Sambaza....

Kuna wengine watakumbuka sanaa ambayo alikuwa akiionesha uwanjani, magoli aliyokuwa anayafunga yanaweza yakawa kumbukumbu kubwa vichwani mwa wengi.

Kuna mengi sana ya kumkumbuka huyu gwiji wakati akiwa mchezaji lakini kuna mengi ya kuyatukuza ya huyu gwiji kipindi alipoamua kuwa kocha.

Alitamani kubadilisha mpira wa miguu na kuna wakati alitamani dunia nzima icheze aina ya mchezo ambao alikuwa anaufikiria kichwani mwake.

Kwake yeye hakuwaza timu kushinda pekee, lakini alichokuwa anakiwa ni namna gani timu imeshinda mchezo husika.

Haimanishi kuwa alikuwa haipi uzito timu kushinda, la hasha lakini alichokuwa anataka timu ishinde ikiwa imecheza mpira wa kuvutia.

Kwake yeye alikuwa hapendi timu kufungwa ndiyo maana aliwahi kusema kuwa kama utashindwa kushinda hakikisha unaifanya timu yako isifungwe.

Neno kufungwa lilikuwa mbali sana na ubongo wake, kichwani mwake neno ushindi lilikuwa limetawala na aliliongezea thamani neno ushindi kwa kuhakikisha ushindi unapatikana kipindi timu imecheza soka la kuvutia.

Alitaka kuufanya mchezo wa mpira wa miguu uwe sehemu ambayo mchezaji atafurahia kucheza na shabiki atafurahia kutazama mchezo husika.

Alitaka timu yote ihusike kucheza kuanzia golikipa mpaka mshambuliaji wa mwisho, ndiyo maana aliamini kuwa katika timu yake golikipa ndiye mshambuliaji wa kwanza.

Mwanzoni ilikuwa ngumu kwa wengi kumuelewa, ilikuwa ngumu kwa wengi kumwamini. Watamwamini vipi wakati ambao masikio yao yanasikia kutoka kwake kuwa golikipa ni mshambuliaji wa kwanza?

Ilikuwa ngumu kueleweka kwa wakati huo. Kipa kuwa mshambuliaji wa kwanza?, hapana shaka wengi walikuwa wanaamini kuwa anatania , hivo wengi walimpuuzia na wachache walimfuata.

Akabeba wafuasi wachache sana, wafuasi ambao walimwamini na yeye akawaamini kuwa kupitia hawa wanaweza kueneza injili ambayo alikuwa anaiamini.

Johan Cruyff

Alichagua watu ambao wangeweza kueneza injili yake kwa nguvu kubwa ili ienee kwa kasi. Moja ya watu ambao aliwachukua ni Pep Guardiola.

Huyu aliwekeza kila kitu chake kwenye kichwani cha Mhispania huyu, alitaka siku moja dunia icheze kwa pamoja. Kipa awe sehemu ya kuanzisha mashambulizi, ndiyo maana alimuona ndiye mshambuliaji wa kwanza.

Aliamini kupitia kipa ambaye anauwezo wa kucheza mpira au kupiga pasi (ball player), aliamini timu imara ni ile ambayo kipa wake anaanzisha mashambulizi vizuri kwa pasi fasaha.

Alilisimamia hili na hata wafuasi wake aliwaaminisha kuwa hili linawezekana ndiyo maana hata baada ya yeye kufa wafuasi wake waliendelea kuendeleza imani ambayo alikuwa anaiamini Johan Cruyff.

Taratibu Pep Guardiola alianza kuifanyia kwa vitendo mara baada ya kupewa Barcelona. Alitaka kipa mwenye kujiamini anapokuwa na mpira miguuni mwake.

Alitaka kipa ambaye anauwezo wa kupiga pasi nyingi kwa ufasaha ndani ya mchezo mmoja, alitaka kipa ambaye anauwezo wa kutoka katika eneo lake na kusogea nje ya eneo lake ili tu awe na uwezo wa kuhusika kwenye mchezo kwa pamoja.

Dunia ilikuwa inamshangaa lakini yeye alitafuta sababu ya kuishangaza dunia, na alifanikiwa kwa hilo, alipata mafanikio makubwa sana kupitia imani yake.

Na aliendelea kuihubiri hii imani hata alipoenda Bayern Munich na alipokuja kwenye ligi pendwa ya England aliendelea na imani hiyo.

Imani ambayo makocha wengi kwa sasa wanaifuata wameshakubaliano nayo, wanaiona ina faida kubwa kwa sasa. Ndiyo maana vilabu vingi vinacheza kutokana na Pep Guardiola anavyotaka.

Arsenal wanaye kipa mwenye uwezo wa kupiga pasi, Chelsea pia, Tottenham Hotspur’s pamoja na Liverpool. Timu zote hizi zimeanza kuingia kwenye falsafa ya Johan Cruyff.

Falsafa ambayo imeanza kueneza dunia nzima kwa sasa, hata hapa nyumbani tunaye kipa ambaye anaendana na falsafa ya Johan Cruyff.

Ramadhani Kabwili anauwezo mkubwa wa kupiga pasi kwa ufasaha, anajiamini anapokuwa na mpira miguuni na kikubwa zaidi anatengeneza nafasi za kufunga.

Mfano kwenye mechi ya jana dhidi ya Biashara alifanikiwa kutengeneza nafasi moja pamoja na kupiga pasi 18.

Kiwango ambacho kikubwa kulinganisha na soka letu , lakini ni kitu ambacho kinaonesha kuwa Ramadhani Kabwili ni aina ya makipa wa kisasa ambao Johan Cruyff alikuwa anawaota awali.

Sambaza....