Sambaza....

Dunia iko mbele sana, na imetuzidi hatua nyingi sana sisi WATANZANIA ambao tunaishi kwenye dunia yetu ya peke yetu inayoitwa TANZANIA. Hii ndiyo sayari yetu, sayari ambayo tumejitengenezea sisi tuishi maisha yetu ambayo tunayapenda na kuyafurahia sisi wenyewe.

Hii ndiyo sayari ambayo tumehararisha mambo ya HOVYO kuonekana na vipaumbele vikubwa. Tumewekeza kwenye vitu vya hovyo sana ambavyo havina tija kwenye safari yetu ya mafanikio. Hakuna ambaye anaumizwa na umasikini wetu!, hakuna ambaye anatamani kujifunza kwa wale ambao wametutangulia.

Tunaona kawaida tu, tena kawaida sana kwa sababu tumezoea kuishi kwenye ukawaida usio wa kawaida. Haya ndiyo maisha yetu , maisha yanayoshangaza sana!. Maisha ambayo ni rahisi kumuona mtu akimpima tembo kwenye mizani ya dukani!. Kwa sababu kwetu sisi ni kawaida kufanya vitu vya kawaida na tena visivyo na tija kabisa katika maisha yetu.

Ndiyo maana hata kwenye fainali ya kombe la klabu bingwa barani Afrika kati ya Esparance na Al Ahly hatukuona kitu cha kujifunza kwenye mechi ile. Uliiona jezi ya Esparance ? Ilikuwa imepambwa na matangazo mengi ya wadhamini mbalimbali wa klabu hiyo.

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji.

Wadhamini zaidi ya watano , tena hapo mbele ya jezi, bado nyuma ya jezi na kwenye bukta!. Hata kiatu chao pia kilikuwa na nembo ya mdhamini. Kwao wao wako radhi hata kwenye ngozi ya mwili wao waweke matangazo ya wadhamini mbalimbali ambao wamekuja kuwekeza ndani ya klabu hiyo.

Uwekezaji ni ushawishi!, kufikia mfanyabiashara mpaka kuja kuweka pesa yake sehemu inahitaji ushawishi wa hali ya juu. Ushawishi ambao utamuonesha ni namna gani atairudisha pesa yake na kupata faida. Namna gani ambayo ataweza kukuza masoko yake ndani ya nchi na nje ya nchi baada ya yeye kuingia mkataba wa kutangaziwa bidhaa yake na klabu husika.

Hili siyo jambo jepesi hata kidogo!, linahitaji kitu kinaitwa “KUMWAMINISHA” Umwaminishe mfanyabiashara kuwa akija kwako atapata faida kubwa baada ya kuweka pesa yake. Mazingira ya yeye kurudisha pesa yake yanatakiwa kuandaliwa na viongozi imara, hapo ndipo panapohitajika kitu kinachoitwa KLABU IMARA.

KLABU IMARA itavutia wawekezaji imara, wawekezaji ambao watakuja na pesa nyingi ambazo wataweka ndani ya klabu hiyo imara kwa imani kuwa watapata faida kubwa sana watakapoweka hiyo pesa. Hapa ndipo tunapokuwa tunapishana na kanuni ya mafanikio. Muda ambao tunatakiwa kujenga “TAASISI IMARA” tunapigania kujenga “MTU IMARA NDANI YA TAAASISI DHAIFU!”.

Mtu ambaye ataishi kwa muda mfupi kama kiongozi wa timu na baada ya muda wake kuisha ataondoka! Ataiacha timu kama ilivyo ikiwa dhaifu hata uwezo wa kulipa mishahara ya wachezaji haina kabisa!.

Hapa ndipo uajabu wetu unapoonekana. Hapa ndipo utofauti wetu na wao unapoanzia. UNAANZIA KWENYE KUFIKIRIA. Hatufikirii vyema ndiyo maana hakuna chema tunachokipata ndani ya vilabu vyetu.

Tupo kwenye sayari ya peke yetu tu kabisa na inawezekana TANZANIA ni sayari ya kumi baada ya zile sayari tisa zinazotambulika. Tuna tabia za kipekee sana, tena za kitofauti sana na watu wa sayari ya DUNIA ambayo tunasingiziwa kuwa tunaishi. Hatuishi kabisa kwenye sayari hii ya DUNIA. Tupo kwenye sayari yetu kabisa ya kwetu sisi.

Sayari ambayo mambo ya Hovyo yanapewa kipaumbele cha kwanza. Sayari ambayo tunapenda kumtukuza mtu badala ya kutengeneza taasisi ambayo inaweza kujiendesha kibiashara na tukawa tunaitukuza yenyewe!

Hapa ndipo hatua zetu za maendeleo zinapotofautiana na kina Esparance. Wakati wenyewe wanawaza kuongeza idadi kubwa zaidi ya wadhamini sisi tunafikiria kulilia Yusuph Manji arudi ili aendelee kutoa pesa zake mfukoni bila mkabata wowote wa kibiashara!.

Sambaza....