Sambaza....

Klabu ya soka ya Kinondoni Municipal Council ya Dar es Salaam imemtangaza kocha wa zamani wa Mbao FC Etienne Ndayiragije kuwa kocha mkuu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu soka Tanzania Bara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamin Sitta amesema wameamua kufanya maamuzi hayo baada ya kujiridhisha kiwango cha kocha huyo hasa katika kukuza kosa la vijana kama alivyojipambanunua alipokuwa katika klabu ya Mbao.

“Sisi kama serikali ni wajibu wetu kuhakikisha tunamfikia mtoto ambaye ana kipaji, kwa maono hayo ambayo tumeyaona kwa kocha huyu kwa rekodi tuliyoiona kwa wachezaji wengi aliowalea kwenda kucheza timu kubwa ambazo zipo kwenye ligi, tumeridhika na kiwango chake na ndio maana tumeamua kumpa nafasi hiyo,” Sitta amesema.

Kwa upande wake kocha Ettiene Ndayiragije ameushukuru uongozi wa timu kwa kumuamini na kumpa kibarua hicho na ameomba mshikamano kutoka kwa wanakinondoni ili kuweza kuisaidia KMC kuweza kufanya vizuri msimu ujao.

“Natoa shukrani kwa uongozi kwa kutuamini katika kazi hii, kama inavyojulikana ni timu ya uma na kila mtu anamchango wake, mimi binafsi siwezi kufikisha KMC mahali inapotaka kufika ila tukishikamana na mchango wenu naamini tutafika,” Ndayiragije amesema.

Kocha huyo aliondoka Mbao FC zikiwa zimesalia mechi saba kumalizika kwa ligi baada ya kupata pressure kubwa kutoka kwa mashabiki ambao walikuwa wanataka matokeo makubwa.

Anajiunga na KMC ikiwa ni kwa mara nyingine tena anajiunga na timu ambayo imepanda daraja kwani alifanya hivyo mwaka 2016 akiwa na Mbao iliyokuwa imepanda daraja na kuisaidia timu hiyo kubaki kwenye ligi, kuingia fainali ya kombe la Shirikisho lakini pia kuwa katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya kocha bora kwa msimu wa 2016/2017.

Sambaza....