Sambaza....

Yanga waliingia na mfumo wa 4-4-2 Diamond wakati Wallayta Dicha walikuwa wanacheza mfumo wa 4-4-2

Lakini pamoja na kwamba Yanga kwenye karatasi ilionekana wanacheza 4-4-2 Diamond , uwanjani walionekana kucheza bila mshambuliaji halisi wa katikati , ambapo Raphael Daud alikuwa anacheza kama false 9

Kitu ambacho kilikuwa kinamsaidia kushuka chini katikati kuchukua mipira hali ambayo ilikuwa inawalazimu mabeki wa Wallayta Dicha kupanda juu yao na kuacha uwazi kule nyuma, uwazi ambao ulikuwa unatumiwa na kina Yusuph Mhilu pamoja na Emmanuel Martin , wakati mwingine Ibrahim Ajib.

Hiki ndicho kilikuwa msaada mkubwa wa Yanga katika eneo la Mbele, ambapo iliruhusu wachezaji wengi wa Yanga kuwa katika eneo la box kipindi walipokuwa wanashambulia.

Walipokuwa wanashambuliwa Yanga, wachezaji wawili walikuwa wanakuja katikati kuungana na Kamusoko na Pius Buswita katika eneo la katikati, ambapo Emmanuel Martin na Ibrahim Ajib ndiyo walikuwa wanaongeza idadi ya watu eneo la katikati , hivo Yanga ikawa inakuwa na watu wanne dhidi ya wawili wa Wallayta Dicha.

Hali hii ilikuwa ngumu sana kwa Wallyta Dicha kwa sababu walipokuwa wanajaribu kwenda mbele kuanzia katika eneo la katikati Yanga waliwapokonya mipira na kuanza kushambulia kwa kasi kuanzia eneo la katikati.

Kitu ambacho kilikuwa kinawagharimu Yanga walipokuwa wanaanza kushambulia ni Ibrahim Ajib kupoteza mipira mingi sana.

Upi ulikuwa ubora wa Wallyta Dicha katika mechi ya leo?

Kumiliki kwao mpira kulikuwa na msaada kwao kwa sababu waliwezesha kupunguza kasi ya Yanga

Lakini walipokuwa wanamiliki mpira walikuwa wanamiliki mpira bila tahadhari na wao kutengeneza uwazi sehemu mbalimbali ndani ya uwanja.

Uwazi huu ulikuwa unatumiwa na wachezaji wa Yanga, mfano magoli yote mawili ya Yanga yamefungwa wakati ambao wafungaji wa Yanga walipokuwa katika eneo ambalo kulikuwa na uwazi hivo kuwa na uhuru zaidi wa kupiga kichwa.

Pili, magoli yote ya Yanga ƴyamefungwa kutokana na mipira ya krosi (mipira ya juu) hii inaonesha kabisa udhaifu mkubwa wa Wallayta Dicha wakati wanajizuia ni mipira ya juu

Upi ulikuwa ubora wa Yanga?

Nidhamu yao ya kujilinda ilikuwa silaha kubwa kwao, utulivu ilikuwa mkubwa kuanzia kwa golikipa mpaka kwa viungo wa kati.

Kuanzia katikati mpaka nyuma Yanga walikuwa wanajilinda vizuri hawakuruhusu presha kubwa ndani yao hali ambayo iliifanya timu iwepo ndani ya mchezo kwa muda mrefu.

Tatizo kubwa ambalo walikuwa nao Yanga ni nidhamu ya matumizi ya nafasi walizokuwa wanazipata ambapo Yusuph Mhilu pamoja na kucheza vizuri leo lakini yeye pamoja na Ibrahim Ajib walikosa nafasi nyingi ambazo zingeiwezesha Yanga kuwa na mtaji mkubwa kwao.

Hitimisho: Tangu msimu huu uanze Yanga haijawahi kufungwa magoli kuanzia 3-0 katika mechi moja, ushindi wao wa magoli 2-0 utawalazimu Wallayta Dicha kushinda magoli 3-0 dhidi ya Yanga ili wapite katika hatua ya makundi kitu ambacho Yanga hawajawahi kuruhusu msimu huu, hivo kwa 75% Yanga watakuwa wana nafasi kubwa ya kufuzu kwenda katika hatua ya makundi

Sambaza....