Blog

Mguu wa Sharaf Shiboub unafaa kuchezea Yanga

Sambaza....

Tuanzie hapa,  msimu uliopita Yanga walikuwa na kiungo ambaye alikuwa akitengeneza magoli na kufunga magoli akitokea katikati ya uwanja. Kiungo ambaye alifanikiwa kufikisha pasi 20 za mwisho za magoli huku akiwa amefunga magoli 7.

Kwa kifupi alihusika kwenye magoli 27 ya Yanga msimu uliopita. Lakini kwa msimu huu hayupo tena kwenye jezi ya Yanga, yuko kwenye jezi ya Simba na kwa bahati mbaya ana kaa sana kwenye benchi kuliko kucheza uwanjani. Huyu ni Ibrahim Ajib “Migomba”.

Ibrahim Ajib Migomba.

Binadamu ambaye kwa msimu jana aliitwa ana miguu ya dhahabu akiwa kwenye jezi ya Yanga , lakini leo hii mguu wake wa dhahabu hauonekani akiwa kwenye jezi ya Simba . Jezi ambayo imemfunika pia Sharaf Ali Shiboub , kiungo hodari na mahiri kutoka Sudan.

Kwa bahati mbaya sana hawa wote wawili yani Ibrahim Ajib pamoja na Sharif Ali Shiboub hawana nafasi kubwa sana kwenye kikosi cha Simba kwa sasa. Benchi limekuwa na urafiki nao kuliko nyasi za uwanjani.

Wote wawili wanauwezo wa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga magoli pamoja na wao kufunga wakitokea katikati ya uwanja. Kwa kifupi unaweza ukasema Simba wameweka kwenye benchi magoli pamoja na pasi za mwisho za magoli.

Sharaf Eldin Shiboub.

Wakati Simba wakiwa wameweka kwenye benchi magoli pamoja na pasi za mwisho za magoli , watani wao Yanga hawana kiungo wa kati ambaye anaweza kufunga magoli kwa wingi akitokea katikati ya uwanja , pia hawana kiungo wa kati ambaye ana uwezo wa kutoa pasi nyingi za magoli.

Mapinduzi Balama , Haruna Ninyonzima na Papy Kabamba Tshishimbi ambao mara nyingi hucheza katikati eneo la kiungo cha juu , uwezo wao wa kufunga na kutoa pasi nyingi za magoli pamoja na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga siyo mkubwa sana ukilinganisha na Ibrahim Ajib pamoja na Sharif Ali Shiboub.

Inawezekana kwa sasa Yanga ikawa ngumu kumchukua Ibrahim Ajib , lakini wanaweza kufikiria namna ya kumchukua Sharif Ali Shiboub ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa akitengeneza nafasi ya kufunga magoli akitokea katikati mwa uwanja.

Sharaf Eldin Shiboub akiwa dimbani.

Kwa sasa Yanga wamekuwa wakihangaika sana kufunga magoli kwa sababu hawana mchezaji anayefunga sana akitokea pembeni , hawana mshambuliaji anayefunga sana los hawana kiungo wa kati ambaye anafunga na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.

Kwa kuanza kutatua tatizo hilo ni vizuri kwa Yanga kufikiria namna sahihi ya kumsajili Sharif Ali Shiboub ambaye anaonekana amekosa namba kwenye kikosi cha Simba . Sharif Ali Shiboub ana uwezo wa kuhakikisha anaziba udhaifu wa Yanga katikati eneo la kati mwa uwanja.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.