Mataifa Afrika U17

Ajax, Manchester City wapigana vikumbo kwa Kelvin John.

Sambaza....

Jarida maalumu la kuripoti michuano ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 inayoendelea hapa nchini, limeripoti kwamba tayari vilabu kadhaa barani Ulaya vimeonesha nia ya kufanya mazungumzo ya awali na walezi ama wazazi wa mshambuliaji wa Tanzania Kelvin John ili kumnyakua.

Jarida hilo limewataja mawakala wa vilabu vya Manchester City na Ajax kuwa ndio ambao wameonesha dhahiri uhitaji wa Kelvin John maarufu kama Mbappe kutokana na aina yake ya uchezaji licha ya Tanzania kupoteza michezo miwili ya kwanza kwenye kundi lake.

“Kelvin John ana sifa nzuri za mshambuliaji wa kati, ana kasi, ujuzi na umakini katika umaliziaji,” Jarida hilo limemnukuu mmoja wa mawakala waliopo jijini Dar es Salaam.

Ila inawezekana kukawa na ugumu wa kupata saini yake kwani kinda huyo mwenye umri wa miaka 16 tayari ameshakuingia makubaliano na klabu ya HB Koge ya Denmark ambapo alikwenda mwaka jana kwa ajili ya kufanya majaribio na kufanikiwa.

Kwa sasa zaidi ya mawakala 20 wapo jijini Dar es Salaam wakijaribu kuangalia vipaji vya watoto wanaotoka kwenye mataifa yanayoshiriki michuano hiyo iliyoanza jumapili ya April 14, 2019.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.