Sambaza....

Nipo ndani ya uwanja mpya wa Taifa nikifatilia Mpambano wa Fainali wa mashindano yaliyopewa jina la URAFIKI CUP kati ya AZAM FC vs SIMBA SC jukwaa lile lile ambalo anapenda kukaa Pacha wangu wa Nje Bwana Frank Robert Rweyemamu mara inarushwa chupa ya maji kuelekea uwanjani aliposimama mshika kibendera kutoka jukwaa la juu yetu la rangi ya Bluu nageuka kumtazama mrushaji wa Chupa ile bila Mafanikio lakini simuoni wakati naendelea kutafuta mara nakutana na Bendera ya rangi Nyekundu ikiwa na Maneno haya “IKO SIKU KILA MTU ATAISHABIKIA SIMBA SPORTS CLUB” naachia tabasamu angavu kisha narudisha macho yangu uwanjani kuendelea kufuatilia yanayojiri mechi inaisha mikwaju ya penati inapigwa na Juma K. Juma kwa mara nyingine anaibuka shujaa kwa kudaka penati mbili za wachezaji wa Azam na Simba inakuwa Bingwa, siku inayofuata nayachukua yale maneno kama yalivyo nayatupia katika Wall yangu ya Facebook kisha naya-copy kwenye group mbili ya Kandanda na SportsXtra yanazua mjadala mkali huko mimi naendelea na shughuli zangu.

Baada ya takribani masaa 48 kupita timu yenye jina dogo ya Atletico Club kutoka Burundi inaiangushia dhahama Yanga SC kwa kuichapa mabao mawili kwa sifuri nakuipigia mpira mwingi sana wafatiliaji wa mambo ya Kandanda wananielewa navyosema hivi, nayakumbuka yale maneno ya ile bendera nakuyarudishia tena kwa wall yangu na katika zile group yanaleta taabu tena dah! Maisha yanaenda kasi sana siku hizi mara mchangiaji mmoja anaitwa Bwana Raymond Mlowe akijitambulisha kuwa yeye ni Shabiki wa Azam FC anaamua kutoa yake ya moyoni na hii ilikuwa sehemu ya majadiliano yetu;

Raymond Mlowe: Azam fc.. with time,will be Tanzania’s and Africa’s #1 choice …4get the twins…

Me: In your Dreams

Raymond Mlowe: Ha ha ha! Nilijua utacrush tu.. but ukweli ndo huo. Itafahamika tu

Me: Ray I was the first one before you taken by what I can say propaganda za hao watu wako but it took me only 4 months to realize kuwa jamaa ni magumashi tu, ukihitaji details i will write makala nikutumie!

Raymond Mlowe: Dizo naomba hiyo makala, haraka iwezekanavyo

Me: Just send me your email then will make sure unaipata as soon as possible! Written by me Ray!

Hivi ndivyo tulimaliza majibizano yetu, nikaingia mzigoni kutimiza AHADI yangu!


Azam Football Club ilianzishwa mwaka 2007 Pindi nipo mwaka wa pili naelekea wa tatu katika Chuo Cha Usimamizi wa Fedha na waliokuwa wafanyakazi wa SSB kwa nia ya kujifurahisha baada ya kazi ngumu za kila siku, kwa kuwa walikuwa wanajifurahisha likaja wazo la kujenga Timu ambayo itakuwa inashindana katika Ligi na Yusuph Bakhresa akaja na mpango mkakati wa kuijenga timu, na msimu wa 2008/2009 ikapanda hadi Ligi kuu ya Tanzania Bara, katika msimu wake wa Kwanza ikashika nafasi ya 8, na Msimu wake wa pili ikashika nafasi ya 3!

Source: www.azamfc.co.tz

Kufuatia mafanikio hayo ya muda mchache nikashawishika kutaka kujua nini hawa jamaa wa Azam FC wanafanya nikawa muhubiri wao na kuwatangaza japo nilikuwa silipwi hata senti, siku moja nilibishana sana na pacha wangu Rweyemamu mwisho wa siku tukakubaliana kutokukubaliana, miaka imeenda kasi sana Azam ikaingia kwenye maboresho ya timu yao kwa kuanza walianza na Academy walichukua wachezaji wote waliowaona wamefanya vizuri kwenye Copa Coca cola, akiwemo mchezaji bora na kipenzi changu Joseph Mahundi kutoka ile timu Bingwa ya mashindano ya mara ya kwanza kabisa kufanyika ya mkoa wa Ruvuma, wakatengeneza timu kali ya vijana nakumbuka Azam wakati wanafanya hivi Simba na Yanga zilikuwa zimelala usingizi mzito hata yalipokuja mashindano ya Uhai Cup walijaza vijeba kwenye timu zao na mwisho wa Siku hawakuleta tija, Azam ikatamba katika fainali mbili za mashindano yale kipindi ipo na aliyekuwa Kocha wa viungo na Stars ya Marcio Maximo, Itamar Amorin, timu ilionekana ipo vizuri kifiziki na kiufundi nikasema Muokozi wa soka letu amepatikana kumbe nilikuwa najidanganya maruwe ruwe yakaanza

Makocha walioipandisha timu hadi Ligi kuu Kocha King, aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo wakaonekana hawawezi kazi yao hivyo anatakiwa Kocha wa hadhi ya Ligi kuu baada ya timu kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kusua sua viongozi wa Azam bila kupiga mahesabu yoyote wakafunga safari hadi kwa aliyekuwa kocha wa Simba Mbrazil Neider dos Santos wakampa mkataba wa miaka kadhaa akisaidiwa na Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa makipa akaja na mahitaji yake la kwanza ikiwa ni kuifumua timu ufanyike Usajili wa wachezaji kumi na kuwatoa wengine kumi kwa mkopo ili wasivunje taratibu na kanuni za ligi, hili lilifanyika katika mapumziko ya ligi walisajiliwa wachezaji wa ndani na nje ya nchi hapa palinistua kidogo na kuwaza lini hawa wachezaji watakuja kuzoeana na kutengeneza Bond?? Sababu aliyoitoa kocha huyu kuwa ligi kuu inahitaji watu waliowahi kucheza na wenye kuijua Vipi Swansea ilisajili hivi mbona bado imezitesa vigogo kama Arsenal, Liverpool na hata Mabingwa Man City walifungwa walipoenda Liberty Stadium kule Wales

