Ligi Kuu

Mtazamo wangu Ligi Kuu- VPL.

Sambaza....

Kulikuwa na dalili za Mbaraka Yusufu mshambuliaji wa Kagera Sugar kuibuka mchezaji bora wa ligi kuu msimu huu wa 2016-17 lakini kadi nyekundu mechi ya juzi na Yanga SC inamtoa katika kinyang’anyiro hicho . Suala la nidhamu huenda likachafua mbio hizo.

Namuona Haruna Niyonzima kurudi kwenye tuzo za mchezaji bora wa kigeni mwaka huu kama alivyonyakua tuzo hiyo mwaka 2013. Amekuwa katika kiwango kizuri na msaada mkubwa kwa timu yake huenda akaleta upinzani kwa Kamusoko anaeshikilia tuzo hiyo. Lakini pia Obrey Chirwa na kipa wa African Lyon Youthe Rostand wanaweza kuwa katika kinyang’anyiro hicho.

Njia ni nyeupe kwa Saimoni Msuva kuibuka mfungaji bora wa ligi kuu mwaka huu . Magoli 13 kileleni ni mtaji tosha kufanya hivyo endapo A. Mussa wa Ruvu shooting mwenye goli 12 asipokaza buti kumfikia.

Licha ya wengi kuzipa nafasi Toto Africa na Majimaji FC kuungana na JKT Ruvu kushuka daraja lakini kuna timu inaweza kushuka daraja na watu wote kubaki vinywa wazi. Kuanzia Mbeya City nafasi ya 8 katika ligi kuu mpaka alipo Ndanda FC timu hizo zote hazijavuka mstari wa kifo wa alama 35 ambazo Toto na Majimaji wanaweza kuzifikisha wakishinda michezo yao miwili. Hivyo Mbeya City , Prisons, Ndanda , A. Lyon na Ruvu Shooting zote zipo kikaangoni.

Tunzo ya kipa bora wa ligi kuu ni mtihani mkali mwaka huu . Aishi Manula , Youthe Rostand , Deogratius Munishi , Daniel Agyei na licha ya kupata mechi chache Beno Kakolanya anaweza kuingia katika mizani hiyo kutokana na kipaji chake kushitua wengi.

La kuvutia sana katika ligi yetu ni mchuano wa ubingwa kati ya wakongwe Simba SC na Yanga SC . Wamefungana vilivyo kwa hesabu ya namba ;

YANGA SC ; amecheza mechi 27 ameshinda mechi 19 , sare 5 na kufungwa mechi 3. Ana alama 62 kileleni mwa ligi kuu akiwa na GS ya 54 na GD ya 42.

SIMBA SC : amecheza mechi 28 akishinda mechi 19 , sare 5 na kufungwa mechi 4 . Anashikiria nafasi ya 2 katika ligi kwa alama 62 kinachomtofautisha na Yanga ni GS ya 46 na GD ya 31 huku akibakiwa na michezo 2 mkononi na Yanga michezo 3.

Ligi imekuwa na ushindani mkubwa msimu huu na kuna wachezaji wameonesha uwezo mkubwa toka mwanzo wa msimu na kudumu vyema katika ubora wao . Beki wa kushoto wa Simba SC Mohamedi Hussein ‘ Zimbwe jr ‘ anashikiria rekodi ya kucheza mechi zote ndani ya Simba SC na huenda akawa ndio mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi ligi kuu mpaka sasa.

Beki wa kushoto wa Azam FC Gadiel Michael amekuwa gumzo kwa uwezo mzuri wa kuicheza nafasi hiyo.

Kenny Ally Mwambungu kiungo wa Mbeya City nae ametaradadi vilivyo msimu huu. Anaingia katika orodha ya viungo bora watano wa ligi kuu msimu huu ; Himidi Mao , Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Jonasi Mkude na Kenny Ally . Ubora huu ndio unawafanya wababe wa ligi hiyo Yanga SC kuhaha kuisaka saini yake pia akihusishwa kutua Singida United msimu ujao lakini waajiri wake wa sasa MCC wakijinadi kumbakisha hapo.

Dirisha dogo la usajili lilituletea changamoto mpya ligi kwa kuona vipaji vingine vipya vyenye ubora mzuri . Zahoro Pazi mshambuliaji wa Mbeya City amekuwa gumzo kwa uwezo wa kufumania nyavu na aina ya uchezaji wake . Daniel Agyei golikipa wa wekundu wa Msimbazi akitokea timu ya Medeama SC nchini Ghana kurithi mikoba ya Angban aliyetimuliwa , amekuwa bora kwa timu hiyo na kuonesha uwezo mzuri kulinda langa lao.

Sambaza....