Ligi Kuu

Kuvaa koti zuri juu ya shati chakavu hakutoisaidia Yanga.

Sambaza....

Hakuna kitendawili tena kwenye maisha ya Yanga, kwao wao maisha yao siyo fumbo tena kama tafasri halisi ya maisha ilivyo.

Wanaishi kwenye maisha yaliyowazi, maisha ambayo yanawafanya wasiwepo katika dunia ya tambo na furaha.

Wameshachagua dunia hii isiyopendwa na wengi, dunia ya huzuni na majonzi, dunia ya masimango na kubezwa sana.

Dunia isiyo toa nafasi kwao kutembea kifua mbele kuwa wana timu imara yenye ushindani mkubwa kuzidi timu yoyoye ile kama misimu mitatu iliyopita.

Kwao wao nyimbo za mdundiko siyo rafiki tena, wanachokifanya ni kutazama jua kama linaweza kurudi nyuma mpaka kipindi ambacho walikuwa na uwezo wa kushona suti yenye bendera ya Yanga.

Utamwambia nini shabiki wa Yanga wakati timu yake ilikuwa inasajili wachezaji bora ambao walikuwa na uwezo mkubwa wa kuifanya Yanga ionekana tishio?

Mshale wa sekunde una nguvu kubwa sana wa kusukuma mshale wa dakika na wa saa ili kuikaribisha siku mpya, siku mpya inapofika huja na viatu vya furaha na viatu vya huzuni na kila mmoja huwa hupewa kiatu chake kulingana na zamu yake kwa siku husika.

Leo ni zamu ya Yanga kukivaa kiatu cha huzuni , Yanga wanalia baada ya jana kucheka, kicheko chao cha jana kilitokana na uimara wa mtu mmoja.

Leo hii mtu imara hayupo tena katika timu ya Yanga na imebaki Yanga dhaifu, Yanga isiyo kuwa na uwezo wa kulipa mishahara ya wachezaji, Yanga isiyokuwa na uwezo wa kusajili tena wachezaji nyota ndani ya kikosi chake.

Yanga isiyokuwa na uwezo wa kutoa motisha kwa wachezaji wake ili wapigane, Yanga inaongozwa kwa kusukumwa na pumzi ya mdomoni bila kujali uzito wa Yanga, ndiyo maana inaenda kwa kuchechemea.

Hawana uhakika wa rangi ya kesho kwa sababu jana walitumia nguvu kubwa kumtengeneza mtu imara na kusahau kutengeneza taasisi imara. Hawakujua taasisi imara hudumu kwa muda mrefu kuliko mtu imara.

Hii yote ni kwa sababu wanaopewa dhamana ya kuongoza hupenda vitu vyepesi kwa sababu ya kukosa maono.

Hawatamani kuweka alama itakayodumu vizazi na vizazi, alama ambazo zitatumika kama kijiko cha kuilisha chakula Yanga kwa muda mrefu.

Hawaoni aibu kuongea mbele ya vyombo vya habari kwa kulalamika kuwa TFF inawafanyia fitina kwenye mapato ya mlangoni na kuna wakati mwingine hufikia hatua ya kulalamika wingi wa makato kwenye mapato ya mlangoni.

Wangekuwa na uwanja wao binafsi kuna baadhi ya makato yangepungua na kuingia moja kwa moja kwao.

Mazingira haya hayakuandaliwa toka awali kwa sababu waliowahi kubahatika kupewa nafasi ya kuiongoza Yanga walipenda vitu vyepesi kutokana na kukosa maono.

Maono ambayo yangewawezesha kujenga vyumba vya biashara pembezoni mwa uwanja wao, maono ambayo yangewawezesha kujenga kituo cha kuibua, kulea na kukuza vipaji vitakavyopandishwa kwenye timu kubwa na kuepukana na gharama ya kusajili wachezaji wengi kwa gharama kubwa.

Hawakuwaza hata jinsi ya kutengeneza mazingira mazuri ya kuingiza pesa kupitia nembo ya klabu yao ya Yanga. Nembo ambayo ina nguvu kubwa kutokana na wingi wa mashabiki wa Yanga nchini.

Nani aliwahi kufikiria namna bora ya kuingiza pesa kutokana na wingi wa mashabiki wa Yanga waliokunywa maji ya bendera ya Yanga?.

Kiongozi yupi alifikiria kuiongoza Yanga katika mazingira ya kibiashara?, mazingira ambayo yatamruhusu mwekezaji/mfanyabiashara yoyote aje awekeze kwao ili kupunguza gharama za uendeshaji?

Ni aibu kwa Yanga kuomba kukopeshwa pesa na TFF kwa ajili ya kwenda Algeria kwenye mchezo wa kombe LA shirikisho wakati dunia ya leo ina mashirika mengi ya ndege.

Viongozi walishindwa kuongea na shirika moja la ndege kwa ajili ya kufanya biashara yenye manufaa pande zote mbili?, kuna shirika gani la ndege lingekataa kuwapa ofa ya nusu bei ya tiketi kwa kila mchezaji aliyekuwa anaenda Algeria ili shirika hilo la ndege litangazwe na Yanga kwa kipindi maalumu ?

Kuna wakati mwingine unaweza ukapata usingizi wa uchovu kipindi unaposikia Yanga wanahangaika kupata GYM ya kupiga mazoezi wakati kuna GYM nyingi ambazo zinaweza kuwa mmoja wa wadhamini wa Yanga?.

Na cha kushangaza bado Yanga wanamlilia Manji!, bado wanatamani mtu imara , hawataki kuwaza kutengeneza taasisi imara, hakuna walichojifunza kupitia haya mapito yao, wao wanaamini njia bora ni kumrejesha Manji kwenye timu.

Manji akirudi atakaa miaka minne baada ya hapo ataondoka na kuiacha Yanga iendelee na maisha yake halisi, maisha ya kuhangaika bila msaada kwa sababu hawataki kujenga mazingira ya kujitegemea.

Kumrejesha Manji ni sawa na kuvaa koti zuri la gharama kubwa , linalovutia kutokana na ufundi uliotumika kushona koti hilo wakati ndani yake umevaa shati chafu, lilichokaa na kuchanika mgongoni.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x