Wachezaji hawa walikuwa na timu mzunguko wa kwanza wa Ligi kuu kipindi hicho kabla hakijapanguliwa Kassim Kilungo, Saidi Bakar Nachikongo, Abdul Aziz Hamza, Shaaban Abdallah Kisiga ‘Malone’, Ally Suleiman Alawy, John Raphael Bocco ‘Adebayor’, Salum Machaku, Shekhan Rashid Abdallah, Jamal Simba Mnyate, Yussuf Juma Gogo, Zuberi Ubwa, Yahaya Saidi Tumbo, Saidi Khamis Sued, Salum Abubakar Salum, Luckson Jonathan Kakolaki, Adam Shomari Ngido, Abdulhalim Chilumbe, Ngoy-Pichou Botwetwe, Mussa Khalid Kipao, Iddi Abubakar Mwinchumu, John Faustine Mabula, James Adriano Kilongola, Malika Philipo Ndeule, Paulo John Nyangwe, Abubakar Pawasa na Vladimir Niyonkuru.

Timu ikapanguliwa na kuingizwa wachezaji hawa wafuatao Danny Wagaruka, Ibrahim Shikanda, Ben Kalama, Crispin Odula, Philip Alando, Seleman Kasim, Aggrey Morris, Ibrahim Mwaipopo, Salvatory Ntebe, Erasto Nyoni utashangaa mbona majina ya wachezaji wa kigeni yapo mengi kipindi hiki timu zilikuwa zinaruhusiwa kuwa na wachezaji wa kigeni 10! Na shirikisho la soka TFF

Ikapigana vya kutosha na kufaulu kubaki katika ligi kuu ikishika nafasi ya 8, Benchi la Ufundi likiongozwa na Neider dos Santos likaingia kwenye usajili tena safari hii likiwaacha wachezaji wengine kumi wengi wao waliowatoa kwa mkopo kipindi cha dirisha dogo na baadhi ya walioongezwa wakiwamo Chrispin Odula, Habib Mhina, Maridad Haule, Nsa Job, Said Swed, Salum Machaku, Yahya Tumbo, Ben Kalama, Shaaban Kisiga na Dan Wagaluka

Hii iliifanya Azam FC ibaki na wachezaji 14 ndipo walipofanya usajili wa wachezaji hawa Mohamed Binslum (Huru) Jackson Chove(JKT Ruvu), Jabir Aziz na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ (Simba), Mrisho Ngassa (Yanga), Kalimangonga Sam Daniel Ongala Rampling ‘Kali Ongala’ (GIF-Sweeden), Patrick Mutesa Mafisango (APR- Rwanda) na Peter Senyonjo (Polisi-Uganda.)

Waliopandishwa toka Azam Academy wachezaji sita ambao ni Sino Augustino, Himid Mao, Mau Ali, Tumba Swed, Ali Mkuba na Samih Nuhu katika listi ya wachezaji waliosajiliwa hapo juu kuna mmoja sijawahi kupata taarifa zake kama yupo hadi sasa akicheza mpira na wala sikusikia siku alipoachwa.

Ambao walijiunga na waliobaki kwenye timu John Bocco, Erasto Nyoni, Jamal Mnyate, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Vladmir Niyonkuru, Philip Alando, Luckson Kakolaki, Malika Ndeule, Aggrey Morice, Salum Swed, Ibrahim Shikanda, Ally Manzi, Seleman Kasim ‘Selembe’ na Ibrahim Mwaipopo.

Hii itakuonyesha ni jinsi gani timu ilivyokuwa inaendeshwa kiholela holela ndani ya kipindi cha dirisha dogo na usajili mkubwa walisajiliwa wachezaji zaidi ya 26 na kuachwa wachezaji 20 hapa vipi unaweza kusema hawa jamaa wapo kwenye mipango yakinifu ya kuendeleza soka kweli?? Jibu hapana!

Tukaingia kwenye Ligi walikosa nini Azam sijui???, Bus zuri la kusafiria, kambi nzuri, chakula kizuri posho kwa wachezaji, vifaa bora na vya kisasa, lakini kwa maajabu ya wengi timu hii ilikuwa inaelekea kushuka Daraja ndipo Uamuzi wa kumfukuza kazi Neider dos Santos ulipochukuliwa ili kuinusuru timu! Nilitangulia kusema hapo juu hawakufanya hesabu yoyote juu ya aina ya Kocha wanaemuhitaji wenyewe walifata porojo tu kuwa Santos aligombana na Viongozi wa Simba hivyo Viongozi walikuwa wamekosea.

Itamar Amorin (Kushoto)

Katika harakati za kujinasua kutoshuka daraja wakampa timu aliyekuwa Kocha wa timu yao ya vijana na mtaalamu wa fiziki Bwana Itamar Amorin uamuzi huu nauchukulia kama kujipiga mkuki kwenye Moyo, Azam wakaua soka lao la vijana bila wenyewe kujua Itamar akaichukua timu katika nusu ya pili ya Ligi na kufanikiwa kuipeleka hadi nafasi ya 3 kwenye msimamo Ligi ilipoisha, Vipi kwenye soka la Vijana wakapoteza ubingwa wao wa Uhai kwa Simba na msimu uliofuata JKT Ruvu wakaibuka mabingwa wakiwafunga ndugu zao wa Ruvu Shooting walipozaliwa kina Frank Domayo hapa! Azam timu yao ya Vijana ikakosa uelekeo haikufika hata Fainali, mwaka uliofuata wakajitutumua wakafika fainali safari hii wakifungwa na Simba tena hivyo ubingwa kwenda Simba, Tuachane na katimu haka ka vijana kalikokosa muendelezo

Baada ya kumaliza ligi vizuri Azam Fc ikajipanga kwa Msimu mpya ambapo kwa kuanza ikamleta Kocha wa vijana ambae pia ni msaadizi wa kikosi cha kwanza kutoka India aliyejulikana kwa jina la Vivek Nagul kuja kuchukua mahala pa Herry Mzozo katika hili sikuona mafanikio yoyote maana timu badala ya kusonga mbele imerudi nyuma ikakutana tena na Simba SC kwenye fainali ya Uhai wakafungwa kwa matuta safari hii sijamsikia tena yule Kocha Vivek Nagul aliyekuja na mipango mingi na CV kubwa ya kutisha.

