Blog

Kifo cha Jeba ni funzo kwa jamii ya ‘Watu wa mpira’

Sambaza....

Wakati mwingine Jamii inachangia sana kupotosha watu. Ibrahim Rajab “Jeba” alikuwa Mchezaji wa Azam FC akikuzwa pale Azam Academy.

Hakuna shaka juu ya kipaji kikubwa alichokuwa nacho uwanjani. Kutokana na kuwa na kipaji kilichojidhihirisha wazi, kama ilivyo desturi ya vilabu mbali mbali vya soka duniani vyenye vituo vya kukuza na kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana; Azam FC ilimpa mkataba rasmi wa kukitumikia kikosi cha kwanza kwa Msimu wa 2012/2013.

Katika hali ya kukikubali kipaji na uwezo wake wa kulisakata kabumbu; Klabu ya Simba ilitangaza kumsajili Jeba kama mchezaji huru, huku yeye pia Jeba akiwa tayari ameshalewa kwenda kucheza huko “Ndoto yangu katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ni kuvaa jezi za rangi nyeupe na nyekundu”. Likaibuka sakata kubwa kutokana na usajili huo, na Klabu ya Azam ikidai Jeba ni mchezaji wao halali na ina mkataba naye. Simba haikuwa tena na la kufanya na hivyo Jeba alirejea Azam FC.

Aliporejea Azam FC ndipo aligundulika kuwa na matatizo ya kiafya katika mfumo wa upumuaji. Azam walimshauri aachane na soka kwa Usalama wa Afya yake, na katika kuonesha umuhimu wa ushauri huo kwake Azam walimwacha Jeba.

Lakini wadau wa soka wakapumbazwa na kipaji chake murua na kuizodoa Azam FC kwa kumuacha Jeba. Walienda mbali na kusema kwamba Azam imeamua kumkomoa Jeba kwa ‘kumsingizia ugonjwa’ ili wapate sababu ya kumwacha.

Kwa bahati mbaya na Jeba mwenyewe hakukubaliana na ushauri wa madaktari wa Azam (pengine ni kutokana na ukweli kwamba mpira ndiyo ilikuwa ajira yake kuu). Akaamua kwenda kujiunga na Mtibwa Sugar ya Morogoro na hivyo kuwapa nguvu wale waliokuwa wakimuunga mkono na kubeza ushauri wa Azam.

Kama unaijua nguvu ya mashabiki wa Simba na Yanga hasa pale wanapomtetea mchezaji ambaye yupo Klabuni kwao ama anatarajiwa kuwa kwao utakubaliana na ukweli kwamba Azam hawakuweza kuwa na nguvu tena ya kuielezea jamii vyema juu ya kile walichomshauri Jeba zaidi ya kukaa kimya na kuiacha jamii iamini kwamba walimkomoa eti tu kwakuwa alikubali kusajiliwa Simba huku akiwa na mkataba na Azam.

Tangu hapo hajasikika tena kama Mchezaji mkubwa katika soka hadi inatoka taarifa hii ya umauti wake kuzikwa leo saa saba huko Zanzibar.
Jeba alikuwa alikuwa anaumwa, na leo (jana) mchana alizidiwa na akakimbizwa hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo alikutwa mauti jioni hii” Mattar Mohammed, Katibu wa Chuoni FC. Taarifa hii inaashiria kabisa Jeba alikuwa na viashiria vya kutokuwa timamu kimwili kwa ajili ya kazi aliyokuwa (Kucheza mpira) na hakuna siri kwamba alikiuka ushauri aliopewa na madaktari hapo awali. Marehemu hasemwi, lakini Jamii inawajibika katika hili kwa kupotosha ukweli.

Sisi wote ni wa Mola na kwake tutarejea.
Pumzika kwa amani fundi wa mpira Ibrahim Rajab “Jeba”.


Imeandaliwa na Raymond Mlowe, Shabiki wa Azam Fc na Arsenal FC


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.