekano yao haionyeshi dalili za ushindi na uthabiti wa hali.

Dunia ya michezo hasa KANDANDA imebadilika sana, mashabiki wamekuwa wakifurahia hadithi za ushindi wa timu vimeo “ underdog” kuliko simulizi za ushindi kwa timu kubwa. Huenda hujanielewa bado, usijali nitakupa tafsiri yake.

Nikurudishe nyuma kidogo hadi mwaka 2002 katika mashindano ya Kombe la dunia, yalifanyikia nchini Korea kusini.  Timu ya Korea Kusini ambao ndio walikuwa wenyeji katika mashindano hayo walifanya maajabu pale walipothubutu kufika hatua ya nusu fainali.

Katika hatua ya makundi Wakorea walianza kwa kuibamiza 2-0 Poland, kisha wakatoka sare 1-1 na Marekani, kwa alama walizokusanya na kundi jinsi lilivyo walihitaji ushindi dhidi ya Ureno ili kufuzu. Kumbuka kipindi hicho Ureno ina mtu kama Luis Figo, ambaye ndiye aliyekuwa mchezaji bora wa dunia kipindi hicho na kuifikisha Ureno nusu fainali za Kombe la Mataifa ulaya (EURO) mwaka 2000. Lakini Wakorea walifanikiwa kuwachapa Wareno goli 1-0 na kuingia hatua ya 16 bora.

Baada ya hapo, Wakorea wakaichapa Italy 2-1 katika muda wa nyongeza kwa goli la ajabu la Ahn Jung-Hwan’s na kumfanya mchezaji huyo kufukuzwa katika klabu yake ya nchini Italy iliyoitwa Perugia.

 Baada ya hapo, Wakorea wakaendeleza moto wao  kwa kuichapa Hispania kwa mikwaju ya penati lakini walikuja kutolewa na Ujerumani hatua ya Nusu Fainali.

Kwa maneno ya kawaida Korea Kusini unaweza kuiita “Underdog” aliyefanikiwa.

Ukiachana na mechi hiyo kuna mechi nyingi ambazo zimeuacha ULIMWENGU WA SOKA mdomo wazi, ikiwemo timu ya Iceland katika mashindano ya Euro mwaka 2016, nakumbuka ilikuwa kundi moja na Ureno,. Austria, na Hungary lakini ilifanikiwa kupenya 16 bora baada ya kuifunga Austria na kutoa sare mechi mbili za Ureno na Hungary. Kisha wakaibamiza England goli 2-1 licha ya kufungwa goli la mapema kwa mkwaju wa penati.

Hadi hatua hiyo, Iceland walikuwa “Underdog” waliotia matumaini na kuwashangaza wengi kabla ya kubanguliwa goli 5-2 wakitokea nyuma kwa goli 4-0.

Timu nyingine ni Ureno katika mshindano hay ohayo ya Euro 2016, kuingia katika hatua ya 16 bora ilikuwa ni kwa nafasi ya Upendeleo “best looser” lakini baada ya hapo ureno ilionyesha matumaini  kuanzia safu ya ulinzi kwa golikipa, kiungo, chini ya Renato Sanchez na William Cavalho, na ushambuliaji chini ya Christiano Ronaldo na Nani.

ChristianoRonaldo, Mreno aliyeisaidia timu yake ya Taifa kushinda taji la Euro 2016.

Ureno ilifanikiwa kuingia fainali na kisha kubeba taji hilo kwa ushindi wa goli 1-0 katika dakika 120. Goli hilo liliwekwa Kimyani na Eder. Ni taji lao la kwanza kwa timu ya taifa, ikiwa ni miaka 12 tangu walipokosa kulichukua mwaka 2004 wakiwa ndio waandaaji.

Ukiachana na Ureno “Underdog” wengine waliofanya vizuri ni Cameroon katika kombe la dunia la mwaka 1990, Ugiriki mwaka 2004 katika mashindano ya EURO.

Nisingependa kuisahau Monaco ya msimu wa mwaka 2016 na 2017 katika mshindano ya Klabu Bingwa Ulaya na ligi kuu ya Ufaransa “Ligue One” chini ya moto mkali wa Kylian Mbappe, Thomas Lemar, Bernardo Silver na Benjamin Mendy.

Kylian Mbappe. Mchezaji wa zamani wa Monaco na sasa ni wa PSG.

Mwisho ni msimu wa 2015/2016 kwa klabu ya Leicester City kuonyesha maajabu yake kwa kubeba ndoo, katika ligi ngumu ya Uingereza. Bila kutarajiwa wala kupewa nafasi, Leicester walinyanyua kwapa msimu huo.

Katika dunia ya soka neno “Underdog” hutumika sana lakini maana yake ni timu ambayo katika mashindano inatarajiwa kutoonyesha ushindani wowote yaani ni rahisi kufungwa. Na ile timu inayotarajiwa kushinda inaitwa “top dog” na endapo ikitokea timu “Underdog” imeshinda matokeo yake huwa ni ya kushangaza.

Katika ulingo wa soka kumejaa vituko na vibweka vingi kiasi kwamba wengine wanatamani kujitoa hata uhai kwa kile kinachoitwa Mapenzi ya soka na timu. Mapenzi haya huleta kitu kinachoitwa furaha pale timu inapofanya vizuri na huleta huzuni na majonzi wakati timu inapofanya vibaya.

Acha nikuulize swali hili, hivi zikicheza timu mbili, moja ni “Underdog” na nyingine ni kubwa wewe utafurahi zaidi kama timu gani ikipata ushindi? Jibu lako lipime kwa kiwango cha msisimko, yaani matokeo hayo yanasisimua? Kama yanakusisimua basi hiyo ndio furaha ya kushangilia. Ukweli ni kwamba ushindi wa “Underdog” unaleta msisimko, kushangaza “exciting” na kufurahisha.

Kwanini tunajipa tabu kuzishabikia timu “Underdog” katika mashindano? Hili ni suala la kisaikolojia, ukatae ukubali lakini ukweli ni kwamba akili ya binadamu hupenda kufurahia matokeo ya kushangaza.

Tafiti za mwaka 1991 zinaonyesha kuwa mashabiki wengi wa soka hupenda kuzipa timu ndogo matumaini ya kupata ushindi ili kujihakikishia furaha katika mioyo yao. Hili linathibitishwa na takwimu za hivi karibuni za mwaka 2007, ambapo watu 71 walihojiwa, kwa kuulizwa wangependa timu zipi zipate ushindi zikikutana kati ya timu kubwa na ndogo, na asilimia kubwa walipendelea ushindi kwa timu ndogo “Underdog”.

Kiufupi kabisa naweza kusema, timu “Underdog” huwa na mvuto kwa mashabiki, na mioyo  ya mashabiki wa aina hii inaamini kuwa ushindi kwa timu wanazozitaka huleta ushindi katika nafsi zao. Yaani mfano timu yako ikishinda na hata wewe unajiona Mshindi.

Mashabiki wa “Underdog” ukiwauliza nini maana ya ushindi ? basi watakujibu hivi “USHINDI NI FURAHA ISIYOTARAJIWA” ! yaani ushindi kwa “Underdog” ni mara kumi kwa ushindi wa timu kubwa, na ndio maana Liverpool walipofungwa na Wolves ikawa ndio habari kubwa kuliko hata Wolves wangefungwa na Liverpool.

Sambaza....