Sambaza....

Asubuhi ya leo tulipata taarifa za Kuitwa kwa timu ya Taifa pale Ikulu, wapenzi wanamichezo wote walikuwa na shauku kujua kuna jambo gani. Ingawa tulijua ni kuhusu safari yetu ya Cameroon 2019, lakini shauku ilikuwa kubwa kujua Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli ataongea nini.

Hii ni sehemu ya taarifa kutoka Ikulu kupitia mkurugenzi wa habari wa Rais .

“Nawapa Millioni 50 kwa ajili ya safari ya Lesotho, fedha hizi zitumike kwa ajili ya wanaotakiwa kusafiri tu, sio mambo ya wachezaji 15, viongozi wasindikazaji 30. Haya mambo yafikie mwisho.” – Rais Magufuli

“Sitaki ‘excuse’ yoyote”

“Nitasikitika sana kama tutarudi kutoka Lesotho tumefungwa halafu tuanze visingizio vya chakula kibaya au kuna altitude kubwa. Hii ni vita na lazima tuishinde.” – Rais Magufuli

Hili neno hakika ni muhimu kwa benchi la ufundi na wachezaji kuelekea Lesotho. Ametuwakilisha wapenzi wote wa timu hii kama wangepewa nafasi ya kuongea na Taifa Stars, tunahitaji kushinda ili tutimize malengo yetu. Adui anaweza kuwa na mbinu nyingi, lakini tunahitaji kushinda hizi mbinu zake tusonnge mbele.

Raisi pia hakusita kuonesha furaha yake na matamanio ya timu ya taifa kufanya vizuri.

“Nitafurahi sana tukifanikiwa kwenda Cameroon, na tukiingia kule turudi na kombe. Nitafurahi sana nyinyi vijana mkifanikiwa kuiwezesha nchi kushiriki kwenye mashindano ambayo hatujashiriki tangu mwaka 1980.” – Rais Magufuli

Raisi pia aliongelea kuhusu hali ya ufisadi ndani ya mpira wa miguu.

“Ufisadi wa viongozi wa michezo, umepelekea tumekosa fedha za FIFA za mwaka huu. Haya mambo yanakatisha tamaa wachezaji wetu.” – Rais Magufuli

Rais pia hakusita kuonesha kuumizwa kwake na hali ya timu kutofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

“Nilipoingia madarakani na kuona timu zote hazifanikiwi, nikawaza kuondoa timu zote niwaweke wanajeshi, na hiyo timu iwe pia timu ya taifa, wanajeshi hawa wasifanye kitu kingine zaidi ya Mpira tu.” – Rais Magufuli.

Hivo Rais akawaasa TFF wamtumie ipasavyo kocha Emmanuel Amunike katika maendeleo ya mpira wa miguu.

“Huu ni wakati wa mabadiliko, tayari tuna kocha mzuri Amunike. Nawaomba viongozi wa mpira msimuingilie kocha kwenye majukumu yake. Aachwe apange timu anayoona inafaa, “Nilipata matumaini wakati alipokuja Amunike, kuna hali ya kutaka kushinda unaiona, lakini mlipofungwa 3-0 nilikiwa discouraged sana, nilimwambia Waziri Mwakyembe.” – Rais Magufuli

Taifa Stars ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Cape Verde, na kufufua matumaini ya kwenda Cameroon mwakani katika michuano ya Mataifa ya Afrika. Timu yetu imebakiza michezo miwili, dhidi ya Lesotho ugenini na Uganda hapa Tanzania.

Hakika tiketi yetu ya kwenda Cameroon ipo Lesotho!

Sambaza....