Ligi Kuu

Mahadhi wakumbuke Mazembe ujifunge masombo

Sambaza....

Najua ushapitia nyakati tofauti zenye majira tofauti sana katika maisha yako, na kuna wakati mambo yako yalienda shoto na yakarudi upogo kwa sababu mbalimbali na kuna nyakati mambo yako yalitembea kwenye mstaari mnyoofu.

Nyakati hizi zilikuwa na maana kubwa sana kwenye maisha yako kwa sababu maisha ya mwanadamu hukamilika kipindi ulimi wake unapoonja pilipili na asali.

Maisha hayawezi kuitwa maisha kama yatakuwa na upande mmoja wa shilingi, ndiyo maana tunatakiwa tuwe dhabiti pindi kombo anapotutembelea sebuleni kwetu.

Kuna wakati miguu yako ilikuwa mizito kwa kila hatua uliyokuwa unajaribu kupiga ili usogee kwenda mbele.

Mbele yako hukuona mwangaza wowote, giza lilikuwa linatawala mboni zako za macho kiasi kilichopelekea wewe kutoiona njia sahihi uliyotakiwa kuifuata ili kufika ulipokuwa unatamani kupafikia kabla hujakanyaga jiji la Dar es Salaam.

Jiji ambalo hutia upofu wa akili kipindi unapotanguliza kichwa kukanyaga ardhi yake na kuipa miguu jukumu la kuona na kufikiria kwa sababu tu inauwezo wa kupiga hatua.

Jiji ambalo lilikufanya usahau uliyokuwa unayaota kipindi ambacho upo Coastal Union.

Kipindi ambacho ulikuwa unafanya mazoezi kwa jitihada kubwa ili ufanikiwe kufika kariakoo ukiamini ndiyo njia sahihi kwenda alipofanikiwa kwenda Nonda Shabani.

Hapana shaka habari zake zilikuwa zinakupa matamanio ya kufikia hatua kubwa ya mafaniko, ukaongeza jitihada za mazoezi kila uchwao.

Jitihada ambazo zilizaa matunda ya wewe kufika Kariakoo, sehemu ambayo ina mengi mapya ya kuvutia machoni mwa mgeni yoyote.

Mapya ambayo huyumbisha kwa kiasi kikubwa malengo ambayo awali mgeni yoyote huwa anayapanga kabla hajafika Kariakoo, na kusahau kabisa umuhimu wa kufanya kilichokupeleka.

Ndiyo maana ulipunguza juhudi za kufanya mazoezi mara baada ya kukanyaga ardhi ya Kariakoo, na ukawezeka bidii zako sehemu nyingine tofauti na ile iliyokupeleka Kariakoo

Bidii za kubadilisha muonekano wa mwili zikazidi bidii za kufanya mazoezi kwa juhudi na kusikiliza walimu wa mpira, masikio yako yakawa yanatamani kumsikiliza mwalimu wa mitindo ili akupe mbinu za uanamitindo zilizokufanya bidii zako uziwekeze huku.

Ukafanikiwa kuwa na muonekano uliowavuta warembo wa kariakoo ambao walikutia upofu na mapenzi yao mazito.

Akili yako ikawa inawaza zaidi nani ana penzi tamu kati ya Mwajuma na Asha na kusahau kabisa kujiuliza nani atakuangalia uwanjani ili akupeleke alipofanikiwa kwenda Nonda Shabani

Akili yako ikajaa ukungu, na ukawa unaona kucheza mechi na Asha kuna umuhimu mkubwa kuliko kwenda kucheza timu moja na Lukaku.

Ukamuonesha ushirikiano Asha, hukutosheka ukamuongeza Mwajuma ambaye alikufunza kutumia vileo ambavyo vilikuondoa kwenye mstari uliokuwepo awali.

Mstari ambao ulikuwa unaonesha uko kwenye daraja la kuwa mchezaji bora baadaye kutokana na kipaji chako.

Kipaji ambacho kilikuwa madhubuti na murua, kipaji ambacho kiliwaacha hoi TP Mazembe walipokuja kucheza na Yanga kwenye uwanja wa Taifa

Mahadh akifanya yake katika mechi dhidi ya TP Mazembe

Mechi ambayo ilionesha njaa uliyokuwa nayo kipindi hicho, mechi ambayo ilionesha dhahiri una lengo la kufika mbali.

Ulikuwa mmoja wa wachezaji waliocheza katika kiwango ƙkikubwa sana, kiwango ambacho kama ungetulia na kukiendeleza leo hii ungekuwa mtu unayemfuata Simon Msuva.

Nakumbuka mpaka nywele zako ulivyokuwa umeziweka siku ile, nakumbuka mpaka rangi ya viatu ulivyotumia siku ile hii ni kwa sababu ulikuwa nyota wa mchezo ule.

Lakini kwa sasa nyota yako ishafifia kwa kiasi ƙkikubwa, hakuna jitihada kubwa unayoionesha kufikia malengo yako makubwa uliyokuwa unayahubiri kipindi ulipokuwa unahojiwa na vyombo vya habari.

Kuna wakati inauma sana unapoona kipaji kama chako kikikosa mwelekeo sahihi, kipaji ambacho unaamini kingeweza kuwa na faida kubwa kwa taifa kama kingepata msimamizi sahihi wa hicho kipaji.

Hapo ndipo huwa tunajikwaa mara kwa mara bila kuchukua tahadhari yoyote, vipaji vingi havina wasimamizi wazuri ndiyo maana ni rahisi kupeperushwa hata kwa upepo wa mluzi.

Inawezekana ni eneo ambalo haliangaliwi kwa jicho pana, lakini ni eneo muhimu katika makuzi ya kipaji cha mchezaji.

Juma Mahadhi alikosa mtu mzuri wa kukisimamia kipaji chake ndiyo maana akaenda njia tofaufi na njia yake ya awali, natamani awe anaiangalia mara kwa mara mechi aliyocheza dhidi ya TP Mazembe natumaini itamsaidia kurudi kwenye njia yake sahihi, hajachelewa bado ana muda wa kukaa na kujirekebisha.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x