Ligi Kuu

Juma Mgunda na utamu wa Coastal Union yake!

Sambaza....

Mwanzo kabisa wa msimu huu 2021/2022 Coastal Union “Wagosi wa Kaya” wenye maskani yao jijini Tanga walichagua kuanza na Mmarekani Melis Medo kama Mwalimu mkuu wa timu, ambaye aliiongoza timu kwa muda mpaka Wanamangush walipoamua kuachana nae.

Tarehe 31/03/2022 Idara ya habari na Mawasiliano ya Coastal union Fc walithibitisha kumrudisha kwenye kiti Mwalimu Juma Mgunda ambaye katika kipindi cha Melis Medo alibadlishiwa majukumu na kuwa Mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo.

Juma Mgunda (mwenye koti la bluu) akizungumza na wachezaji wake wa Coastal Union.

Jahazi la Coastal Union limeonekana kuwa katika mikono salama chini ya mchezaji huyo wa zamani wa Coastal Union akisaidiwa pia na Juma Lazaro mchezaji mwenzie wa zamani pia. Mgunda aliikuta timu katika mechi kumi (10) za mwisho ikiwa na takwimu za kushinda michezo mitatu, kupoteza michezo sita na sare moja. Lakini pia bado ilikuwepo katika michuano ya AzamSports Federation Cup.

Baada ya kurejea katika majukumu yake ya mwanzo (Kama Mwalimu mkuu wa timu) mpaka sasa ameshaiongoza timu katika mechi tisa (9) na huu ndio mfululizo wa matokeo yake katika mechi hizo:

Mshambuliaji wa Coastal Union Adam Uledi “Balle” akimuacha mchezaji wa Polisi Tanzania.

Katika michezo tisa, Juma Mgunda ameshinda michezo minne, amepoteza michezo mitatu na kupata sare michezo miwili pekee, hivyo kuisaidia Coastal kukusanya alama kumi na nne kati ya ishirini na saba.

Sasa Coastal Union imebakiwa na michezo dhidi ya Yanga na Namungo ugenini, halafu watamalizia nyumbani dhidi ya Geita Mkwakwani Tanga.

Wachezaji wa Coastal Union wakishangilia.

Mpaka sasa Coastal Union inashika nafasi ya sita ikiwa na alama 34 ikishuka dimbani katika michezo 26. Lakini Pia Coastal chini ya Juma Mgunda imefanikiwa kufika nusu fainali ya kombe FA na Jumapili itakua mkoani Arusha kukipiga dhidi ya Azam Fc.


Sambaza....