Itamar akaanza ligi akiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kufuatia mafanikio aliyoyapata katika muda mfupi tangu aichukue timu mambo hayakwenda vile alivyofikiria utovu mkubwa wa nidhamu wa wachezaji ukaibuka na kuzua tatizo kubwa, ilipata kuripotiwa wakati timu imetoka kucheza na Polisi Dodoma mjini Dodoma wachezaji wawili wa timu hiyo walikiuka maadili ya kambi na hivyo kusababisha baadhi ya wachezaji kuchukia na kocha Itamar alipotaka kuchukua hatua alionekana kama Kiranja wa zamu ambae hakuwa na uwezo wa kuamua lolote mbele ya nyota hao ambao mmoja aliachwa Hoteli waliyofikia siku wanarudi Dar es Salaam kujipanga na mechi inayofuatia na ilipogundurika hivyo mwenzie ambae alikuwa hajiwezi kwa pombe akashinikiza gari lirudi hadi Hotelini au wamshushe arudi amfuate swahiba wake huyo, Amri ambayo Itamar aliipinga lakini kwa nguvu ya mchezaji huyo ilibidi Bus lirudi si chini ya kilometa 10 hii ilitokea kwasababu tu wachezaji wale walikuwa na nguvu kuliko Mwalimu wao pamoja na Viongozi walioambatana na Timu kwa safari ile, Wachezaji wale hawakuwa na cha kuhofia kwasababu walikuwa wanajua hakuna hatua yoyote ya kinidhamu ingechukuliwa dhidi yao!

Hatimae Timu ikamshinda Itamar ikapoteza mechi mfululizo akashindwa kudhibiti nidhamu ya wachezaji akaamua kukaa na Viongozi wa Azam na kuvunja Mkataba kwa Faida ya Timu, Yeye mwenyewe na Wachezaji! Stori ya Mbrazil huyu aliyeijenga timu ya vijana ya Azam ikaishia hapo ilikuwa Oktoba 31 2010 ndipo katibu Mkuu Nassor Iddrisa alipotangaza hilo!

Azam Fc wakaingia kwenye mchakato wa kutafuta Kocha mpya katika kipindi kama kile yaani kati kati ya Ligi walichovunja mkataba na Neider dos Santos hivyo timu akakabidhiwa Habib Kondo kama interim coach kwa mechi mbili za mwisho za mzunguko wa kwanza, yakasemwa mengi kuwa aliyekuwa Kocha wa Simba SC wakati huo Patrick Phiri ndio alikuwa awe mrithi wa Itamar baadae yakaja majina ya makocha wengine wengi kutoka pembe zote za Dunia lakini haikuwa hivyo aliyekuwa Kocha wa timu ya Taifa ya Zanzibar ambae pia alipata kuomba kuinoa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars Stewart John Hall akatuma maombi ya kazi iliyokuwa wazi katika taarifa yake iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Azam FC Ndugu Nassor Idrissa ilisema “Azam FC imemchukua kochaStewart John Hall baada ya kuridhishwa na CV yake, rekodi yake kama kocha na pia utendaji kazi aliouonesha kwa kipindi kifupi alichoanza kuifundisha timu hiyo ya taifa ya Zanzibar.”

Katibu Mkuu wa klabu hiyo Nassor Idrissa akaendelea kusema wameangalia vyeti vyake na ujuzi alionao hivyo wakaamua kumpa nafasi hiyo.

Lakini katibu mkuu Nassor Idrissa alisisitiza kuwa Stewart hakuwa mmoja kati ya makocha waliokuwa wakiwahitaji lakini jina lake lilikuja ghafla wakati mashindano ya CECAFA yakiendelea baada ya kocha huyo mwenyewe kuwasilisha CV yake na kuuambia uongozi wa Azam FC kuwa baada ya CECAFA atakuwa kama hana kazi kutokana na Zanzibar kutoshiriki mashindano yoyote hivyo kupoteza fedha za wafadhili wake.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyowekwa kati ya Azam FC na kocha Stewart, Stewart ataendelea kuwa Mshauri wa ufundi wa ZFA bure na ataendelea kuisaidia Zanzibar kama sehemu ya benchi la ufundi hadi pale Zanzibar itakapopata kocha mwingine kuchukua nafasi yake.

Swala la msingi la kujiuliza Inakuwaje timu ya khariba ya Azam ikamchukue kocha ambae hakuwa kwenye mipango yao?? Ati kisa katuma CV tu basi inatosha kumpa timu inamaana hawakuwahi hata kuweka mchakato wa kutangaza nafasi hiyo ili Makocha tofauti wenye uwezo waombe Kazi hiyo kuchuana na Stewart weredi uko wapi hapo?? Anyway tuachane na hayo na yeye kama walivyopita watangulizi wake akaingia kwenye usajili hapa unaona madhara ya kubadili kocha katika kipindi cha muda mfupi kila kocha anakuja na mahitaji yake, kwa maana hii timu ilikuwa ikibomolewa kwa mara ya Tatu katika kipindi cha miaka miwili tu! Swali tunajenga tunabomoa??

Safari hii ilikuwa kivingine sana baada ya Ligi kwisha tukiambiwa na Mtu wa karibu wa timu hiyo alijinasibu kuwa watafanya usajili wenye akili sana na ambao haujawahi kufanyika hapa nchini kwasababu wamefuata ushauri wa mwalimu wao hivyo basi wameenda Ghana na kurudi na Beki mahiri wa Kati na Mshambuliaji hatari ambae aliibuka Mfungaji bora kwenye Ligi ya Ghana, Awudu Nafiu aliyekuwa beki toka timu ya King Faisal na Mshambuliaji Wahab Yahaya wa Liberty wakajiunga na Kipre Tchetche kutoka Ivory Coast ambae alionyesha kiwango bora kwenye Challenge, Obren Cuckovic kutoka Serbia na Abdulhalim Humud toka Simba ambae walibadilishana na Kiungo Marehemu Patrick Mutesa Mafisango, katika nilichokiona ni kulipa fadhila kwa Zanzibar kumruhusu kufundisha Azam Kocha Stewart John Hall akawabeba wachezaji wasiopungua saba toka timu ya Taifa ya Zanzibar wakiwamo golikipa Mwadini Ally, Beki wa kushoto Wazir Salum, viungo Abdulghan Gulam, Abduhalim Humud na Khamis Mcha kupelekea timu hii kupewa jina la utani la Wazanzibari wa Chamazi

