Ligi Kuu

Kiyombo geuka nyuma umwangalie Bahanuzi

Sambaza....

Hapana shaka umepata sifa nyingi, kila mtu anafurahia kutaja uwezo wako mahiri. Mwingine atasema unajua kutumia miguu yote miwili.

Huyu akaja na jambo lake la wewe kuwa na uwezo mkubwa wa kufunga magoli ya mbali kwa mashuti makali. Tena huyu atamalizia kwa kusema anafunga magoli ya kiume. Ili mradi tu anogeshe hadithi yake ya furaha juu yako.

Hapana shaka wengi wanasema hustahili kucheza MbaoFC. Na kukutabiria siku chache za kuwepo katika mitaa ya Ilemela. Watu tu wajuvi sana ya kuiona kesho ya mtu hasa hasa anapofanya vibaya au vizuri.

Wengi wetu hutazama kufanya vibaya sehemu fulani katika maisha matokeo yake ya kesho yatakuwa mabaya. Ni wachache wanaoamini kuwa afanyae vibaya leo, kesho anaweza akafanya vizuri. Ndiyo maana hata mtu anayefanya vizuri leo hii wengi wetu huiona kesho yake katika sehemu nzuri.

Huwa tunasahu misukosuko kama iliwahi kuletwa duniani. Akili yetu hutiwa upofu na uzuri wa kitu fulani kwa wakati ule na kushindwa kukumbuka kuwa kuna kushuka kwenye maisha.Siyo kila siku waweza kusimama pale pale ulipo kwenye maisha, kuna mabadiliko hutokea iwe hasi au chanya.

Bahanuzi

Na hii inategemea na wewe unaangalia mbele au unatazama mbele. Hapo ndipo utakuta wengi huachana , mwingine ataenda kulia na mwingine ataenda kushoto. Ndiyo maana kuna wachezaji wengi sana ambao waliwahi kutamba kwa muda mfupi na wakashindwa kuendelezea tambo zao.

Kelele za kuwasifia ziliwadidimiza na wakasahau ni kipi wanachotakiwa kufanya. Usishangae kuona mfungaji bora wa ƙligi kuu Tanzania bara msimu uliopita wa mwaka 2016/2017 leo hii hana hata goli tano.

Ni hii yote ilitokana na yeye kuchanganywa na zile kelele za kumshangalia.Kelele ambazo hutaki kuziamini na kuzipa nafasi kubwa zipite kwenye ngoma ya sikio lako. Maana hukuaminisha umefika , na kusahau kuwa una safari ndefu ya kufika kwenye mafanikio halisi.

Mafanikio ya Adidas/Nike kugombania mguu wako ili wauvishe kiatu bora. Mafanikio ya kulipwa kwa wiki pesa ndefu ambayo kwa hapa Tanzania waweza kutumia miaka mingi kuipata. Mafanikio ya kucheza ligi ambazo huziangalia kwenye Televisheni, ligi ambazo zinawachezaji unaowahusudu.

Habib Kiyombo

Wengi wa wachezaji hawakuwahi kufikia mafanikio hayo kwa sababu waliruhusu sifa ziwapeleke kushoto na kuipoteza njia ya kwenda mbele. Kwao ikawa kila walipokuwa wanageuka na kutazama ndiko mbele yao ilipo. Ikawafanya wakose uelekeo sahihi wa kwenda kwa sababu ya kelele za majukwaani. Sasa hivi wanakuambia uende Kariakoo, Ilemela hapakufai tena. Ukifika Kariakoo watakufanya uamini kuwa uko katika mji wa Catalunya.

Huna haja ya kwenda popote pale kwa sababu utakuwepo kwenye mji bora kisoka kuliko miji yote. Akili yako wataifumba kwa kukuletea wale wasichana wanaotumia dawa za kina Jack Ma kukuza makalio ili mradi uone tofauti ya Ilemela na Kariakoo. Na zile Ofa za bia zitakufanya ulale usiku wa manane na kukusahaurisha kilichokufanya uende Kariakoo. Wengi wakifika Kariakoo huwa wanaona ndiyo wamefika mwisho wa safari yao ya maisha ya kisoka. Hakuna anayetumia Kariakoo kama daraja la kwenda Catalunya.

Ndiyo maana huridhika, hata mazoezi hupungua, kujituma uwanjani huondoka na akili ya mpira hufifia kabisa. Ndoto zile za kucheza Ulaya hupotea ghafla. Hakuna anayewaza kuwa na wasimamizi wao binafsi ambao watawaongoza kukilea na kukikuza kipaji chao.

Hata suala la kuwa na wakala nalo hupotea kwa sababu wengi wao hawaoni haja ya kusogea hatua moja mbele kutoka pale waliposimamia. Umri utazidi kwenda, nguvu za mpira huisha mwilini mwao na uwezo wa kucheza mpira hupungua. Na mwisho wa siku watatupwa kama kopo la chooni na vilabu vya kariakoo bila msaada wowote.

Sisi tutabaki na historia tu ambayo tutatumia kuvielezea vizazi kuwa alikuwepo fulani aliyeng’aa msimu fulani, akaenda timu fulani kwa sababu ya sifa kumlevya kwa sasa hana hata timu fulani.

Kama ambavyo ilivyohadithi ya Bahanuzi na michuano ya Kagame ilivyobadiLisha maisha yake, kutoka mchezaji mwenye njaa kuwa mchezaji aliyeridhika ghafla, ndivyo hivo hofu yangu ilipo kwa Habib Kiyombo.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x