Mataifa Afrika U17

Uwanja wa Uhuru wakamilika 90%, tayari kwa michuano ya AFCON.

Sambaza....

Zikiwa zimesalia siku 12 kabla ya michuano ya Kandanda ya Afrika kwa vijana chini ya Umri wa miaka 17 haijaanza, inaelezwa kwamba zoezi la ukarabati wa uwanja wa Uhuru ikiwa ni pamoja na kubadilisha nyasi linaendelea vizuri.

Meneja wa uwanja huo Nsajigwa Godwin amesema tayari wameshafanya zoezi la kubadilisha nyasi kwa kutoa nyasi za awali na kutandaza nyasi mpya na zoezi la sasa ni zoezi la kuweka mistari kwenye uwanja huo.

Amesema wanajitahidi kukamilisha mapema zoezi la ukarabati wa uwanja huo kwani timu shiriki zitaanza kuwasili April 10 kwa ajili ya mashindano hayo ambayo yanatazamiwa kuanza April 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

“Tayari tumeshabadilisha nyasi, kwa maana tumetoa nyasi za awali na tumeweka nyasi mpya na sasa hivi tupo kwenye hatua za mwisho, tunaendelea kuweka mistari tukiwa tayari kwa ajili ya kuanza kuzipokea timu na kumbuka watakuwa wakiutumia uwanja huu kama uwanja wa mazoezi,” Nsajigwa amesema.

Tanzania watakuwa wenyeji wa mashindano hayo ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ambayo yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi April 14 mwaka huu.

Tanzania ambao ndio wenyeji wamepangwa kundi A pamoja na timu za vijana za Uganda, Angola na Nigeria huku wakitazamiwa kufungua dimba kwa kucheza na Nigeria siku ya ufunguzi kabla ya baadae April 17 kucheza na Uganda na watamaliza hatua ya makundi April 20 kwa kucheza na Angola.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.