Blog

Sure Boy! Afisa mipango wa asili dimbani!

Sambaza....

Ukifika Mbagala rangi tatu, Panda gari zinazoelekea Mbande kisha mwambie Konda akushushe Azam. Hivyo ndivyo utaelekezwa ukiulizia wapi yalipo maskani ya klabu tajiri na kubwa Tanzania, Azam Fc.

Ukifika ofisini utapewa madini mengi, na nakuahidi utafurahia saana lakini ukifika uwanjani wakati timu hiyo inacheza basi utafurahi zaidi na zaidi, unajua kwa nini?.  Mosi jezi zao ni zenye kung’ara, Pili utashuhudia vipaji na mpira unaovutia, tatu ni kumuona afisa mipango akipanga na kupangua mipango kirahisi sanaa katikati ya uwanja.

Ndio, bila ya hata kuambiwa tazama, lazima utaiona jezi iliyochapishwa namba nane (8), mgongoni kwa jamaa flani mfupi kiasi mwili wa kunyumbulika na miguu yenye miujiza mingi, wenyewe wanamuita “Sure Boy”.

Salum Aboubakar “Sure Boy” akimuacha kiungo wa KMC Abdul Hillal.

Jina lake kamili ni Salum Abubakar, huyu ni Ofisa mipango wa asili, kazaliwa na cheo hicho na kupewa kibali na kazi ya kusimamia mipango yote awapo Dimbani na amefanya hivyo zaidi ya miaka 10, kwa ufasaha akiwa ndani ya uzi wa Azam Fc na Taifa Stars.

Kandanda likiwa kwake jua tayari mipango imeanza, kushoto, kulia, mbele, nyuma kote anakua ashatizama huku akili na miguu vimeshawasiliana wapi apeleke kandanda na kwa njia gani.

Iwe Pasi ndefu, fupi, ya juu, ama ya chini hakika itafika vyema pale ilipotakiwa kwenda kwa muda muafaka kisha atatengeneza mpango mwingine ‘Chap chap’ wa kuuchukua mpira na kuupeleka sehemu nyingine, yaani kama uliwahi kusikia maneno ‘Anachukua, anatoa, anaitaka tena’ basi Sure boy ndiye tafsiri kamili.

Salum Aboubakar “Sure boy” akimtoka mchezaji wa Ruvu Shooting

Mpira ukiwa kwa wapinzani pia ataweka mipango madhubuti ili kuupata mapema kabla haujaleta madhara, anatumia njia zote iwe ya damu au maji, yaani kama ni kuziba njia ataziba mapema, na kama ni figisu na kiatu hapo ndipo mipango yake ilipoanzia😂.

Si rahisi, ni juhudi, imani na mambo mengine makubwa kibao ndivyo vinamfanya fundi huyu kuzidi kuwa bora siku baada ya siku huku akiacha historia chanya kila kiwanja anachokanyaga.

Anavyonesa, Anavyokimbia, Anavyomiliki mpira na kuutoa kwa namna tofauti tofauti ni dhahiri ni burudani tosha kwa mtazamaji na mpenzi wa Soka.

Endelea kuuwasha moto, imani yetu ni kubwa sana kwako, Kila la Kheri mtu wa Mpira SURE BOY.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.