Katika usajili huu kwa ujumla wake ulifanya Azam isajili wachezaji wasiopungua kumi kama kawaida yao hivyo kupoteza nafasi ya wale wachezaji waliopandishwa toka Azam B na kupelekea wote kupelekwa kwa mkopo katika timu ambazo hazina vifaa wala khariba kama Azam eti wakanyanyue viwango vyao ili kwasababu wakibaki Azam watakosa nafasi ya Kucheza je hili ni kuwaendeleza ama kuwaua kisoka wachezaji hawa?? Ambao mtangulizi wa Stewart John Hall Bwana Itamar Amorin alishaanza kuwapa nafasi ya kucheza kila wiki katika kikosi chake hivyo kwenda kinyume na maneno aliyoyasema wakati anaichukua timu Stewart Hall aliahidi kupigania soka la vijana na atawapa nafasi na kipaumbele kikubwa lakini katika hali ya kushangaza kilipofika kipindi cha dirisha dogo alivunja mikataba ya Waghana wawili ambao walikuwa wamesaini mikataba ya miaka miwili kila mmoja kwa mbwembwe za yule jamaa yetu na kuwalipa gharama za kuvunja mikataba yao kisha akaingia sokoni kuwanunua wachezaji watatu Kipre Bolou toka Ivory coast, Abdi Kassim “Babi” aliyekuwa ameachwa na klabu yake ya nchini Vietnam na Gaudence Mwaikimba toka Moro United usajili unaosadikiwa kutumia zaidi ya Milioni 90!! Kwa wachezaji ambao siku zao za kucheza mpira zinahesabika kutokana na umri kuwatupa mkono Babi alikuwa ameachwa Vietnam, Mwaikimba alikuwa anafanya vizuri Moro Utd lakini kwenye timu tayari una John Bocco, Kipre Tchetche, Abdulghan Gulam na Khamis Mcha, Mrisho Ngassa ambao wanaweza kucheza namba yoyote ya ushambuliaji Mwaikimba alikuwa anasajiliwa ili aje kufanya nini? Inasadikika Usajili wa Kipre Balou pia lilikuwa ni shinikizo la pacha wake Kipre Tchetche baada ya kuwa mpweke hivyo alitaka asajiliwe ndugu yake yakapita kimya kimya hakuna mtu aliyeuliza na wachezaji hao wote walitumia muda mwingi wa kumalizia ligi kwenye benchi Vipi kama pesa za usajili huu zingewekezwa katika mahitaji mengine ya timu?? kufuatia usajili huo usiokuwa na tija vijana wote waliopandishwa toka timu B na Bwana Itamar Amorin ambayo wenyewe wanaiita Academy walitoswa!

Kichekesho eti unajua sababu ya wale Waghana kuachwa ilikuwa Viwango vibovu kuliko wazawa hii ilipelekea kocha Stewart ashindwe hata kuwapanga kwenye Mazoezi mechi ya timu hii ilinifanya niamini kuwa Azam hawana tofauti na Simba na Yanga kwenye siasa za usajili nikimaanisha Kocha anaambiwa tulia sema unataka mchezaji wa kucheza nafasi ipi tutamsajili tutakuletea hivyo kwasababu hakuwahi kuwaona hapo kabla ilikuwa rahisi kuwatema tu, lakini wenyewe walipita wakilalamika kuwa wanarogwa na wazawa mimi nikaishia kucheka sana na kuendelea na mipango yangu ya kila siku ya maisha

Hadi wanatangaza wachezaji wao watakao kuwa nao kwenye msimu ujao wa 2012/2013 ni majina mawili tu ya wachezaji waliopandishwa toka timu B yamesalia nao ni Himid Mao na Samih Nuhu, swali la msingi wako wapi kina Sino Agustino, Mau Ali, Tumba Swed, Ali Mkuba waliopandishwa toka timu B na kocha Itamar Amorin? Yuko wapi Joseph Mahundi mchezaji Bora wa Copa Cocacola ya kwanza?? Yuko wapi Jamal Mnyate mchezaji aliyetajwa kuwa na uwezo mkubwa sana wa kumfikia na pengine kumpita Mrisho Ngassa? Unamtoa Jamal Mnyate, Salum Machaku unawaleta Zahor Pazi, Mrisho Ngassa hapa napo nina lawama walimsajili Zahor Pazi wakati akiwa kwenye fomu ya juu sana wakati akiwa Mtibwa Sukari na baadae African Lyon leo hata ile timu ya Julio ya vijana alikuwa anakaa Benchi na wakati mwingine tulikuwa nae majukwaani nilipomuuliza yule Jamaa dah akanipa jibu eti hata yeye anashangaa kiwango cha Pazi kimeenda wapi? Mchezaji ambae Marcio Maximo alimpa jezi namba 9 kwenye timu yake akiongoza mashambulizi kwenye Taifa Stars yetu!!

Kuna kitu kinaitwa SABAMETRIC hizi ni hesabu za kitakwimu za mchezaji zitumiwazo na timu kubwa nyingi sana Duniani kabla hawajaamua kumsajili mchezaji hasa za America ya Kusini, hesabu hizi zinahusu Mechi alizocheza mchezaji husika na kiwango chake kama mshambuliaji kafunga goli ngapi vipi afya yake na nidhamu yake kwa ujumla Simba na Yanga hawafuati hili ndio maana Simba iliwahi kumsajili mchezaji kwa dakika 25 tu alizoingia uwanjani katika mechi ya kirafiki mchezaji ambae hadi leo wanahangaika kumpeleka kwa mkopo timu ndogo lakini unajua walitoboka shilingi ngapi?? Siri yao!! Azam nao wanapita humu humu kila kukicha japo watu wao wanapinga vikali kuhusu hili.

Ngassa

Vipi kuhusu ule Usajili wa milioni 58 wa Mrisho Ngassa kuilipa YANGA je umelipa?? Ngassa mwenyewe akilamba kiasi kinachodhaniwa kufikia milioni 50 hivyo kufanya usajili wake uwe ghali zaidi na kikubwa ukizihusisha timu za ndani milioni 108!! Alisajiliwa ili iwe nini?? Au mtasema mlikuwa mnajenga timu? Mtasemaje mnajenga timu ikiwa kila baada ya msimu mnaacha wachezaji 15 mnasajili 16? Hakuna timu inajengwa hivi jamani! Mwisho wa siku mmempeleka kwa lazima Simba ili mumkomoe?? Hapa mnaendeleza au mna ua?

