Emmanul Okwi
Blog

Sitoshangaa Okwi akisajiliwa tena msimu ujao na Simba

Sambaza....

Kuna penzi tamu kama penzi la Emmanuel Okwi na timu ya Simba ?. Hapana shaka ni mara chache sana kuona wapenzi wa aina hii katika dunia ya leo.

Wapenzi ambao mioyo yao wamekabidhiana kwa dhati kabisa. Hata wakigombana hurudiana kwa bashasha na furaha tele.

Hili ndilo penzi ambalo hunishangaza sana, penzi ambalo mara nyingi huwa wanaachana na kurudiana kwa mabusu kila sehemu ya mwili.

Okwi (kulia)

Emmanuel Okwi aliwahi kuachana na Simba akajiunga na Yanga. Ulikuwa usaliti mkubwa sana unaouma kwa Simba.

Simba walisalitiwa sana, ni sawa na mpenzi wako kuanzisha mahusiano na adui yako mkubwa duniani.

Hiki ndicho kilichotokea, Emmanuel Okwi alienda kuishi kwa adui mkubwa wa Simba tena akimtumikia kama mpenzi wake ndani ya mwaka.

Mwaka ulipoisha mapenzi na Yanga yaliisha Emmanuel Okwi akarudi sehemu ambayo moyo wake uliumbwa, sehemu ambayo moyo wake kawekeza.

Hata baada ya yeye kuamua kuanzisha mahusiano na mzungu wa Denmark, na tukaamini kuwa atatulia kwa sababu atapata kila aina ya huduma muhimu lakini ikawa tofauti.

Pamoja na huduma nzuri, maisha mazuri kule Denmark, Emmanuel Okwi aliamua kurudi tena Simba.

Alikumbuka mahaba ya msimbazi, alikumbuka upendo wa msimbazi, alikumbuka kudekezwa na hata Simba walimkumbuka sana Emmanuel Okwi.

Kwa kifupi wote walikumbukana sana, wakarudiana tena kwa mara nyingine na penzi lao likaanza kupamba moto ipasavyo.

Haya ndiyo maisha ambayo yamejengwa kati ya Simba na Emmanuel Okwi. Kila Emmanuel Okwi anapoondoka hujikuta anayakumbuka maisha ya Simba, na Simba nao hujikuta wanakumbuka huduma ya Emmanuel Okwi.

Kukosekana kwa mtu ambaye anaweza kuziba ipasavyo pengo la Emmanuel Okwi kiufasaha ndicho kitu ambacho husababisha Simba kutaka kurudiana na Simba.

Na hiki ndicho kitu ambacho naanza kukiona mapema. Simba watamtamani sana Emmanuel Okwi kurudiana naye tena kwa mara nyingine.

Wamemsajili Deo Kanda, mtu ambaye ndiye atakayeamua kuendeleza au kulizika penzi la Emmanuel Okwi na Simba.

Yeye ndiye yuko katika eneo ambalo Emmanuel Okwi amekuwa akicheza kila alipokuwa anacheza Simba, yeye ndiye anayetakiwa kuwasahaulisha wana Simba kuhusu Emmanuel Okwi.

Njia pekee ya kuwasahaulisha ni yeye kufunga sana magoli kama ambavyo alivyokuwa anafanya Emmanuel Okwi na kutoa sana pasi za mwisho za magoli, tofauti na hapo Emmanuel Okwi atarudi tena Simba


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.