Sambaza....

Msemaji wa klabu ya soka ya Mbao ‘Wabishi’ Clisant Malinzi ameutaja mchezo wa Jumamosi hii wa ligi kuu soka Tanzania Bara baina yao na Alliance FC kama dabi ya pili kwa ukubwa Tanzania Bara ukitoa mchezo wa Simba na Yanga.

Malinzi amesema kwa kuwa Mwanza ni jiji la pili kwa ukubwa ukitoa Dar es Salaam basi hilo linatosha kabisa kuifanya mechi hiyo kuwa kubwa Tanzania Bara na hivyo amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo.

“Mechi ya Jumamosi hii sio ya kukosa kwa Mashabiki, kwa sababu naweza kuiita kama Dabi ya pili kwa ukubwa Tanzania, kwa sababu ukiacha Dar es Salaam ndio mji Mkubwa unaofuata ni Mwanza, hivyo nafikiri baada ya mechi ya Simba na Yanga, inayoifuata ni mechi hii ya Mbao na Alliance, kwa hiyo mashabiki wasiache kuja kuiona ni mechi ya kufungulia Mwaka,” Malinzi amesema.

Akizungumzia kuhusu maandalizi ya mchezo huo Malinzi amesema kila kitu kipo sawa, ila watamkosa kiungo Hussein Kasanga ambaye bado anamajeraha lakini wachezaji wote kwasasa wapo katika hali nzuri na wana morali ya kutosha kuelekea kwenye mchezo huo utakaopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

“Kwa taarifa kutoka kwa Daktari, kuna mchezaji wetu ambaye ana majeraha takribani mwezi mzima sasa hivi Hussein Kasanga, tunaweza kumkosa kwa mchezo wa Jumamosi, lakini kwa wengine wote waliobaki wapo katika afya njema hata waliosafiri kwenda Dar es Salaam na kupitiliza kwenda Bukoba wote wamerudi na wana Afya njema,” amesema.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Mbao FC walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Alliance na hivyo kuufanya mchezo ujao kama wa kulipiza kisasi kutokana na matokeo ya hivi karibuni ambazo timu hizo zimekuwa zikiyapata.

Kwa michezo miwili iliyopita ya ligi, Mbao FC wametoka sare yote na kufikisha alama 26 ili hali Alliance wao wameshinda mmoja na kutoka sare mmoja na kuwafanya kufikisha alama 20 kwenye msimamo wa ligi.

Sambaza....