Blog

Antonio Nugaz haoni AIBU kuongea UONGO na kuwa msema HOVYO?

Sambaza....

Hakuna kitu cha kawaida kwa sasa kama kuongea UONGO kwenye mpira. Ni kitu cha kawaida sana na kimehararishwa kabisa na wenye mpira wao. Kuna wakati unaweza kuona bila uongo mpira wetu hauwezi kwenda , na hii ni kwa sababu uongo huzaa matumaini ya uongo.

Matumaini ambayo wengi wa mashabiki huyapenda sana. Na mara nyingi mashabiki hujiona wao ni wababe sana kwa sababu ya uongo wanaoaminishwa na viongozi wao , hasa hasa hawa wanaojiita wasemaji au Ma Afisa habari wa vilabu.

Bila shaka unajua tambo za Masau Bwire, Afisa Habari wa Ruvu Shooting. Na nina uhakika hujasahau mbwembwe za Thobias Kifaru , Afisa Habari wa Mtibwa Sugar. Hawa kwa kutumia vinywa vyao unaweza ukafikiria hizi timu hazikuzaliwa hapa Tanzania.

Wana ndimi tamu , ndimi zinazojua kupaka make-up kwa ustadi mkubwa kuzidi mikono ya Maznath Bridal. Cha kusikitisha hizi ndimi zimeanza kuwa nyingi na zinaonesha kabisa kuwa silaha ya ndimi zao ndiyo ukubwa wa biashara yao. Lakini kuna kitu kimoja tu ambacho wanakosea.

Wanatumia ndimi zao vibaya , wanatumia ndimi zao kusema hovyo. Huwezi kukosea utakaposema hawa ni Ma-Afisa wasema hovyo wa vilabu. Wanavisemea hovyo sana vilabu vyao. Sawa kuna wakati mwingine wanaziongoza vyema ndimi zao lakini kuna wakati ndimi zao zinakuwa haziongozwi vyema na bongo zao.

Ukweli uliowazi ni kuwa Hassana Bumbuli na Antonio Nugaz ujio wao ulikuwa kwa ajili ya kupambana na Haji Manara. Huu ndiyo ukweli kabisa. Wana Yanga wengi wanaamini Simba ilifika pale kwa sababu tu ya ulimi wa Haji Manara, Yanga wakaamua kutafuta Haji Manara wao.

Ulimi wa Antonio Nugaz ukakabidhiwa majukumu hayo. Ingawa kwa Mara ya kwanza alikataa kabisa kuwa hajaja kupambana na Haji Manara ila amekuja kukuza chapa (brand) ya Yanga kupitia ulimi wake na akaongeza kwa kusema yeye hatokuwa msema hovyo.

Muda umezidi kudhihirisha uongo wake na ukweli wake. Uongo ni kuwa Antonio Nugaz hajaja kupambana na Haji Manara, ukweli ni kuwa Antonio Nugaz amekuja kupambana na Haji Manara. Ni ngumu sana kwake yeye kuiongelea Yanga bila kumtaja Haji Manara.

Uongo wa Antonio Nugaz umepitiliza mpaka amekuwa msemaji asiyetafakari kwa kina. Kwanini nasema hivo ?. Jana nimekutana na mahojiano kati ya Antonio Nugaz na mtandao wa BONGO 5. Mahojiano ambayo yalinifanya nianze kufikiria namna ya kumpeleka Antonio Nugaz katika kundi la wasema hovyo wa vilabu.

Antonio Nugaz anatudanganya kuwa uwekezaji mkubwa siyo kitu chochote kwenye mpira wa miguu. Hapa alikuwa anawazungumzia wapinzani wao katika mechi ya kombe la shirikisho barani Afrika, Pyramid FC. Alibeza uwekezaji wao na kuzidi kuwaaminisha wana Yanga kuwa uwekezaji siyo kitu kwenye mpira.

Haya ni matumaini ya uongo ambayo yanajaribu kujengwa kwenye damu za mashabiki wa Yanga. Matumaini ambayo yanatumia maji , udongo na tofali za uongo, kitu ambacho kinatia hofu kuhusu uimara wa nyumba ambayo wanaijenga kwa pamoja.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.