Sambaza....

Kwenye mechi kumi (10) kabla ya jana alikuwa amefanikiwa kufunga magoli mawili (2)pekee, hapana shaka tangu kifo cha mama yake kiwango chake kilikuwa cha kupanda na kushuka.

Hakuwahi kusimama kwenye kiwango bora kwa muda mrefu mara baada ya mama yake kuachana naye na kwenda kwenye makazi yake ya milele.

Alikaa darajani akiwa mpweke sana, ule msaada aliouonesha kwenye msimu ambao Leicester City ( 2015/2016) ulipungua kwa kasi kubwa sana, msimu huo alionekana ndiye mwenye msaada mkubwa zaidi kwenye timu mara.

Kwa mara nyingine jana alisimama kama mtu mwenye msaada mkubwa kwenye timu.

Willian Borges da Silva jana alianza kwenye kikosi cha Antonio Conte ambacho kilirudi kwenye mfumo wake wa msimu uliopita wa 3-4-3, wakati wapinzani wao Barcelona walicheza mfumo wa 4-3-3.

 

Lakini kulikuwa na mabadiliko ya kimfumo kwa kila timu kutokana na hali ilivyokuwa inabadilika ndani ya mchezo.

Mfano, Chelsea walipokuwa wanazuia walikuwa wanatumia mfumo wa 5-4-1. Ambapo Marcus Alonso na Victor Moses walikuwa wanarudi nyuma kuungana na mabeki watatu na kuongeza idadi ya watu watano nyuma, huku wakimwacha Hazard mbele.

Messi akifanya yake

Barcelona walikuwa wanatumia mfumo wa 4-3-3 wakati wanashambulia, lakini walipokuwa hawana mpira Iniesta alikuwa anarudi katikati kuongeza idadi ya wachezaji na kutengeneza mfumo wa 4-4-2 wenye umbo la Diamond.

Wapi Chelsea walifanikiwa wakati wakujilinda?

Moja ya silaha kubwa ambayo Barcelona wako nayo kwa muda mrefu na wanaitumia bila kuisha makali ni Lionel Messi, jana alikuwa anashuka chini katikati, kushuka kwake chini walikuwa wanatarajia beki mmoja wa Chelsea kushuka naye kumkaba ili Chelsea watengeneze uwazi eneo la nyuma , uwazi ambao ungetumiwa na Luiz Suarez, lakini kila Lionel Messi alipokuwa anashuka katikati hakuna beki wa Chelsea aliyekuwa anashuka naye.

Conte akihamaki baada ya Willian kugongesha mwamba

Hali hii ilisababisha eneo la nyuma la Chelsea kutokuwa na uwazi muda mwingi mwa mchezo, ndiyo maana wakati Barcelona walipokuwa na mpira katika eneo la Chelsea ilikuwa ngumu kwao kupenyeza eneo la kumi na nane kwa sababu hakukuwa na uwazi wa kupitishia mipira.

Kipi kilisababisha Chelsea kusawazishiwa?

Moja ya faida kubwa waliyokuwa nayo Barcelona ni wao kuanzia kukabia juu, hali ambayo ilisababisha mabeki wa Chelsea kufanya makosa na kupoteza umiliki mpira.

Mfano goli la Lionel Messi , Chelsea walilazimishwa kufanya makosa kutokana na Barcelona kukabia juu kitu ambacho kilimpelekea Andreas Christensen kupoteza umiliki wa mpira na Barcelona kuwaadhibu Chelsea.

Kipi kilisababisha Chelsea kutangulia kufunga goli?

Wakati Barcelona wakinufaika na kukabia juu, Chelsea walikuwa wananufaika na wao kuwa na wachezaji wenye kasi (pace) kule mbele, kitu ambacho kilikuwa kinawapa faida ya wao kulazimisha kufanya mashambulizi kwa kasi.

Eden Hazard ndiye alikuwa funguo la goli la Chelsea , alicheza kama false 9 mara nyingi alikuwa anakuwa huru kushuka chini na kuwalazimisha mabeki wa Barcelona kutengeneza uwazi eneo la nyuma, uwazi ambao mara nyingi ulikuwa unatumiwa na Willian.

Mkwaju wa Willian kuelekea kwenye mwamba

Mfano kabla hajafunga goli, alipiga mashuti mawili yaliyogonga mwamba, wakati anapiga mashuti hayo alikuwa huru kwa sababu alikuwa sehemu ambayo kulitengenezwa uwazi uliotokana na Hazard kushuka chini, hata goli la kwanza alilofunga, kafunga akiwa eneo ambalo ni huru na alitumia uwazi ulioachwa na mabeki wa Barcelona.

Jana Willian alikuwa ndiye nyota wa mchezo na karata ya Conte kuamini miguu ya Samba aliichanga vyema, wengi wanaweza kuongelea kwa ukubwa na upana kuhusu Lionel Messi kuvunja mwiko wa kutoifunga Chelsea baada ya michezo nane , lakini kiwango cha Willian ndicho kitu kizito kinachostahili kuongelewa lakini kwa sababu kimefanywa na mtu mwepesi watu watakichukulia kiwepesi

Sambaza....