Ikiwa usajili wa dirisha dogo wa wachezaji wa tatu ambao haukuwa na tija yoyote uliigharimu timu zaidi ya Milioni 90 hili lilitokea miezi michache kabla makala hii kuandikwa vipi usajili wa wachezaji kumi unaigharimu timu mamilioni mangapi?? Kama kuna siku Bakhresa ataamua kupiga hesabu ya pesa anazopoteza kwenye kujenga timu shindani basi ataachana na mpira wenyewe maana nachokiamini haujawahi kumuingizia faida kama biashara zake nyingine!

Pata kisa hiki cha mchezaji huyu anayeitwa George ‘Blackberry’ Odhiambo pasipoti yake inasema kazaliwa 1992 miaka 3 iliyopita alikuwa mchezaji Bora wa ligi kuu Kenya ina maanisha alikuwa na miaka kumi na saba tu! Akapata Deal katika klabu ya Randers FC ya Denmark timu inayoshiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya haijalishi inatolewa katika raundi ya ngapi leo hii eti Azam wana Ubavu wakumrudisha Tanzania acheze ligi kuu kwasababu ya kutafuta changamoto mpya jamani tuamke jamani eeh tuwe wakweli na tukubali ukweli jamaa kashindwa kucheza Randers FC hivyo karudi kuanza upya! Kabla hata ligi yenyewe haijaanza Blackberry kakutwa na kesi ya utovu wa nidhamu mkubwa na kumfanya atupiwe Virago unajua pesa ngapi ilitumika kumsajili mchezaji huyu?? Watu wa Azam wanajua hili, vipi pesa ya kuvunja mkataba nayo??! Usajili wa Deogratius Munishi umekuja kumfunika Bwana Mwadini Ally anyway ni changamoto kwa Mwadini Ally na Deo Munishi mwenyewe mimi najua Azam wametoboka si chini ya milioni 30 kuilipa Mtibwa Sukari Juu ya usajili huu vipi kuhusu pesa alizopewa mchezaji ni kiasi gani?? Mtibwa mafundi sana mwaka jana waliwapiga Yanga kwa Shaaban Kado mwaka huu Munishi kwa Azam yuko wapi Daudi Mwasonge yule kipa chipukizi aliyekuwa backup ya Mwadini Ally pale Azam FC na aliyetajwa kuwa mrithi halali wa Juma Kaseja Stars!???

Azam niliwapenda pindi mlipokuja mkiwa na Mission na Vision za kuendeleza mpira na wachezaji vijana kwa ujumla wake lakini kadri siku zinavyokwenda mnazidi kuwameza Simba na Yanga kitabia kinachoficha madhambi yenu ni kale ka uwanja kenu na hostel basi vinginevyo nanyi hamna jipya kama hivi vilabu vikongwe nchini!

Leo hii Simba imeweza kuingiza zaidi ya wachezaji Saba kwenye timu yao ya wakubwa toka timu B haijalishi wanacheza mechi gani lakini wapo na kwenye usajili wao unawaona na hili ndio maana hata Yoso wenu mwenye Uwezo mkubwa kisoka Ibrahim Jeba aliwakimbia na kwenda kuingia katika kikosi cha kwanza cha Simba, kama si kutofuatwa kwa taratibu huenda angekuwa mchezaji halali wa Simba SC, kitu kibaya toka arudi Azam FC sijamuona kwenye timu yenu B wala kikosi cha kwanza sasa sijui ndio mmepa Adhabu ya kumkomoa kimya kimya! Mimi sijui bwana.

Nilitegemea kwa uwekezaji huu wa pesa timu yenu iwe imechukua ubingwa wa ligi kuu hata mara mbili kwasababu ni kama mlijiwekea malengo ya muda mfupi kutwaa ubingwa wa ligi kuu bara, lakini ubingwa mnaojivunia eti wa Kombe la Mapinduzi kwa pesa zenu zote mlizowekeza na zinazoendelea kupotea kila kukicha mnatamba kwa ka-kombe ka milioni 5 shame on you eti Mapinduzi cup vipi kale ka-timu ka Simba B ambako hakana matunzo yoyote mbona kalitwaa kombe la BancABC la milioni 40 ambazo wale watoto waliahidiwa watapewa lakini hadi leo kalenda wasemaje??, kiukweli Azam Mnanisina sana tena sana, natamani hizo pesa mngeziwekeza katika kuendeleza timu zenu za vijana na watoto mngeisaidia sana nchi hii lakini zinaliwa na watu wachache wanaojifanya wajanja na watoto wa mjini, nafikiri kuna tatizo katika Uongozi!

Vipi kuhusu ile kesi ya Ramadhan Chombo mkatangaza mmemfukuza sababu ya tabia zake mbaya na utovu wa nidhamu uliokithiri na Kocha wenu kusema zilipigwa kura na wachezaji wenzie aondolewe mliposikia kapata timu Msumbiji mkagoma kumruhusu leo mmemrudisha kundini nini atajifunza Himid Mao?? Kuwa ukishakuwa na Jina tu basi hakuna atakae kusumbua atahangaikia jina baada ya hapo ni dharau na kiburi kitafuata dhidi yenu

Kuna siku nilikutana na huyu jamaa anaejiita PK yeye hanikumbuki ila mara ya kwanza namuona ilikuwa Kagame ya 2008 Uwanja wa Taifa mpya Simba wakicheza dhidi ya Vita’lo ya Burundi aliniuzia Jarida la Number Ten wakati huo tukapiga stori nyingi sana kuhusu Simba SC na yeye kujinadi ni Mnazi mkubwa wa Mnyama, Nilipomuona Azam nilishtuka nikakutana nae tena safari hii akiwa Azam FC akanipa mipango endelevu mingi sana lakini nilipokutana nae baada ya ule Usajili wenu wa wachezaji 13 kwenye dirisha dogo sikumuelewa alichokuwa anajaribu kunielezea hadi leo simuelewi kabisa, yupo bize akituma habari za Azam kuwa timu bora, ina timu ya vijana bora, inapigwa vita na Simba na Yanga kwa sababu wanajua mapinduzi ya kweli katika Soka yamekuja, kwangu mimi ubora wa timu ndani ya uwanja unapimwa kwa vikombe inavyochukua na sio kuwa na Bus zuri, uwanja mzuri wa mazoezi, Kambi nzuri na kutangazwa sana kama ndugu zetu wale wa Kijani wamenunua Media zote sijui wanazilipa shilingi ngapi???!!!!

