Ligi Kuu

Haukuwa muda sahihi kwa Pierre kuja Simba

Sambaza....

Rasmi Simba jana imeingia mkataba na kocha Mfaransa Pierre Lenchantre na anatarajiwa kuanza kazi na kikosi cha Simba jumanne.

Ni kocha mwenye elimu kubwa ya ukocha , hapana shaka ana mafanikio makubwa pia katika mpira wa Afrika.

Mshindi wa Afcon mwaka 2000 akiwa na Cameroon na akafanikiwa kuwa kocha bora wa CAF mwaka 2001.

Elimu yake kubwa ya UEFA pro licence aliionesha kwa vitendo uwanjani akiwa anaifundisha Cameroon.

Sifa kubwa zikawa juu yake na heshima kubwa akawa nayo.

Ni moja ya makocha wenye mafanikio na soka la Afrika.

Siyo mgeni na mpira wa Afrika kwani ashafanikiwa kufundisha mpira Cameroon, Congo Brazzavile , Tunisia.

Hana ugeni wowote na mpira wetu wa Afrika, ni moja ya faida kubwa ambayo Simba wanaenda kunufaika nayo kutoka kwa huyu ƙkocha.

Simba imekuwa timu yenye bahati kubwa ya kupata makocha wenye historia nzuri na mpira wa Afrika.

Hata kocha mkuu aliyepita, Joseph Omog alikuwa na historia nzuri na soka la Afrika.

Aliwahi kushinda kombe la shirikisho barani Afrika akiwa na AC Leopards ya Congo.

Akafanikiwa kuwa kwenye orodha ya makocha watatu ambao waliingia hatua ya mwisho ya kuwania tunzo ya kocha bora wa Afrika mwaka 2012.

Lakini alipofika Simba hakufanikiwa kwa kiasi kikubwa kama ambavyo alikuwa AC Leopards.

Inawezekana mashabiki wa Simba kwa sasa wanamatumaini makubwa na kocha Pierre Lechantre.

Wakiamini kuwa anaweza kuwa tiba sahihi kwao wao kwenye ugonjwa wa kutobeba ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania kutokana na historia yake inavyombeba.

Inawezekana ikawa sahihi kwao kuwa na matumaini kwao, lakini inaweza ikawa kamari pia.

Wanatakiwa waelewe hivo kwamba hii ni kamari ambayo inaweza ikawa kweli au isiwe kweli.

Na kamari hii inaonekana kuwa ngumu kufanikiwa kuwa kweli kwa sababu ya kipindi ambacho kocha huyu kaja.

Masoud Djuma

Kaja kipindi ambacho timu ipo katikati ya Ligi. Lazima anapokuja kwenye kikosi hiki atajaribu kuingiza falsafa mpya za kwake anazoziamini ili timu ifanye vizuri.

Falsafa hii inaweza ikawa tofaufi na watangulizi wake ( Joseph Omog na Masoud Djuma)

Hivo wachezaji watalazimika kuanza kujifunza kitu kipya tofauti na cha awali.

Kwa maana nyingine timu inaanza upya tena.

Tuliona hiki kitu kipindi ambacho Joseph Omog anaondoka, Kocha Masoud Djuma ilimchukua takribani mechi tano kuhakikisha falsafa yake angalau inaanza kueleweka na wachezaji wa Simba.

Kocha huyu mpya anakuja na kitu chake kipya, kitu ambacho kitachukua muda kueleweka kwa wachezaji.

Haijalishi muda ambao utatumika wachezaji kuelewa, uwe muda mfupi au mrefu, muda ambao Simba itakuwa inasubiri falsafa za kocha huyu ziweze kueleweka vizuri kwenye kikosi cha Simba ndiyo muda ambao wapinzani wake watautumia kumzidi.

Tukunbuke mpaka sasa Simba yuko mbele ya alama mbili mpaka sasa dhidi ya Azam FC, ni alama chache ambazo hazimpi nafasi ya yeye kujiona yuko huru kukimbia katika mwendo anaoutaka yeye.

Nilikuwa nafikiria kama Simba wangeamua kumwachia kocha Masoud Djuma amalize ligi ya msimu huu ungekuwa uamuzi wa busara sana kwa sababu mpaka sasa hivi inaonesha kuna kitu kikubwa amekiweka ndani ya kikosi cha Simba.

Kuna maelewano ameyajenga kati yake na wachezaji.

Wachezaji wanacheza kwa kuelewana ndani ya uwanja.

Wachezaji wanayofuraha kwa sasa ndani ya mfumo wa kocha Masoud Djuma.

Wanakuja tena kuhamishwa na kwenda katika mfumo mpya wa kocha mpya, hatujui kama watakuwa na furaha au La kucheza ndani ya mfumo mpya wa kocha Pierre Lenchantre.

Na hii pia inachangia kuwachanganya wachezaji kwa sababu ndani ya msimu mmoja mchezaji anakuwa chini ya makocha watatu wenye falsafa tofauti.

Mchezaji anakuwa mtu wa kuanza upya kila mara.

Hivo kuepukana na vyote hivi naamini kocha Masoud Djuma alikuwa mtu sahihi kuachiwa timu mpaka mwishoni mwa msimu mwa msimu huu, ujio wa Pierre Lenchantre katikati ya ligi haukuwa wakati mzuri kwa timu ya Simba.Kungekuwa na faida kubwa sana kama Pierre angeanza na Simba msimu ujao ili apate muda mwingi na sahihi kuweka kitu anachokiamini kwenye kikosi, kipindi hiki Simba ina presha kubwa ya kushinda kombe muda huu hivyo hatokuwa na mazingira tulivu ya kuweka falsafa anazoziamini ndani ya mazingira yaliyopo sasa hivi

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x