Blog

Nani chaguo sahihi kiufundi: Tshabalala/ Gadiel?. Sehemu ya 1.

Sambaza kwa marafiki....

Karibu katika sehemu ya kwanza ya makala hii ya Nani Chaguo sahihi Kiufundi kati ya mabeki bora zaidi kwa sasa kwa upande wa kushoto, Gadiel Michael na Mohamedi Husseni, Zimbwe Jr.

Mchezo wa mpira una ladha yake, ladha hunoga pale wachezaji wanapoonyosha uwezo wao wote katika mechi mbalimbali na hata ndani ya kikosi kimoja katika harakati za kugombania namba.

Kutoka, Friends Ranger ya Magomeni kule mkoani Kagera namleta kwenu Mohamedi Husseni Mohamedi, aka, Tshabalala au Zimbwe Jr.

Tshabalala alizaliwaJanuari 11 mwaka 1995, kwa sasa ana miaka 24. Kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Market, Shabalala ana thamani ya Euro elfu 75 ikiwa ni zaidi ya shilingi milioni 191 za kitanzania.

Maisha ya soka ya fundi huyu yalianzia katika timu ya nyumbani kwao Kagera inayoitwa Friends Rangers, kisha alichezea timu nya mkoa wa Kinondoni ya Cocacola, na kisha kuchaguliwa timu ya vijana ya Serengeti Boys, kisha watu wa Azam walimuona na kutaka kufanya nae dili.

Baada ya kujiunga na Azam,Tshabalala alianzia kwenye Academy kabla ya kupandishwa timu kubwa na kushushwa tena baada ya ujio wa benchi jipya la ufundi.

Ndani ya Azam alidumu kwa takribani misimu mitatu, kabla ya ujio wa  Stewart Hall, aliyechukua mikoba ya kipenzi cha Tshabalala Mbrazil Itamar Amorim.

 Stewart alimshusha tena na kumrudisha katika timu Academy.  Huo ndio ulikuwa mkono wa kwaheri kwa Tshabalala, na hapo ndipo alipojiunga na Kagera Sugar msimu wa 2013/14.

Huko alikutana Na King Kibadeni Mputa, kisha Jackson Mayanja, huku majeraha yakimuandama na kumfanya kukaa nje ya uwanja kwa nusu msimu, kabla ya kupata nafasi katika raundi ya pili. Kiwango alichokionyesha baada ya kupewa nafasi, kiliwavutia mabosi wa Simba na msimu wa 2014/15, alijiunga na Simba hadi sasa ninavyoongea bado ni mwekundu.

Baada ya kutua tu mitaa ya Msimbazi alikutana na wachezaji wenye majina makubwa kama Issa Rashid Baba Ubaya ambaye pia kipindi hicho alikuwa ni beki tegemeo wa U20, Huku Zimbwe akiwa tegemea U17, pia msimu huo huo Simba ilimsajili na Abdi Banda, yaani KAzi Kazi tu.

Mafanikio yake ni mengi lakini msimu wa mwaka 2015/16, Zimbwe alichaguliwa kuwa mchazaji bora chipukizi wa VPL huku Mashabiki wa Simba wakimchagua kama mchezaji bora wa msimu. Mwenyekiti wa Usajili kipindi hicho, Zakaria Hans Pope akimpatia gari kama zawadi baada ya kuwa na msimu mujarabu.

Tukija kwa upande wa ushabiki, Zimbwe ni shabiki lialia wa Manchester United, bila shaka kwa sasa presha ni juu nje ndani…

Nikiachana na Zimbwe saa acha nimuangazie Gadiel Michael Kamagi.

Alizaliwa Septemba 12, mwaka 1966, ana miaka 22 pekee. Amejiunga na Simba msimu huu akitokea Yanga Afrika, kwa mkataba wa miaka miwili, mkataba wake unatarajiwa kumalizika  June 30 mwaka 2021.

Kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Market, thamani ya Gadiel kwa sasa ni Euro laki moja ambayo ni zaidi ya shilingi milioni 254 za kitanzania.

Gadiel safari yake hadi kuifikia Simba haikuwa na mlolongo mkubwa, kwani alitoka na kukulia katika akademi ya Azam kuanzia mwaka 2014, na baadae alipandishwa timu ya wakubwa.

Aliitumikia Azam kwa kipindi cha zaidi ya misimu miwili kabla ya kujiunga na Yanga msimu wa 2017/18 akiwa kama mchezaji huru. Gadiel hakuondoka vyema kutoka Azam kwenda Yanga, Azam walionyesha nia ya kumtaka lakini kwa bahati mbaya zaidi, naye alionyesha nia ya kutimka.

Baada ya kutua Yanga, alichukua Namba moja kwa moja. Aliitumikia yanga kwa misimu miwili pekee kabla ya kusajiliwa na mnyama msimu huu.

Gadiel anakuwa mchezaji wa aina yake, aliyezichezea timu kubwa za Tanzania tena kwa mfuatano.

Gadiel uwanjani mambo yake sio ya kitoto, anaweza cheza nafasi zaidi ya moja, anaweza cheza kama beki wa kushoto, winga wa kushoto au kiungo wa pembeni upande wa kushoto yaani Left midfielder.

Gadiel Michael Mbaga na Mohammedi Husseni Zimbwe Jr ni miongoni mwa mabeki bora kabisa nchini . Mpira wanaocheza ni kiburudisho tosha cha kuwafanya watu wazidi kuwapenda na kuzidi kuwaaminisha kuwa, wao ndio mabeki bora zaidi wa kushoto kwa sasa nchini.

Msimu uliopita wawili hawa walikuwa ni mabeki wa kutumainiwa katika timu zao, Gadiel alikuwa hana mbadala pale Jangwani vivo hivyo baada kutoka majeruhi Zimbwe aliishikilia namba iliyomponyoka Asante Kwasi kutokana na Majeraha.

Wachezaji hawa wote wawili wamecheza timu tofauti, Azam ndio kituo pekee ambacho wote walikipitia japo hawakukutana, kituo cha pili ni Msimbazi. Kituo hiki kinaonekana kigumu kwa kila mmoja, kwani wote wana ubora Mkubwa.

Tukutane sehemu ya pili, ambapo huko tutagusa uchambuzi kiufundi, kuona jinsi wachezaji hawa wanavyocheza wakiwa uwanjani na sifa zao kuu katika takribani kila mchezo. Asante.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.