Umeshawahi kujiuliza kwanini Simba na Yanga zinashindwa kupiga Hatua?? Unafikiri hawana viongozi wa kufanikisha malengo wanayojiwekea kila wanapoingia kwenye kipindi cha kampeni za chaguzi zao?? Jiulize maswali haya ukipata majibu jipe majibu mwenyewe baki nayo nafikiri Azam FC wanatakiwa kuajiri watu ambao watakuwa responsible kila hatua hivyo wakikwama wanawajibishwa na sio haka katabia kakufukuza makocha kila leo na kutuhumu HUJUMA kwa wachezaji kama hizi timu zetu za kariakoo tu, tumekuajiri uperform hivyo kila mtu atimize wajibu wake Maisha yanaendelea kwanini iwe kila Msimu usajili wa zaidi ya milioni mia mbili huku tukitumia zaidi ya milioni mia tano kwa mwaka kulea watoto ambao hatuwatumii mwisho wa siku timu kama Simba zinatumia madhaifu yetu kutupora bila ridhaa yetu wenyewe, najiuliza kwanini mchezaji kijana atoke Azam yenye kila kitu aende Simba?? Kuna tatizo hapo

Sikiliza kisa hiki cha Mrisho Ngassa baada ya mechi dhidi ya VITA SC ya Congo nusu fainali ya Kombe la Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame na yeye kuwa miongoni mwa wafungaji wa magoli mawili ya Azam FC ambayo yaliwafanya wacheze Fainali dhidi ya Yanga SC, na baada ya mechi ile akaonekana akiibusu beji ya jezi ya Yanga kwenye jukwaa la washabiki wa Yanga, viongozi wa Azam waliichukulia ile kama ni ishara ya tusi kubwa kwao, na kumuamuru Kocha wao Stewart Hall asimtumie kwenye mechi ya Fainali! Hapa nina lawama kwa Mchezaji mwenyewe Ngassa kwa kukosa Weredi na pia Kwa Uongozi Mzima wa Azam FC, kwanini wasingemwita Mchezaji kwa mahojiano na kuwaeleza sababu za kufanya “dhihaka” ile aliyoifanya?? Pasi kukurupuka na kutoa amri kwa kocha kumtumia mchezaji husika??

Mechi ya Fainali ikafika Magoli mawili ya Hamisi Kiiza na Saidi Bahanuzi yakahitimisha ndoto za Azam FC kucheza fainali katika mashindano yao ya kwanza ya Kagame na kutwaa Kombe, seke seke likamrudia Kocha Stewart Hall kwanini alimchezesha Ngassa mchezaji ambae aliitusi timu kwa kubusu jezi ya wapinzani?? Pamoja na utetezi wake wooote alioutoa Stewart Hall kuhusu kikosi chake na umuhimu wa Mrisho Ngassa akatupiwa virago na miongoni mwa sababu walizoitoa hawa watu wa Azam FC ni kuwa Stewart Hall alikuwa amepamisi kwao na familia yake kwa ujumla hivyo basi asingeweza kuendelea kubaki nchini ikapelekea mkataba kuvunjwa kwa Faida ya pande zote mbili, ulipita mwezi mmoja tu Stewart Hall akaibukia SOFAPAKA FC ya Kenya, hapa utajiuliza juu ya hizo sababu hapo juu ina maana kwa mtu aliyechoka kuishi Afrika tena Mashariki akae siku zisizozidi 25 tu arudi tena mbona Watanzania tunadanganywa kirahisi rahisi hivi??

Baada ya filamu Stewart Hall kwisha ikaja tena ya Ngassa hapa ndipo nilipochoka na hawa jamaa wa Azam FC, kwa mapenzi yake yote Ngassa alionyesha nia ya kwenda kuchezea timu yake ya zamani ya Yanga na Yanga walishakubali kumnunua Mrisho Ngassa lakini walitaka kumkomoa mchezaji husika wakampeleka Simba SC kwa madai eti Yanga walishindwa kufikia Offa ambayo Azam FC na Simba SC walifikia hili lilitokea bila Mchezaji husika kujulishwa, akawa anasikia kwenye Vijiwe vyetu vya Kahawa kabla habari haijawa Rasmi, Mchezaji mwenye Wakala ambae ameshaenda kufanya Majaribio Westham United na Seattle Sounders Marekani dah, kwa hili nilisikitika vipi hawa jamaa wapo kwenye kuinua Soka au Kuua Soka? Kuendeleza wachezaji au kudidimiza wachezaji? Ushajiuliza kuhusu wachezaji waliobaki kwenye kambi ya Azam wanalichukuliaje hili suala? Haliwezi kuwatokea mmoja wapo huko mbeleni??

Suala la kufungwa kwenye mechi na kushutumu wachezaji wameuza mechi ni suala zoelefu kwa vilabu vyetu vikongwe vya Simba na Yanga sasa vipi liingie kwa Timu yetu hii ya Mfano?? nilishangaa kuona hili suala hawa jamaa wamekopi na kupesti kwao! Baada ya mechi ya Fainali ya Kombe la Kagame kuna wachezaji nyota sita walishutumiwa kuuza Mechi, hivi hapa tunajifunza nini? Uongozi ni Mbovu na ndio sababu kama hizi zinatokea! Baada ya kukosa kujitetea uongozi wowote usio makini hukimbilia kutoa shutuma bila kufikiria repercussion ya hizo SHUTUMA katika siku za usoni na maisha ya wachezaji klabuni! Katika timu yangu ninayoiongoza na kuiandaa kisaikolojia siwezi kufanya kitu kama hiki

