Sambaza....

Dakika mbili za mwanzo zilitoa tumaini la Manchester City kupindua matokeo dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa barani ulaya.

Kadri muda ulivyokuwa unaenda tuliamini kuna sekunde itawadia kwa Manchester City kufunga goli jingine la pili, goli ambalo lingeongeza morali ya wachezaji ndani ya timu

Kipindi cha kwanza kiliisha, utulivu wa mabeki wa Liverpool ulisaidia magoli mengi kutokuwepo kwenye mchezo huu pamoja na kwamba Manchester City walikuwa wanaonekana wana nia ya dhati ya kufanya kitu kikubwa.

Nia ambayo ilikuwa inaonekana kuanzia kwenye paji la uso la kila mchezaji, kila mchezaji aliamini sekunde ijayo watafunga goli.

Miguu yao ilikuwa miepesi sana, ilikuwa inaukimbiza mpira kwa haraka kuelekea eneo ambalo Liverpool walikuwa wamekaa kwa utulivu.

Utulivu ambao ulihitajika kuharibiwa na mshambuliaji ambaye alikuwa na uzoefu mkubwa ambapo kipindi hicho alikuwa benchi.

Tulienda kipindi cha kwanza tukiamini kipindi cha pili ataingia mtu atakayevuruga utulivu uliokuwa eneo la nyuma.

Bahati mbaya kipindi cha pili kilianza na giza kwa Manchester City, mwanga wa kipara cha Pep pale mbele ya benchi la ufundi haukuwepo tena.

Wachezaji uwanjani walikuwa wanakosa mwanga wa kuwaongoza ni wapi wanatakiwa kwenda na kipi wanatakiwa kukifanya ili wafikie kwenye matamanio yao waliyokuwa nayo kipindi cha kwanza.

Hakuwepo mtu wa kuwakumbusha majukumu yao ipasavyo, hakuwepo mtu wa kufanya maamuzi ya haraka kimbinu ndani ya uwanja tena.

Mikel Arteta alikuwa mpweke, hakujua ni kipi anatakiwa kufanya kipindi kile, wakati anafikiria sana kipi cha kufanya Jurgen Klopp ndipo alikuwa anazidi kumpa maswali mengi ya kumuumiza kichwa

Mawasiliano kati yake na Pep Guardiola aliyekuwa amekaa jukwaani yalikuwa yanahitajika sana lakini maamuzi yake binafsi yalihitajika muda ule.

Kilikuwa kipindi ambacho angetakiwa kutumia muda mwingi kuwakumbusha thamani ya udongo wa Etihad

Nyasi za Etihad zilikuwa zinahitaji furaha kwa wakati ule, mashabiki walikuwa wanahitaji furaha majukwaani, jezi ya Manchester City ilikuwa inahitaji kukwepa aibu

Jukumu lilikuwa mikononi mwa Mikel Arteta, lakini alikuwa anashindwa kufanya kipi katika kipindi kipi ili timu isimame vizuri.

Ili timu itunze heshima yake, heshima ni kitu chenye thamani kubwa sana katika dunia hii ya mpira ndiyo maana tunaiheshimu Yanga kwa sababu ya jina lake kubwa pamoja na mafanikio makubwa ambayo waliwahi kuyapata ndani ya uwanja

Mafanikio ambayo yamejenga heshima kubwa klabuni hapo, ndiyo maana ni mara nyingi sana huwa wanahitaji mtu wa kuitunza heshima hii.

Mechi ya Yanga dhidi ya Singida United jana ilionesha kabisa Yanga inahitaji mtu kwenye benchi la ufundi

Mtu ambaye amekomaa kwenye ufundishaji , mtu ambaye ataiongoza timu hii iliyo kwenye presha ya kutetea ubingwa wake.

Kuna wakati Shadrack Nsajigwa alikuwa anaonekana kushindwa maamuzi ambayo yanalingana na muda husika wa mchezo.

Kocha Shadrack Nsajigwa ndiyo kwanza anaanza kukaa kwenye benchi la timu kubwa kama Yanga, anahitaji mtu wa kumuongoza

Mtu ambaye atamfundisha jinsi ya kuishi katika mazingira ambayo timu iko kwenye presha kubwa ya kupata matokeo. Muda huu bado hajafika huko

Naheshimu sana uwepo na uwezo wa Shadrack Nsajigwa kwenye benchi la Yanga na ninamuombea afike mbali lakini kwa sasa anahitaji kukaa zaidi na mtu atakayemuonesha njia ya kufika mbali

Bado hajafikia ukomavu wa kuibeba timu katika mazingira magumu kama haya, timu inahitaji kufanya vizuri katika mechi za kimataifa, mechi ambazo zinahitaji kocha mkomavu mwenye mbinu ambazo zitaisaidia timu kufika mbali.

Kama ilivyokuwa kwa Mikel Arteta kwenye mechi dhidi ya Liverpool, ndivyo itakavyokuwa kwa Shadrack Nsajigwa katika benchi la ufundi

Anahitaji kupatiwa kiongozi kipindi hiki, kiongozi ambaye atamfundisha mambo mengi, inawezekana uwepo wa George Lwandamina umemsaidia kwa kiasi kikubwa lakini bado haujamfikisha sehemu ambayo anaweza kudumu kwenye presha kubwa

Sambaza....