Sambaza....

Mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or na mchezaji wa zamani wa klabu ya Liverpool na timu ya Taifa ya England Michael Owen amesema Mohamed Salah anapaswa kuchukua tuzo ya Ballon d’Or kwa mwaka 2018 kama Liverpool itachukua kombe la Klabu bingwa Ulaya.

Owen akihojiwa na kituo cha Omnisport  katika kipindi cha Sports Tonight/Dubai Eye 103.8 amesema Salah ana nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo mwaka huu kuliko mchezaji yoyote lakini itakuwa haki zaidi kama itaambatana na taji la Ulaya.

“Ni hakika, nina maana kwa namna anavyocheza, labda tuiweke kwa namna hii: ana uwezo na ana haki ya kuchukua tuzo hiyo,” Alisema Owen mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or kwa mwaka 2001.

“Ila itategemea na medali ambazo atatwaa mwishoni mwa msimu huu, unaweza kuwa na msimu mzuri lakini usiposhinda chochote, una kuwa na bahati mbaya, unahitaji kuwa na kikombe chochote au kushinda UEFA Champions League, ndio maana nasema kama Liverpool itachukua taji hilo basi Salah ana nafasi nzuri zaidi,” Owen amesisitiza.

Mpaka sasa Salah amekuwa na msimu mzuri akiwa na timu ya Taifa ya Misri pamoja na klabu yake ya Liverpool akifunga mabao 44 huku mabao 11  yakitokea katika michezo 14 aliyocheza katika mashindano ya Klabu bingwa Ulaya.

Salah amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 32 katika michezo 38 ya ligi kuu England, na kushinda kiatu cha dhahabu, pamoja na kuchukua tuzo ya Mchezaji bora wa msimu (PFA Player of the Year) na tuzo ya waandishi wa habari (FWA Footballer of the Year).

Kama Salah akichukua tuzo ya Ballon d’Or kama Michael Owen alivyopendekeza basi atakuwa ameweza kuzima zama za magwiji Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ambao wamegawana tuzo tano katika kipindi cha miaka kumi iliyopita (2007-2017), na ikumbuwek mwaka 2007 ndio ulikuwa mwaka wa mwisho kwa Liverpool kucheza fainali ya UEFA Champions League wakifungwa na AC Milan kwa mabao 2-1.

Mwaka huu Liverpool watacheza fainali na Real Madrid mjini Kiev baada ya kufanikiwa kuwaondoa FC Porto, Manchester City na AS Roma katika hatua za mtoano.

Sambaza....