Boris Bunjak wakati anakuja toka Serbia Kocha huyu aliyekuja kurithi mahala pa Stewart John Hall tuliambiwa ana uwezo mkubwa saaana kuliko mtangulizi wake, tukaonyeshwa CV yake Nzito hawa watu ni HODARI sana kwa PROPAGANDA, wakasema walifanya upembuzi yakinifu kumpata Kocha huyu, na kwa sababu Stewart uwezo wake ulifikia ukomo wakataka kocha mwenye khariba ya Jose Mourinho au Alex Ferguson na wakasema wamempata Boris Bunjak lakini baada ya Mechi 8 akishinda 5, akitoa sare 2 na kufungwa 1 ameonekana hafai ndani ya miezi mitatu tu, wanasema timu inacheza Soka Bovu, haina muunganiko bora, hivyo ni bora wachukue maamuzi magumu kabla ya mambo hayajakuwa mabaya mbeleni huko. Vipi huyu Kocha akijitetea kuwa wachezaji aliowakuta hawana kiwango mtasemaje? Mwisho wa siku Boris ameondoka na Kutoa Kauli moja nzito kuwa “Anajutia uamuzi wake wa kuja kufundisha Azam timu ndogo, isiyo na Uongozi yakinifu wala Vision na Mission wamemchafulia CV yake ila atafanyaje ameamua kuondoka”

Azam FC Tv Show nini hasa Malengo ya kuanzisha kipindi hiki?? Mimi hadi sasa sijaona tija badala yake ni kupoteza pesa ya kulipia matangazo tu basi! Nilifikiria labda hii ingekuwa fursa ya wao kujitangaza mbali zaidi hata watoto wa kizazi hiki waipende na kujenga mashabiki wao wenyewe wamekileta hiki kipindi kama fimbo kwa marefa wetu, utasikia wakijitangaza usikose kuangalia Azam FC Tv show uangalie uozo wa marefa wetu ulivyoinyima pointi tatu muhimu Azam FC! Huwa nashangaa siku zote, nilifikiria kipindi hiki kingekuwa cha kuwatambulisha wachezaji wao wachanga na wa kikosi cha kwanza “Player Profiles”, kuonyesha highlights za mechi zao na mambo mengine muhimu badala yake wao wanatumia kama sehemu yao ya kujilinda juu ya utendaji wao mbovu, na Ukiwaambia wabishi hao hadi mapovu ya mdomoni yanawatoka!

Team Manager nilipata kuomba kupewa HADIDU ZA REJEA juu ya majukumu ya huyu mtu, Maana huyu Timu Meneja wa Azam FC nafikiria hajui majukumu yake ama kama anayajua basi anafanya makusudi mazima kuto yatekeleza, kuna muda anafanya kazi za Afisa Habari na hata ya Kocha kabisa, kama wiki imepita tangu watangaze kumrudisha Kocha wao Stewart John Hall kupitia Ukurasa wa Kundi linalojulikana kama Ligi Kuu ambalo yeye ndio muanzalishi kwenye Mtandao wa kijamii Facebook unajua kile alichokiandika kama sababu ya kumrudisha Stewart John Hall kama kocha wao mkuu mpya namnukuu “ Tangazo Azam FC imeamua kuvunja mkataba na kocha Boris Bunjak na kumrejesha kazini Stewart Hall, hii imetokana na Maombi na Maoni ya mashabiki pamoja na wataalam wa mambo ya ufundi mbalimbali ambao walitoa maoni kuwa ni vema tukamrejesha kocha Stewart Hall. Anicet Njovu, George Massawe, Braza Gossy Bon, Nelson Nsekela, Mphamvu Daniel Donati, Seu Son, Kennedy Mwaisabula, Hamisi Shaku etc, kilio chenu kimesikia, Uongozi wa Azam FC ni sikivu ….” swali la kujiuliza wakati wanamfukuza huyu Kocha waliomba Ushauri toka kwa hawa watu kumi ambao leo wanaonekana Muhimu kiasi cha kuweza kutoa kilio ambacho kinamrudisha mtu madarakani na kumfukuza mtu?? Hawa jamaa hawako serious! Hivi ikitokea siku washabiki wa Simba na Yanga wakiamua jambo lao ambalo si la manufaa kwa timu itakuwaje?? Mimi sioni WEREDI wa hawa watu ambao kila siku wao wanakosoa yale mabaya ya vilabu vingine huku kwao hata hawaangalii nini kinatokea? Miongoni mwa majina yaliyotajwa hapo juu sijui kama wanajua hata dhima kuu ya Azam FC?
Kurudi tena kwa Stewart Hall tena ikisemekana kwa sasa ndio Kocha anaelipwa pesa nyingi kuliko wote Afrika mashariki, Sababu zilizomfukuzisha ukiachana na ile ya kupamisi kwao na familia yake ilisadikika uwezo wake wa Kufundisha umefikia kikomo, sasa swali la msingi kujiuliza hapa ndani ya hii Miezi mitatu ambayo Azam FC walikuwa na Boris Bunjak ina maana Stewart alikwenda kuhudhuria kozi yoyote ile iliyopandisha uwezo wake hadi awe na jipya la kuipatia Azam kwa kipindi hiki kiasi kumpa mkataba mnono kiasi hicho kitu kilichothibitishwa na Mmiliki wa SOFAPAKA Papaa Kalekwa kuwa Azam wanataka kumlipa mara mbili ya pesa walizokuwa wanamlipa wao. Inafika kipindi inatupasa tuwe waKweli, washabiki tuwe wakweli, wanachama tuwe wakweli na Viongozi wetu pia muwe wakweli na mpende kusimamia ukweli na mkubali mnapoambiwa ukweli hasa pale mnapokosolewa na sio kujenga Chuki!

Leo ukienda kumuuliza Mmiliki wa Azam FC nini Malengo yake atakwambia kuzifunika Simba na Yanga na Azam FC iwe timu Bora ndani na Nje ya Nchi ukimuuliza hiyo ndio vision na mission yenu atakujibu hapana, ukimwambia nipe Strategy za kukufikisha huko ataanza propaganda tu ambazo hazina Tija hata kidogo, Ninachokiamini kuna kundi kubwa la watu wanaojiita watu wa Mpira wapo Azam FC ukiwauliza kwanini mpo Azam hawatakupa majibu yakinifu, Utawasikia wakihubiri Hujuma na mambo mengine mengi kama ya Kuifanya Azam kuwa Manchester United ya Bongo ukiwauliza wana UHAKIKA na MANENO yao watakujibu HAWAJUI, hawa sio Viongozi Bora! Mwenye Azam mwenyewe kwa sasa hajui hata Vision na Mission ya Timu yake kifupi Kavurugwa na PROPAGANDA kuwa kuna HUJUMA kubwa ya kuipoteza Azam FC inayofanywa na Simba SC na Yanga SC kama zilivyopotea Palsons FC na Moro Utd FC kwenye Soka letu, hivi ushawahi kujiuliza kwanini Mtibwa Sugar haipotei? Japo kwa siku za karibuni imeyumba kutokana na Sera ya kuuza Wachezaji lakini bado ni Timu shindani ambayo inapata matokeo kwa hivi vilabu vyetu viwili!

