Sambaza....

Haruna Akidhimana Fadhil Niyonzima amerudi katika ubora wake huku klabu yake ya Simba sc ikiwa katika wakati muhimu kabisa katika msimu huu haswa klabu bingwa Africa na hata ligi kuu Bara. Haruna yule “mtoto wa Kisenyi – Rwanda” ni kama anaturejesha miaka ya nyuma alipokua Yanga akiwa kwenye ubora wake.

Kiwango cha Haruna Niyonzima kimeimarika haswa katika michuano ya Mapinduzi huko Zanzibar kiasi cha kuwafurahisha mashabiki wa Simba na hata benchi la ufundi wa Simba. Kutokana na kuonyesha kiwango bora ilipelekea kuchaguliwa mchezaji bora wa katika mchezo uliowakutanisha Simba dhidi ya Mlandege baada ya kufunga bao moja lililowapa ushindi Simba huku yeye akiwa nahodha.

Kurudi kwa kiwango cha Niyonzima ni kama “timing” nzuri kwake na klabu ya Simba haswa kutokana na Simba kuwepo katia hatua ya makundi katika Klabu Bingwa Africa. Kwa kiwango cha Haruna kwa sasa hakika mwalim Auseems hatosita kumpa nafasi uwanjani ili kuonyesha mavitu yake mguuni.

Sina shaka na uzoefu wa Haruna Niyonzima mashindano haya kutokana na kucheza muda mrefu akiwa na klabu ya Yanga kabla ya kuhamia Simba. Ameshiriki zaidi ya mara nne mfululizo akiwa na Yanga huku mara moja walifika hatua ya makundi katika kombe la Shirikisho Africa huku baadhi ya michezo akiwa kama nahodha.

Kwa klabu ya Simba kuelekea katika michezo ya makundi ya klabu Bingwa Africa ni kama wamefanya usajili mpya kwa kurudi kwa kiwango kile cha Haruna Niyonzima. Hii ni kutokana na uzoefu na uwezo wake alionao katika michuani hiyo.

Kwa sasa Simba sc ni kama imepata msaidizi wa Chama ndani ya uwanja na hivyo kuongeza ubunifu katika eneo la mwisho la adui. Pasi za mwisho, umiliki wa mpira, kasi akiwa na mpira na uwezo mkubwa wa kukaa na mpira ni kama ingizo jipya Simba kuelekea kutafuta nafasi ya kufuzu robo fainali.

Sambaza....