Sambaza....

Kuna mengi yamebadilika sana tangu mwalimu Pierre Lenchantre na Masoud Djuma walipoichukua timu. Wengi wanaweza wakaona mabadiliko ya kimfumo peke yake kutoka timu kucheza 4-4-2 mpaka 3-5-2

Hiki ndicho kitu kinachoonekana kwa nje, lakini kwa ndani kuna vitu vingi sana ambavyo vinaonekana na vinadhihirisha kuwa kwa sasa Simba inacheza kibingwa.

Baada ya Simba kutolewa na Al-Masry tulitegemea timu ingepoteza uelekeo kwa sababu ya kutoka kwenye mashindano makubwa

Mashindano ambayo walikuwa wanayaota kila siku baada ya kukaa misimu minne bila kucheza mashindano haya, walikuwa wameyakumbuka katika kiwango cha hali ya juu kuanzia kwa mashabiki, viongozi mpaka wachezaji.

Shauku ya kufika mbali ilikuwa kubwa, siku ya mechi ya Al-Masry katika uwanja wa Taifa , Dar-es-Salaam ilijidhihirisha hilo. Mashabiki walikuja wengi kuishabikia timu yao

Muda mwingi walikuwa wakipiga hamasa ya kuwataka vijana wao wapigane bila kuchoka, wachezaji walipigana, miguu yao ilikuwa na shauku ya kuwa na mpira kila muda. Matokeo ya sare ya 2- 2 hayakuwa matokeo yaliwakatisha tamaa.

Walipanda ndege wakiamini kabisa wanaenda kufanya vizuri nchini Misri, nia ya kufanya vizuri ilionekana uwanjani ,matokeo ya bila kufungana yaliwafanya watolewe kwenye michuano hii.

Michuano ambayo walikuwa na hamu nayo, kama tunavyojua kwa timu zetu kubwa hapa nchini zinapotolewa katika mashindano ndicho huwa chanzo cha migogoro ndani ya klabu.

Migogoro ambayo husababisha mwenendo wa timu kuwa mbovu kwenye ligi kuu, mara hii ikawa tofauti, utulivu ulitawala ndani ya timu na wachezaji waliandaliwa dhifa ya mchana wakapata chakula cha pamoja na wachezaji kupongezwa kwa jitihada walizozionesha.

Kwenye kombe la mapinduzi kulitokea jambo ambalo lilikuwa siyo la kinidhamu nzuri baada ya kuonekana Kichuya kususia kukaa benchi baada ya kutolewa yeye pamoja na Jonas Mkude, lakini benchi la ufundi lilimaliza tatizo hilo bila kuleta mpasuko kwenye timu

Hii ilionesha kuna mshikamano mkubwa ndani ya timu na klabu kwa ujumla, hata Yanga ilipofanikiwa kufikia alama za Simba na kulingana nao wengi walitegemea Simba itakuwa na presha kubwa kuwaona wapinzani wao wakiwa wamewakaribia.

Yalitokea msimu uliopita wengi wakaona yanaweza kutokea tena msimu huu, lakini ikawa tofauti presha hawakuruhusu iwe ndani yao. Akili , nguvu waliziweka kwenye kila mechi walizokuwa wanacheza hawakufikiria tena kuhusu Yanga aliyekuwa karibu yake

Alikimbia huku akijiangalia yeye ni wapi alipokuwa anaelekea hakuruhusu kabisa kutazama alikotoka kuona ni wapi alipo mpinzani wake.

Utulivu ukawa mkubwa ndani ya timu, hata aina ya kucheza mechi husika kukawa kuna badilika kila baada ya mchezo.

Baada ya kufunga goli la kwanza dhidi ya Njombe Mji walianza kulinda goli lao. Hawakuona haja ya wao kuendelea kufunguka kutafuta magoli mengi, wameshajua kabisa kipindi hiki ligi ilipo ni kipindi ambacho timu inahitaji ubinngwa na siyo magoli mengi

Hiki kitu hata kwenye mechi ya leo dhidi ya Tanzania Prisons kilionekana, baada ya kupata goli walionekana kuwa imara kulilinda goli lao na hata walipofunga goli la pili ilitosha kuwaonesha kuwa wameshapata alama muhimu kwa ajili ya ubingwa.

Mzunguko wa kwanza timu ilikuwa inashinda magoli mengi, kipindi hiki timu ilikuwa lazima ifunguke kwa ajili ya kupata ushindi mnene kwa akiba nzuri kwa tahadhari kama iliyotokea msimu jana

Hata mzunguko huu wa pili,viungo wa kati wanaotumika ni wale ambao wanauwezo wa kushambulia na kukaba kwa pamoja (Shomari Kapombe na Asante Kwasi aliyetumika mechi ya leo dhidi ya Tanzania Prisons)

Hii ni kuiwezesha timu iwe na uwiano mzuri eneo la katikati mwa uwanja (wakati wa kukaba na wakati wa kushambulia)

Hiki kilionesha kuwanufaisha Simba kwa sababu wakati timu ilipokuwa inashambulia viungo hawa walikuwa wnahusika katika kujenga mashambulizi,na timu ilipokuwa inashambuliwa walisimama imara kukaba (hii inaonesha timu inacheza kwa tahadhari bila kujali wanakutana na mpinzani wa aina gani , kila mpinzani walimheshimu) na hii ndiyo sifa ya timu bingwa ( kumheshimu kila aina ya mpinzani).

Heshima hii imeanzia kwa mashabiki wao ambao wanaonekana kuwa pamoja na benchi la ufundi, viongozi na wachezaji.

Viongozi pia wako kwa ajili ya wachezaji muda mwingi. Mshikamano huu ni tasafri tosha kuwa Simba inaendeshwa kibingwa.

Sambaza....