Sambaza....

Kuna vitu vingi sana vya kuvutia katika dunia ya leo, dunia tunayoishi ni moja ya kitu bora kuwahi kutokea ambacho kinavutia katika macho yetu.

Dunia imebeba kila kitu ambacho kinastahili sifa ya mvuto, imebeba mbuga za wanyama wenye wanayama wengi wa kuvutia.

Wanyama ambao wanategemea maji kutoka kutoka katika vyanzo vya maji mbalimbali.

Kuna mito, maziwa na bahari. Vyote hivi vinavutia kwa kifupi ardhi hii ya dunia iliumbwa kwa ufundi ambao hujawahi kutokea.

Ufundi ambao ulifanikisha kutenganisha mabara, na moja ya bara ambalo lilipendelewa ni bara la Afrika.

Bara ambalo linautajiri mwingi, wazungu hufunga safari kila wapatapo mapumziko kwa ajili ya kuja kuiangalia Afrika.

Ndilo bara ambalo linatunza na kuenzi utamaduni wao mkubwa, utamaduni ambao unavutia kwa kiasi kikubwa.

Leo hii tunajivunia kuwaona wamasai kwa sababu walitunza na bado wanaenzi utamaduni wao.

Utamaduni wao bado unaishi na kikubwa zaidi utamaduni wao unavutia sana. Kwa kifupi sisi Wafrika ni watu wa kipekee.

Upekee wetu ulionekana kwa ukubwa katika kombe la dunia La mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.

Kombe la dunia lililoacha kumbukumbu kubwa katika vichwa vya watu wengi.

Kila mmoja atakuwa na kumbukumbu yake lakini kumbukumbu inayobaki katika vichwa vya watu wengi ni Vuvuzela.

Huu ni utamaduni mkubwa na wa kiutofauti katika ushangiliaji wetu.

Ushangiliaji huu ulikuwa tofauti na aina nyingine ya ushangiliaji. Hapa ndipo upekee wa bara la Afrika lilionesha upekee ambao ulikuwa haujawahi kutokea sehemu yoyote.

Upekee ambao mpaka leo unadumu katika kumbukumbu zetu kwa sababu WaAfrica tulikuwa na kitu ambacho kiliacha alama.

Alama ambazo mara nyingi hubaki kama kumbukumbu zinazoishi. Ndiyo maana katika kumbukumbu zangu kuna tukio moja linaloishi.

Tukio hili lilifanyika katika michuano hii ya kombe la dunia la mwaka 2010 huko Afrika Kusini.

Inawezekana Luiz Suarez alikuwa mtu aliyechukiwa kwa kiasi kikubwa katika michuano hiyo na kuwa shujaa katika nchi yake.

Lakini kuna tukio moja la kutisha na kushangaza ambalo lilitokea kwenye michuano hii.

Tukio la Argentina kuwa na safu Kali ya ushambuliaji. Safu hii kabla ya michuano hii washambuliaji wake walifunga magoli 176 kwenye ligi ambazo walikuwa wanachezea.

Idadi hii ya magoli ilikuwa inatisha! , ilikuwa inaogofya! , na ilikuwa inatia matumaini makubwa kwa watu wa Argentina kuwa timu yao inaweza kubeba kombe hili la dunia.

Hadithi ilikuwa tofauti sana, hawakuweza kufanikiwa kubeba kombe la dunia. Safu yao ya ushambuliaji haikuwa na uwezo wa kuibeba timu mbele ya timu imara kama Hispania (waliokuwa mabingwa wa michuano hiyo).

Argentina walikuwa na safu Kali ya ushambuliaji lakini haikuwa na timu imara. Hata katika michuano ya kombe la dunia nchini Brazil mwaka 2014 hawakuwa na uwezo wa kuifunga timu iliyokuwa imekamirika, ambayo ilibeba ubingwa wa kombe hilo (Brazil).

Russia walibahatika kuandaa michuano ya kihistoria, michuano ambayo ilikuwa na mapinduzi makubwa ya kimbinu na kiufundi ndani ya uwanja.

Michuano ambayo Argentina ilienda na safu Kali ya ushambuliaji kwa mara nyingine tena.

Safu ambayo ilikuwa imefunga jumla ya magoli 124 katika ligi mbalimbali ambazo washambuliaji wake walikuwa wanacheza.

Wengi waliona kuwepo kwa washambuliaji nyota duniani katika kikosi cha Argentina ilikuwa silaha kubwa sana kwao.

Ni kocha yupi ambaye angekataa kuwa na Lionel Messi, Paolo Dyabala, Gonzalo Higuain , Angelo Dimaria na Sergio Aguero?

Lakini mwisho wa siku pamoja na kwamba timu ilikuwa imesheheni washambuliaji wa kutisha , timu iliishia katika hatua ya kumi na sita bora.

Hawakuwa na timu imara ila walikuwa na safu Kali ya ushambuliaji, hiki ndicho kitu ambacho kiliwaangusha.

Ndicho kitu ambacho kwa mbali nakiona katika timu yetu ya Taifa ya Tanzania.

Imekuwa na washambuliaji tishio ambao kwa msimu huu wamekuwa wakifanya vizuri katika ligi zao za nje wanazochezea.

Mwezi wa nane ilikuwa mwezi wa Mbwana Ally Samatta, alifunga kila alipokuwa akihitaji kufunga ndiyo maana mwezi wa nane uliisha akiwa amefunga jumla ya magoli 8.

Magoli ambayo yalimpeleka kuwa mfungaji wa 6 bora katika klabu ya Genk.

Hii ni historia kubwa na ndiyo historià ambayo inatafutwa na Simon Msuva, mchezaji ambaye kwa nguvu zake amekuwa akijitahidi kufunga magoli ambayo yamekuwa yakiibeba timu yake, alimaliza msimu akiwa mfungaji bora wa nne katika ligi.

Vipi kuhusu Thomas Ulimwengu? Mchezaji ambaye alizua mijadala mingi kuhusu kutokuwa au kuwa na timu ulaya?

Leo hii yupo Sudan , kiwango chake kinaimarika kila uchwao hata ufungaji wake wa magoli umekuwa ukiimarika kila sekunde zinavyozidi kwenda.

Kitu hiki kinatoa matumaini kuhusiana na maendeleo yake, maendeleo ambayo tunayatamani kwa manufaa yetu , ndiyo maana tunafurahia kuhusu ubora wa Chilunda na umahiri wa Rashid Mandawa.

Ni washambuliaji ambao kwa sasa ni tishio. Kwa kifupi timu yetu ya Taifa imebeba washambuliaji ambao wanafanya vizuri kwa sasa katika ligi zao.

Swali kubwa linabaki , je kutakuwa na muunganiko mzuri ambao utawabeba washambuliaji hawa ili kukamilisha ubora wa kikosi chetu ?

Huwezi kusema una kikosi bora kwa kujivunia safu ya ushambuliaji pekee wakati safu ya kiungo na ya ushambuliaji ina udhaifu, hapo ndipo tafasri ya neno “timu bora na imara” inapoondoka.

Sambaza....