Kocha wa Simba Sc, Aussems
Ligi Kuu

Makocha watano wanaostahili kuifundisha Simba

Sambaza....

Rasmi Simba wameachana na aliyewahi kuwa kocha wao mkuu Patrick Aussems kwa sababu kuu mbili, sababu ya kwanza Patrick Aussems hakuweza kufikia makubaliano ambayo waliwekeana na Simba , Simba na Patrick Aussems walikubaliana msimu huu timu ifike hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika lakini hakufikia lengo hili, sababu ya pili ni ya utovu wa nidhamu ambapo Patrick Aussems aliondoka kwenye kituo cha kazi bila taarifa. Patrick Aussems ashaondoka, nani anastahili kuja Simba ?

KIM POULSEN

Kitu kimoja cha kipekee ambacho kimesababisha nianze na jina la Kim Poulsen ni soka la maendeleo, na soka la maendeleo msingi wake ni soka la vijana. Simba inapigana kuingia kwenye uendeshwaji wa mpira wa kisasa, wanajenga uwanja, hostel na miundombinu ya kisasa ya mpira wa miguu.

Miundombinu hii siyo kitu kama hakuna kocha ambaye atakuja na ramani ya kupata timu bora kuanzia kwenye soka la vijana mpaka timu kubwa. Kim Poulsen amekuwa muumini mzuri wa dini ya soka la vijana kwenye maisha yake ya soka. Kumpata Kim Poulsen watakuwa wanapiga ndege kwa jiwe moja (ndege wa soka la vijana na ndege wa timu kubwa).

DYLAN KERR

Moja ya makocha ambao waliondoka Simba bila kujua kwanini aliondoka ni Dylan Kerr, kocha ambaye anauwezo mkubwa sana . Na uwezo wake umekuwa ukijidhihirisha kila Siku, baada ya kuachana na Simba alipata nafasi ya .

 

Aliipa mafanikio kwa kuipeleka timu katika hatua ya makundi barani ya michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, Simba wanataka kocha ambaye atawasaidia kwenye michuano ya kimataifa, Dylan Kerr anauwezo huo.

MICHO

Moja ya makocha bora sana kwenye bara la Afrika. Analijua vyema soka la bara la Afrika. Huyu ndiye alikuwa mzizi wa mafanikio ya timu ya taifa ya Uganda, timu ambayo ilikuwa na vipaji lukuki. Kipindi chake aliweza kukusanya vipaji vingi kutoka Uganda na kuunda timu tatu za taifa zenye wachezaji wenye vipaji haswa.

Hali hii iliifanya Uganda kuwa tishio kwa vigogo kama Misri na Ghana. Uganda walifanikiwa kufuzu kwenye michuano ya Afcon chini ya Micho, hata alipoondoka Micho , Uganda iliendelea kubaki imara kwa sababu ya misingi ambayo aliiweka. Amefanikiwa kufundisha ligi ya Afrika Kusini tena timu kubwa ya Kaizer Chiefs, ndiye kocha mkuu wa Zamaleki kwa sasa ambaye kibarua chake kiko mashakani. Kwa uzoefu huu inatosha kwake yeye kuwa kocha wa Simba.

PIERRE LENCHANTRE

Alikuja Simba na akakaa kwa muda wa miezi sita tu. Miezi ambayo ilikuwa na mwangaza mkubwa Kwani alituonesha namna alivyokocha bora. Pamoja na kwamba hakuwa na muda mrefu kabla ya kukutana na Al Masry katika ligi ya kombe la shirikisho barani Afrika lakini alionesha uwezo mkubwa sana.

Alitoka sare ya 2-2 hapa nyumbani lakini alipoenda Misri alitoka suluhu ya bila kufungana huku Simba ikicheza katika kiwango kikubwa sana. Huyu ni mshindi wa medali ya Afcon akiwa na Cameroon mwaka 2000 alichukua ubingwa wa Afcon. Analijua vyema soka la Afrika na anaweza kuwa msaada kwenye ndoto Yao ya kufanya vyema hapa Afrika.

FLORENT IBENGE

Najua mtashangaa, mtajiuliza Simba wanaweza kumtoa pale As Vita ? Simba kama wanataka kupambana na TP Mazembe lazima waanzie kwenye kupambana kupata makocha bora na wachezaji bora.

Florent Ibenge bingwa wa kombe la shirikisho barani Afrika akiwa na As Vita. Ni kocha ambaye atayari anayajua mashindano ya Afrika , mashindano ambayo Simba wanayataka. Na kwa bahati nzuri yeye ni mshindi kwenye mashindano haya , kuja kwake Simba kunauwezo wa kuifanya Simba ifanye vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x