Sambaza....

Klabu ya soka ya Alliance School ya Jijini Mwanza imesema bado haijatangaza kocha mkuu licha ya taarifa kuonea kuwa tayari wameshaingia mkataba na kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Rwanda Pappi Kailanga.

Afisa habari wa klabu hiyo Jackson Luka Mwafulango amesema ni kweli wamekusudia kubadilisha benchi la ufundi kuelekea ligi kuu soka Tanzania Bara msimu ujao lakini bado hawajatangaza ni nani ambaye wamemuongezea hivyo amewaomba wapenzi wa timu hiyo kuwa wavumilivu wakati ambapo uongozi unashughulikia suala hilo.

“Mpaka sasa bado sijapewa mamlaka na uongozi kulizungumzia hilo la kocha mpya, bado mchakato unaendelea, ila ni kweli tumekusudia kufanya mabadiliko makubwa kwenye benchi la ufundi, anaweza kuwa Kailanga au Mbwana Makata, yote hayo ni kusubiri taarifa kamili ya klabu,” Mwafulango amesema.

Kwa siku takribani sita sasa kumekuwapo na taarifa za Alliance kuingia mkataba na kocha huyo ambaye aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Amavubi kwa ajili ya msimu ujao, baada ya kuonekana akiwa sambasamba na Mkurugenzi James Marwa Bwire katika mgahawa mmoja hapa jijini Mwanza.

Katika hatua nyingine Mwafulango amesema kuwa wanatarajia kuweka kambi nje ya Tanzania, huku akitaja nchi kama Uganda, Malawi, Botswana na Rwanda kuwa sehemu ambazo wamependekeza.

Alliance imepanda daraja kwenda ligi kuu pamoja na timu za Coastal Union ya Tanga, Kinondoni Municipal Council, JKT Tanzania na African Lyon za Dar es Salaam pamoja na Biashara United ya Mara.

Sambaza....