Ligi Kuu

Kwaheri African Lyon ligi kuu Bara.

Sambaza kwa marafiki....

Klabu ya soka ya African Lyon ya jijini Dar es Salaam itakuwa timu ya kwanza kushuka daraja msimu huu kwenye michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara, kama itapoteza mchezo wake unaofuata dhidi ya Mbeya City.

African Lyon ambayo inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa timu 20 ikiwa na alama 22, italazimika kushinda michezo yote mitano iliyosalia ili angalau kujiweka katika mazingira ya kupambana kucheza Play Off huku ikiwaombea Ruvu Shooting na Biashara United kutoshinda mchezo wowote jambo kimsingi ni ngumu sana kutokea.

Lyon ambao walipanda daraja msimu huu hawakuwa na matokeo mazuri toka kuanza kwa ligi licha ya kuwa na wachezaji nguli na mahiri kama Haruna Moshi Boban, mshambuliaji kutoka Ufaransa Victor Da Coast pamoja na kocha wa kigeni pia Soccoia Lionel.

Mpaka sasa wakiwa wameshinda michezo minne pekee yake na kutoka sare michezo kumi na wakipoteza michezo 19, hata kama wakishinda michezo yote mitano iliyosalia watakuwa wanafikisha alama 37 alama ambazo tayari Mbao FC waliopo nafasi ya 17 wamezikusanya, jambo ambalo haliwezi kuwaondoa kwenye mstari wa kutoshuka daraja.

Ikumbukwe msimu huu timu mbili zitakazoshika nafasi ya 19 na 20 zitashuka moja kwa moja wakati timu zitakazoshika nafasi ya 18 na 17 zitacheza playoff kujinusuru kushuka daraja na timu mbili kutoka daraja la kwanza ambazo zitakuwa zikipambana kupanda daraja.

Lyon wamebakisha kucheza na Mbeya City mwanzoni mwa mwezi wa tano, kabla ya kuwakaribisha Mbao FC na Ndanda, baadae watasafiri kucheza na Mwadui mkoani Shinyanga na watamalizia nyumbani kwa kucheza na KMC.

Wanakandanda wanasema lolote linaweza kutokea kwenye soka, lakini hili la African Lyon kusalia ligi kuu sidhani kama linaweza kutokea, labda kama si sayari dunia! kwa sasa la kujiuliza nani kuungana na African Lyon?!

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.