Mashindano

Kilimanjaro Warriors wapania kupindua Meza dhidi ya Burundi.

Sambaza....

Kikosi cha timu ya soka ya Taifa chini ya umri wa miaka 23 ‘Kilimanjaro Warriors’ kesho, Novemba 20, 2018 kitashuka dimbani kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza dhidi ya Burundi kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika mwakani nchini Misri.

Kilimanjaro Warriors wanashuka katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 2-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika nchini Burundi, hivyo watahitaji ushindi wa zaidi ya maba0 3-0 ili kusonga mbele.
Kocha wa Kilimanjaro Warriors Bakari Shime amesema kikosi chake kimeimarika kiufundi na kitimamu kwani katika mchezo wa awali kuna wachezaji ambao waliwakosa lakini kwa sasa watakuwa nao.

Shime amesema lazima wapindue matokeo ya mchezo wa mkondo wa kwanza na hicho ndicho watakachoenda kukifanya kwani wanajiamini kuwa na uwezo wa kufanya hivyo na wachezaji walionao wanauwezo wa kutosha wa mechi za kimataifa.

“Kwa upande wetu maandalizi yamekamilika kwa maana ya ufundi, wachezaji wapo vizuri kabisa tunafahamu tunamchezo mgumu mbele yetu, ni mchezo wa pili baada ya ule wa awali na sisi kupoteza kwa mabao mawili kwa sifuri,”
“Kimsingi tumeona mapungufu yetu na tumeyafanyia kazi naamini kabisa kwa uwezo wa Mungu kesho tutaweza kuyapindua matokeo, kuna namba ya wachezaji ambao hatukuwa nao Burundi kwa shida tofauti tofauti…. Lakini sasa wote wapo timamu tumejaribu kuwajenga vijana wetu kufahamu umuhimu wa mchezo……pili ni wachezaji wenye uzoefu wanacheza ligi kuu, wanacheza vilabu vikubwa wamecheza michezo mingi ya Kimataifa,” Shime amesema.

Kwa upande wake kocha wa Burundi Omari Nakagero amesema kikosi chake kipo kamili kwa ajili ya kuwavaa Tanzania, na kwamba atacheza mchezo wa kushambulia muda wote ili kuweza kulinda ushindi alioupata nyumbani.

“Wachezaji wote wapo vizuri, na naamini hakutakuwa na mabadiliko kikosi ni kile kile kilichoshinda Burundi hakuna mgonjwa, tunajua mechi ni ngumu Tanzania watataka wajibu zile goli mbili……Tumekuja kucheza, tumewaambia vijana tukitaka vizuri lazima tushambulie, tukizuia watapata nafasi ya kucheza na wanaweza kutufunga, hivyo tutashangalia,” Nakagero amesema.

Viingilio vya mchezo huo utakaoanza saa moja kamili jioni, vitakuwa shilingi 5000 kwa VIP na Shilingi 1000 kwa nafasi nyingine, na Shirikisho la soka nchini TFF limesema maandalizi yote yameshakamilika kwa maana ya waamuzi na viongozi wengine.

Kama Tanzania itafanikiwa kupita hatua hiyo watacheza mchezo mwingine Machi 2019 na watacheza na Congo kabla ya kucheza hatua nyingine ya mwisho itakayowawezesha kwenda Misri kushiriki michuano hiyo inayotarajiwa kufanyika Novemba 8-22 ambapo pia washindi watatu watapata nafasi ya kufuzu kwenye mashindano ya Olmpiki 2020 Tokyo, Japan.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x