Tahariri

Huyo mtu wa kufumua MFUMO wetu wa Soka yuko wapi?

Sambaza kwa marafiki....

Kuna hadithi ambayo imesimuliwa sana kwenye vipindi vya michezo kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Magazeti na Mitandao yetu, ikiwemo kandanda.co.tz imeandika sana hii habari kwenye makala mbalimbali. Makala ambazo kimsingi hubeba njia sahihi na nzuri kufikia sehemu ya mafanikio ya mpira wetu.

Sehemu ambayo kila mpenda mpira huiota kuifikia. Hakuna ambaye hapendi kuiona timu yetu ya Taifa ikishiriki michuano mikubwa kama AFCON na kombe la dunia. Hakuna kabisa asiyependa. Hakuna ambaye hapendi kuishuhudia klabu yoyote hapa nchini ikichukua kombe la ligi ya mabingwa Afrika au lile la shirikisho Afrika.

Hakuna asiyependa kuwa sehemu ya historia hiyo. Lakini tatizo hakuna ambaye anashiriki kikamilifu kuitengeneza hiyo historia.

Tumekuwa watu wa matukio na siyo watu wa mifumo. Tunasubiri timu yetu ya Taifa ikiwa kwenye kampeni ya kufuzu Afcon. Hapo ndipo utakapoona kampeni nyingi zinakuja. Mara saidia Stars ishinde, Mara Tanzania mpaka Gabon.

Huwa zinakuja kampeni nyingi sana. Na hizi kampeni huja kwa sababu ya tukio husika. Na mwisho wa siku kampeni hizi huwa siyo endelevu. Tumekuwa watu wa kuendeshwa na matukio tu. Hakuna mikakati endelevu ya kufika sehemu ambayo tunaiota kufikia.

Unaikumbuka kampeni ya Simba ya mwaka huu kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika?, michuano ambayo mpaka sasa hivi inaendelea?

Ile ya YES WE CAN?, Ni kampeni ambayo imekuja kwa sababu ya tukio tu. Tena tukio ambalo lilisabàbishwa na mtu ambaye aliwaambia Simba ni UNDER DOG. Kuwaonesha kuwa wanaweza kufika mbali ndiyo wakaja na kampeni hii ya YES WE CAN. Hii ilikuwa mahususi tu kumkomesha tena mtu huyo!.

Na ndiyo maana imeanza kufifia baada ya kupokea kipigo cha jumla ya magoli 10 katika mechi mbili zilizopita za ligi ya mabingwa barani Afrika.

Hata Taifa Stars juzi juzi tulibebwa hisia zetu na tukio la timu yetu ya Taifa kupewa ndege ya serikali kwenda Cape Verde. Na wengi wakapandwa na mzuka wakaamini wanaenda kushinda.

Lakini mwisho wa siku hakuna tulichofanyika. Unajua ni kwanini ?, jibu simpo tu. Tumekuwa watu wa kuendeshwa na matukio na siyo mfumo.

Mara nyingi mimi nimekuwa nikisikia hadithi hii yenye kichwa cha habari kinachosema TUFUMUE MFUMO WETU WA SOKA.

Ni hadithi nzuri sana na husimuliwa kila mwaka na kila timu zetu zinapofanya vibaya kwenye michuano ya kimataifa.

Ni hadithi ambayo imebeba mambo ambayo ni ya msingi. Mambo ambayo huchukua muda mrefu sana kuonesha matunda yake.

Lakini cha ajabu hadithi hii sijawahi kuona ikiwekwa kwenye vitendo. Kila uchwao imekuwa ikirudiwa sana kusimuliwa bila mafanikio yoyote.

Kipi kimekosekana.?, nani haswa kakosekana? Au ni nani ambaye ana jukumu la kufumua huo mfumo ?

Na huyo mwenye hilo jukumu la kufumua mfumo wetu wa soka yuko tayari ?, hapa jibu ni dogo tu. Hayuko tayari ndiyo maana tunashuhudia madudu kila kukicha kwenye mpira wetu.

Rais wa Shirikisho la Mpira Tanzania, TFF, Wallace Karia.

Hakuna kiongozi anayewaza maendeleo ya soka. Wengi wao wanawaza migogoro kwa ajili ya kutetea tu tumbo lao. Matumbo yetu ya mpira yana njaa sana. Yamekosa mpishi sahihi wa kutupa chakula cha kutushibisha sisi ili tusiendelee kupata hii aibu.

Namtafuta sana mwenye jukumu hilo la kufumua huo mfumo wetu wa mpira, nimuulize tu kiustaarabu uko tayari kufumua huo mfumo?

Ni lini utaufumua huo mfumo wetu wa soka na hujachoka kusoma makala ambazo zinakusisitiza kufumua mfumo wetu wa soka?

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.