Sambaza....

Jana Antonio Conte alirudi kwenye mfumo wake wa msimu uliopita wa 3-4-3, mfumo ambao ulimpa ubingwa lakini msimu huu akawa anautumia mara chache kwa kuhamia katika mfumo wa 3-5-2.

Jana wakati anautumia mfumo wa 3-4-3, kwenye karatasi ulionekana mfumo ambao unafanana na mfumo uliompa ubingwa msimu jana, lakini kiuhalisia kulikuwa na tofauti kubwa sana.

Moja ya sababu ni aina ya wachezaji ambao walikuwepo msimu jana kwenye mfumo wa 3-4-3 na wachezaji waliokuwepo jana kwenye mfumo wa 3-4-3.

Msimu jana Matic alicheza kama Box to Box midfielder akishirikiana na Kante katika eneo la katikati mwa uwanja, lakini jana alikuwepo Bakayoko katika eneo ambalo Matic alikuwepo msimu jana.

Kuna tofauti kubwa sana kati ya Matic na Bakayoko kwenye kutimiza majukumu ya Box to box midfielder.

Msimu jana katika ligi kuu ya England , Matic alifanikiwa kutoa pasi za mwisho saba (7). Matic alikuwa mtulivu kimaamuzi, majukumu yake alikuwa anayatimiza kwa utulivu, kuanzia jukumu la kukaba alipokuwa anashuka mpaka chini katika eneo la Chelsea kumsaidia Kante majukumu ya kukaba mpaka alipokuwa anaenda kwenye box la timu pinzani kushambulia ambapo alikuwa na uwezo wa kutoa pasi za mwisho na kutengeneza nafasi za magoli vizuri.

Hii ni tofauti sana na Bakayoko, kwenye kujilinda anatimiza vizuri majukumu yake, tatizo linakuja pindi timu inaposhambulia, ameshindwa kuwa mtulivu kama alivyokuwa Matic. Hatengenezi nafasi za magoli kwa wingi, hana utulivu katika umaliziaji ndiyo maana anakosa nafasi nyingi za magoli.

Hata mipira mingi anapoteza pindi timu inapohitaji kuwa na mipira, mfano jana kabla ya kupigwa kadi nyekundu alikuwa amecheza dakika 30, ndani ya dakika hizo 30 alipoteza mipira mara 7.

Hii ndiyo tofauti ya kwanza ya mfumo wa 3-4-3 wa msimu jana na 3-4-3 ya mechi ya jana, pili jana Hazard kacheza kama false 9, msimu jana mtu aliyesimama mbele alikuwa Diego Costa ambaye alikuwa mshambuliaji halisi wa kati ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga pamoja na kutengeneza nafasi za kufunga.

Jana Hazard alikuwa amezungukwa na kina Pedro pamoja na Willian, wachezaji ambao walikuwepo hata msimu jana kwenye mfumo wa 3-4-3 lakini tofauti yao ni kwamba msimu jana walikuwa kwenye kiwango kizuri, msimu jana Pedro alifanikiwa kufunga magoli 9 kwenye ligi kuu ila mpaka sasa hivi ukijumuisha magoli ya Pedro na Willian ya msimu huu kwenye ligi kuu ya England, kwa pamoja wote wawili hawafikishi idadi ya magoli aliyofunga Pedro msimu jana.

Jana Hazard alikuwa anaonekana peke yake akipambana kule mbele huku akipata msaada hafifu kutoka kwa Pedro na Willian.

Je kulikuwa na ulazima kwa Conte kumwanzisha Olivier Giroud?

Hapana shaka kulikuwa na ulazima, Olivier Giroud anahitaji muda kutendea haki ya krosi za Chelsea.

Msimu huu Chelsea ni timu ya pili ambayo imepiga krosi nyingi ikiwa imepiga krosi 393 nyuma ya Manchester United iliyopiga krosi nyingi.

Kati ya huduma ambayo Olivier Giroud huifurahia ni mipira ya juu, ambapo mpaka sasa katika miaka yake mitano katika ligi kuu ya England amefanikiwa kufunga magoli 27 kwa kichwa.

Kulikuwa na ulazima wa kumwanzisha mapema ili kupokea huduma hii ambayo Chelsea inaonesha wako vizuri kwenye utoaji.

Je, Zappacosta alistahili kuanza eneo la Marcus Alonso?

Hapana shaka jana upande wa kushoto kulikuwa na upungufu wa krosi nyingi kutokana na Zappacosta kucheza kama wingback left, eneo ambalo tumezoea kumuona Marcus Alonso akilitumikia kwa ufasaha mkubwa na jana alikosekana kwa kiasi kikubwa na Chelsea walihitaji huduma yake katika mchezo wa jana.

Andreas Christensen jana kaanzia benchi, je David Luiz alifanikiwa kukaa vizuri katika eneo la nyuma?

mara ya mwisho kwa David Luiz kuanza katika kikosi cha Chelsea kwenye ƙligi kuu ya England ilikuwa October mwaka jana. Jana alionekana kukosa sharpness kwenye timu kiasi kilichopelekea Chelsea kutengeneza space eneo la nyuma.

Space ambazo kina Gerard Deulofeu kuzitumia vizuri na kuiadhibu Chelsea.

Eneo la nyuma la Chelsea jana lilikuwa linauwazi sana walipokuwa wanashambuliwa.

Jana Antonio Conte hakuonesha kuhamasisha kama ilivyokawaida yake, hakuwa anashangilia pindi timu ilipofunga goli, lugha ya mwili wake ilikuwa inaonesha kuwa muda wowote anaweza asiwe kocha wa Chelsea tena.

Katika mechi 10 zilizopita Antonio Conte amefanikiwa kushinda mechi mbili tu, matokeo ambayo yanaonesha kabisa Antonio Conte hali yake ni mbaya katika timu ya Chelsea.

Sambaza....