Mwenyekiti wa klabu ya Simba Mo Dewji.
Ligi Kuu

SIMBA SC nayo ni timu ya WANANCHI pia.

Sambaza....

Kuna utaratibu ambao umejengeka kwa watu waliowengi wanaoishi kwenye nchi za dunia ya tatu. Nchi ambazo maendeleo kwao bado yapo kwenye vitabu vya hadithi na siyo kwenye uhalisia.

Utamaduni huu ni wa kudharau sana pesa ndogo. Watu wengi waliokatika dunia ya tatu huwa hawaweki umakini kila wanapopata pesa ambayo huonekano kwao ni ndogo.

Umakini mkubwa kwao huja kipindi ambacho wanapopata pesa kubwa. Na kwa bahati mbaya hata elimu ya kuzitumia ipasavyo hizo pesa kubwa huwa wanakosa.

Tunachane na hiyo mada ya kutumia ipasavyo hela , hii ni mada ya siku nyingine. Tuendelee kuzungumzia tabia za watu wa dunia ya tatu kuhusiana na hela ndogo.

Kwa wao kwenye hela ndogo huwa hawaamini kama wanaweza wakatengeneza kitu kikubwa kwa kutumia hiyo hela ndogo waliyonayo mfukoni.

Tunadharau kiingilio kidogo cha SIMBA, Bhakresa anauza vitu kwa shilingi mia.

Hata katika kuzikimbilia zile ndoto zetu huwa tunasubiria tupate kiasi kikubwa cha pesa ndiyo tuanze kukimbilia ndoto zetu. Nafsi zetu za watu wa dunia ya tatu huwa zinaamini pesa nyingi ndiyo zinaweza kutufanya tupate kitu kikubwa zaidi.

Hapa Tanzania tuna tajiri mmoja anaitwa kwa jina maarufu la Bhakresa. Utajiri wake kwa asilimia kubwa umetokana na yeye kuuza bidhaa ambazo zinawagusa watu wa hali ya kawaida.

Hawa watu ambao wanaonekana wanahali ya kawaida ndiyo hawa ambao kwa asilimia kubwa huwa wanahusika kwenye kununua bidhaa za wafanyabiashara wetu.

Hawa ndiyo wako kwenye mzunguko wa kila siku. Ndiyo maana Bhakresa anauza mpaka bidhaa ya shilingi mia , mita mbili , mia tano , mia saba na bidhaa hizi zinazunguka sana.

Mzunguko wa bidhaa hizi zinafanya Bhakresa auze sana bidhaa zake na ndiyo sababu ya yeye kusimama mpaka leo kuwa tajiri mkubwa hapa Tanzania.

Simba ilitangaza kuwa na kiingilio cha elfu tatu. Kiingilio ambacho kinaonekana ni kidogo sana kwa hadhi ya klabu kubwa kama Simba ambayo inawachezaji wakubwa na wenye thamani kubwa.

Tujiulize swali moja , wapi mashabiki wengi wa mpira wetu ? Aina yao ya uchumi ikoje?

Ni watu wa kawaida tu wenye uchumi wa kawaida ndiyo ambao huenda uwanjani kuangalia mechi. Simba imeweka kiingilio kwa ajili ya hawa watu.

Watu ambao ndiyo walevi wakubwa wa mpira wetu. Wamepewa nafasi ya wao kuja uwanjani. Wamepewa nafasi ya wao kununua bidhaa ya Simba kwa wingi kama ambavyo Bhakhresa alivyotupa nafasi kubwa sisi watu wa kawaida kununua bidhaa zao.

Unaweza kutuandikia kupitia “Tuandikie Usomwe

Sambaza....