Ligi

Simba na Yanga zinatakiwa zirudi kwenye msingi

Sambaza....

Hadithi imejirudia ile ile, hatujawahi kuwa na hadithi mpya tena yenye kufurahisha kwenye michuano ya kimataifa iwe katika ngazi ya vilabu au timu ya Taifa.

Hii ni kwa sababu hatuna misingi imara ambayo tumeijenga sisi kama sisi ya kutuwezesha tufanye vizuri kwenye michuano hii ya kimataifa.

Misingi hii haipo kwenye ligi zetu, shirikisho la mpira wa miguu Tanzania mpaka kwenye vilabu vyetu

Ligi zetu zimekuwa dhaifu sana kuanzia ligi za ngazi za chini mpaka ngazi ya juu (ligi kuu).

Tumetengeneza mazingira ambayo tunatoa timu ambazo siyo shindani kwa sababu ya mazingira mbalimbali kama waamuzi, uwezo wa kuibua vipaji ambavyo vitaleta msaada mkubwa kwenye timu husika.

Ndiyo maana hata timu ambazo zinapanda madaraja mbalimbali zinakuwa timu ambazo ni dhaifu.

Mfano mzuri ligi daraja la kwanza imekuwa ligi yenye kulalamikiwa sana kila siku na hii ni kwa sababu aina ya uendeshwaji wake.

Timu nyingi zimekuwa zikiandaliwa mazingira ya uonevu zinapokuwa katika viwanja vya ugenini, na kuna wakati mwingine waamuzi uhusika moja kwa moja kuharibu mazingira ya mchezo.

Kitu hiki hupelekea kupandisha timu ambazo ni dhaifu katika ligi kuu, ligi ambayo inatoa mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Ni ngumu kupata mwakilishi dhabiti wa kuiwakilisha nchi kama una ligi ambayo ina idadi kubwa ya timu ambazo ni dhaifu.

Bingwa wa ligi atapata jaribio ambalo jepesi ambalo litamfumba macho nakujiona yeye ni bora.

TFF wanatakiwa kusimamia ligi daraja la kwanza iwe ligi ambayo inachezwa kwa haki ili tupate timu imara katika ligi kuu.

 

Kuna kanuni inayo zitaka kila timu za ligi kuu kuwa na timu za vijana, na timu hizo za vijana zinatakiwa zicheze mechi ya utangaluzi kabla ya mechi ya wakubwa.

Hii kanuni usimamizi wake hauwekewi mkazo na TFF, na vilabu vinachukulia kitu cha kawaida.

Maendeleo halisi ya mpira wa miguu yanaanzia chini, hayaanzi kwa mtu mwenye umri wa miaka mingi.

Hatuna muendelezo wa kupata vipaji bora kwa sababu hatuna mazingira mazuri ambayo yanawezesha vilabu kuibua , kulea na kuvikuza vipaji mbalimbali.

Vilabu vyetu vimekuwa vikiegemea katika kusajili wachezaji kwa kutumia pesa nyingi kitu ambacho kuna wakati wanapata wachezaji ambao hawana viwango vikubwa.

Kitu ambacho kama wangeamua kugeuka na kuanza kuibua, kulea na kuvikuza vipaji mbalimbali vya watoto wangepata urithi mkubwa wa vipaji ndani ya timu ya wakubwa na kuwafanya wao waendelee kuwa washindani kwa muda mrefu.

Tunatakiwa tusijilaumu kwanini tumetoka kwenye mashindano, tunatakiwa kujiuliza kwanini tumeshindwa kufanya vizuri kwenye mashindano haya.

Kuna umuhimu kwetu sisi kuumizwa na matokeo tunayoyapata katika mashindano ya kimataifa.

Tunaamua kushindana kimataifa huku tunasura ya kitaifa, hatuna sura ya kimataifa ndani yetu?

Uliiona jezi ya Al-Masry? ina chapa za wadhamini  kuanzia nguo ya juu mpaka bukta yao.

Image result for images almasry

 

Hii inawafanya kuendesha timu katika mazingira rafiki, mazingira ambayo yanatia motisha kwa wachezaji wetu lakini kwetu sisi ni tofauti sana.

Mfano wadhamini wa Township Rollers waliokuwa wanacheza na Yanga ni wadhamini nane (8), wakati Yanga ina mdhamini mmoja tu msimu huu ukiachana na macron ambaye mkataba wake unaanza msimu kesho.

Image result for images township rollers vs yanga

Hii inaonesha tofauti ya uendeshwaji wa timu za wenzetu na timu zetu, hakuna misingi mikubwa ya kibiashara inayohusika kuendesha timu zetu.

Hivo wakati tunatoka Botswana na Misri tunatakiwa turudi na somo kubwa ambalo tunatakiwa kulifanya kwa vitendo.

Somo la kujiendesha kibiashara kwa timu zetu ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza morali kwa wachezaji.

Hata somo la kurudi katika misingi ya kuibua vipaji tunatakiwa tusilipuuzie, wakati tunaiendesha timu kibiashara ndiyo wakati huo huo tunaotakiwa kufikiria kuanzisha timu za vijana ambazo zitakuwa chachu kwenye maendeleo yetu.

Maendeleo ambayo yatachagizwa kwa kiasi kikubwa na TFF kuamua kusimamia ligi ziwe na ushindani mkubwa ili tupate wawakilishi imara.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x