Sambaza....

ARSENAL vs LIVERPOOL.

Arsenal katika mechi hii walitumia mfumo wa 4-3-2-1 wakati Liverpool walianza na mfumo wa 4-3-3, ila walikuwa wanabadirika kulingana na wakati, kuna kipindi walicheza 4-3-2-1 na kuna wakati wakacheza 5-3-2.

Liverpool walianza vizuri katika kipindi cha kwanza kwa kumiliki mpira, na kukaba kwa nguvu hali ambayo iliwafanya Arsenal wafanye makosa binafsi ambayo yaliwafanya wasipate nafasi ya kushambulia kama Liverpool.

Wakati Liverpool walipokuwa wanacheza mfumo wa 4-3-3, Roberto Firmino alikuwa anashuka chini katikati.

Hali ambayo ilisababisha Nacho Monreal kushuka naye chini katikati, alikuwa anafanya man to man marking.

Nacho Monreal alipokuwa anashuka chini, nyuma alikuwa anaacha nafasi, nafasi ambazo zilikuwa zinawafanya kina Countinho, Mane na Salah kuzitumia, hata goli la kwanza lilitokana na Countinho kuwa peke yake akitumia nafasi iliyoachwa wazi na Nacho Monreal aliyekuwa ameshuka chini kumkaba Roberto Firmino.

Goli la pili lilitokana na Firmino pia kushuka chini katikati na mabeki wa Arsenal kumfuata na kuacha nafasi wazi ambayo ilitumiwa na Mohamed Salah kufunga goli.

Mabadiriko ya kutoka Hernderson na kuingia James Milner kulikuwa na faida kubwa kwa Liverpool kwenye suala la kujizuia na kushambulia.

Liverpool walijua beki wake wa kulia Hector Bellerin anapanda sana kushambulia , hivo James Milner alikuwa anakuja upande wa kushoto mwa Liverpool kumsaidia Robertson , hali ambayo ilipunguza nguvu kwa Hector Bellerin.

Liverpool mabeki wake hawakuwa na marking nzuri kwa sababu walikuwa wanawaacha peke yao washambuliaji wa Arsenal. Mfano goli la kwanza la Arsenal ambapo Sanchez alikuwa peke yake kabla na baada ya kupokea mpira.

Arsenal walifanikiwa kurudi kwenye mchezo na kufanikiwa kufunga goli tatu.

Liverpool walirudi katika mfumo wa 4-3-2-1 ambapo Firmino alibaki peke yake mbele na kunyimwa uhuru wa yeye kushuka chini katikati.

Baada ya kuona Arsenal anaongoza goli tatu , Klopp alibadirika haraka na kurudi katika mfumo wa 4-3-3 ambapo Firmino alirudi katika majukumu yake ya awali, na timu ikasawazisha. Baada ya kusawazisha Liverpool walibali mfumo na kwenda katika mfumo wa 5-3-2 ambapo waliongeza watu katika eneo la kujilinda na mbele wakabaki Salah na Firmino.

EVERTON vs CHELSEA.

Sam Allardyce amefikisha michezo 6 bila kufungwa na akiwa na clean sheets nne, huku akishinda michezo minne na kutoka sare michezo miwili

Phil Jagielka na Micheal Keane walifanikiwa kutengeneza ukuta imara wa ulinzi.

Pamoja na kwamba Phil Jagielka ilikuwa mechi yake ya kwanza hakuonesha kukosa sharp nzuri kwenye timu.

Antonio Conte aliamua kumtumia Hazard kama false 9, lakini akawa ameangushwa na kutokuwepo na kiungo ambaye anatengeneza nafasi nyingi za magoli.

Hivo hata wakati Hazard anashuka chini katikati, na kina Pedro na Willian wakitokea pembeni kuja eneo la box la Everton hawakuwa na nafasi ya kupata mipira mizuri kutoka katikati kwa viungo

Sam Allardayce alihakikisha timu yake iwe na ugumu katika ukabaji.

Alitumia mfumo wa 4-1-4-1 ambapi ulimfanya Dominic Calvert-Lewin kuwa mshambuliaji peke yake kule mbele, ambapo Rooney hakuwepo.

Sam Allardayce alifanya mabarikio ya kiufundi ambapo alimwingiza Williams kuchukua nafasi ya Tom Davies na kutengeneza idadi ya mabeki watatu nyuma, na Aaron Lenon nafasi yake kuchukulia na Sandro Ramirez

LEICESTER CITY vs MANCHESTER UNITED.

 

Timu zote katika makaratasi zilikuwa zimeingia na mfumo wa 4-5-1 , lakini hii ilikuwa tofauti kwa Manchester United walipokuwa wanashambulia ambapo walikuwa wanabadirika kwenda 4-3-3 .

Leicester City walitumia muda mwingi kukaa nyuma na kushambulia kwa kushtukiza.

Goli la kwanza la Leicester City , wachezaji wa Manchester United walikuwa mbele , upande wa kushoto Ashley Young alikuwa amepanda kusaidia mashambulizi.

Kitu ambacho kilimpa nafasi Mahrez kuwa peke yake na kuanzisha shambulizi ambalo lilizaa goli la kwanza.

Wachezaji wengi wa Manchester United walionekana kukosa umakini pale walipokuwa wanapata nafasi.

Lingard, Rashford na Martial walipata nafasi za wazi lakini wakashindwa kuzitumia ipasavyo.

Sambaza....