Moro Utd FC na Palsons FC zimepotea si kwasababu ya Simba na Yanga la hasha, ni kutokana na Mission na Vision za wenye timu na matatizo ya kifedha, Azam FC haiwezi kukutwa na tatizo la ukata labda tu pale Bidhaa Bora za Bakhresa zipoteze ubora wake na watu ambao ni mimi na wewe na yule pamoja na fanilia zetu na marafiki zetu tuache kuzitumia ipelekee mapato yashuke kitu ambacho sikioni kikitokea leo wala kesho na Azam FC inazitangaza vizuri bidhaa zake na malipo yake ni mauzo makubwa yanayoingiza kipato kwa bakhresa na yeye kuyagawa katika kuendeshea timu, ila waendeshaji wa timu ndio sio watu Thabiti! Wengi wameikuta Azam FC tayari imesimama wanafanya ujanja ujanja tu wasukume maisha yao na si vinginevyo, sioni mapinduzi yoyote yakiletwa na Azam FC kwenye Soka letu, na wala sioni cha kujifunza toka kwa Azam FC kwasababu ninacho kiamini hata timu yangu ya mtaani Biloko FC inaweza kuwa na kiwanja chake, bus lake zuri na vifaa vyote lakini si matokeo mazuri ndani ya uwanja au kuendeleza soka na wachezaji na hata kuendelea kimataifa pasipokuwa na viongozi thabiti, wenye Nia ya kuendeleza Mpira na Wachezaji kwa ujumla wake!

Tanzania hakuna timu tajiri zaidi ya Simba SC na Yanga SC lakini watu wanaopitia pale, sera za vilabu vyenyewe, katiba zao na kundi la watu wenye mawazo mgando limekuwa kikwazo kwa vilabu vyetu pendwa kupiga hatua, sasa utashangaa hata kwa timu hii isiyo na wanachama mbona haiendelei mbele zaidi?? Inakosa watu wa kuipatia tija

Swali la kizushi Miongoni mwa wamiliki au Mmiliki wa Azam FC ni wakala anaetambuliwa na FIFA ina maana hawajui makocha bora wapi wanapatikana? Hajui mbinu za kuendesha timu iwe Bora ndani na nje ya Tanzania? Hajui pa kuwapata wachezaji bora wa kulipwa hadi ahangaike na wachezaji kila msimu wa dirisha dogo na kubwa la usajili? Mchezaji gani wa Tanzania ambae amemfanikisha kucheza Ligi yoyote ile nje ya Tanzania?? Kuna mambo mengi sana ya kufanya bwana Raymond Mlowe na sio hizi siasa zetu eti Azam FC itakuwa mkombozi wa soka letu, tatizo la watanzania wengi wanawaza sana juu ya kushindwa badala ya kushinda na hii ni kwa rika lote kuanzia mtanzania maskini kabisa wa kawaida na Tajiri hadi viongozi wetu hawana uhakika na kile wakifanyacho kama kitafanikiwa au la, na ndio maana yule kiongozi mkubwa kabisa nchini siku chache zilizopita alishangaa kuona tunaweza kutumia Usafiri wa treni kwa wakazi wa Dar es Salaam kwa kwenda kazini na kurudi nyumbani kama wafanyavyo watu wanaoishi kwenye nchi zilizoendelea akisema haamini kama imewezekana! Mimi naamini kwa kujifunza kupitia kwenye makosa yetu na ya wenzetu kila kitu kinawezekana, lakini sio kwa strategy zenu za sasa mlizoamua kuzifuata za usajili mbovu na kufukuza makocha kila kukicha!

Mtapata wapi wachezaji wazuri bila ya kuwa na SKAUTI? Skauti mzuri ni mchezaji wako mwenyewe huyu anajua wachezaji wazuri walipo, Mtibwa Sukari wamenufaika sana na hili na siku zote wamewasajili wachezaji kwa pesa ndogo ambao hawajulikani na hawana chembe chembe za HUJUMA kutoka Simba wala Yanga lakini nyinyi mmengoja kusubiri Mtibwa avumbue muende kugombea na Simba na Yanga mwisho wa siku mmekuwa mkipigwa pesa za kutosha tu kumsajili mchezaji ambae msimu mmoja uliopita alienda Mtibwa Sukari bure sasa iko wapi tofauti yenu na Simba au Yanga?

Mwisho wa Siku eti Azam FC inaitwa VUNA PESA huku kwetu sio kwa WACHEZAJI na VILABU pekee tu HADI MASHABIKI wanafata pesa wanashangilia na mabendera yao makubwa kumbe washavuta MKWANJA WAO UNAO WAFANYA WAPIGE KELELE MWANZO MWISHO PALE TAIFA MPYA NA CHAMAZI! Hii ilishawahi kutokea nyumbani kwetu Morogoro kwenye timu ya Moro Utd watu walikuwa wanaenda kwa aliyekuwa mkurugenzi Bwana Merrey Balhabou kuvuta pesa na kurudi kuendelea na Maisha yao ya kila siku hawakuwa na mapenzi ya dhati na timu ile hata ilipouzwa kutoka Morogoro hakuna aliyejisumbua kutaka kuirudisha wakaiacha iende zake na hadi sasa inazidi kupotea hakuna anaeijali.

Napenda kumalizia hivi Raymond Mlowe on your Dreams Kaka mje muishike Tanzania nini Afrika mtangoja MIAKA MIA NANE mfikie mnapotaka maana yake mimi na wewe hatutakuwepo kipindi hicho sio leo wala kesho! Coz kimipango kwenye makaratasi Azam Fc wako vizuri saaaana lakini sio kwenye kuitekeleza nasubiri kuona Azam FC wakini-prove wrong!

Eric zomboko (dizo moja)

 

Sambaza....