Ligi Kuu

Tatizo la Lwandamina ni kukimbia na tope mwili mzima

Sambaza....

Huwezi sikia kelele za maumivu au za furaha kutoka kwake, uhakika wa hatua zake ndicho kilichopo kichwani mwake.

Haijalishi njia anayopitia, kwake yeye kitu cha msingi kuuona mguu wake ukisimama na kusogea sehemu moja tofauti na aliyokuwepo awali.

Ndiyo maana anatembea akiwa na jeshi dogo lakini lenye nguvu na ushikamano mkubwa katika ardhi ya vita.

Jeshi ambalo linajua thamani ya nembo iliyopo kifuani mwao, kwao wao nembo iliyopo kifuani ina thamani kubwa kuzidi kitu chochote.

Ndiyo maana wachezaji wanacheza na kuipatia timu matokeo muhimu wakiwa katika nyakati ambazo hawakuzoea awali.

Hawapo katika nyakati zile zilizokuwa zimejaa majira ya maziwa na asali, nyakati ambazo njaa haikuwa karibu na matumbo yao.

Image result for Yanga wakishangilia images

 

Shibe ndiyo hadithi pekee ambayo walikuwa wameizoea kwa misimu mitatu iliyopita.

Ilikuwa nadra kwa Yanga kusikia mchezaji anadai mshahara wa miezi minne kipindi hicho, lakini kipindi hiki imekuwa ni kawaida sana.

Siyo jambo la kushangaza hata kidogo, lakini kinachoshangaza ni pale unapoona wachezaji wakiwa uwanjani, huwezi kuona njaa ambayo inasemwa sana.

Miguu yao imeshiba milo yote mitatu, wachezaji wana njaa ya matokeo wakiwa uwanjani, wanapigana kupata matokeo ambayo yanaisaidia timu kwa kiasi ƙkikubwa.

Ingawa kikosi chao siyo kipana kwa sababu ya wachezaji wengi kukumbwa na majeraha ƙkila mara, lakini jeshi lao dogo linapigana kwa ushirikiano mzuri

George Lwandamina amefanikiwa kuunganisha uzi na sindano kwa ufasaha, hakuna sehemu iliyo wazi ambayo inabaki bila kushonwa.

Wasusi wake wana moyo wa kufanya kazi katika mazingira ya aina yoyote na hili limejidhihirisha kipindi hiki ambacho Yanga haiko imara sana kiuchumi kama misimu mitatu iliyopita na timu ikiwa inakabiliwa na majeraha mengi ya nyota wake.

Nyota ambao walionekana ni nguzo muhimu na imara katika timu.

Timu inamkosa Donald Ngoma, mtu ambaye alikuwa chachu ya mafanikio makubwa ya safu ya ushambuliaji msimu juzi na msimu jana.

Image result for kamusoko na ngoma images

Kuna kitu kinapungua, idadi ya magoli wanayoyapata inapungua, kuna wakati Obrey Chirwa alionekana kuwa msaada lakini majeraha yakawa rafiki kwake akawafuata Donald Ngoma na Amis Tambwe.

Mpaka sasa timu haina mshambuliaji halisi wa katikati , lakini Geroge Lwandamina ameifanya timu ipate magoli kupitia mchezaji yoyote ndiyo maana kina Hassan Kessy, Gadiel Michel, Papy Kabamba “Tshishimbi” wamekuwa wakifunga magoli kipindi hiki kigumu ambacho timu inawakosa nyota wengi katika eneo la ushambuliaji

Eneo hili linaweza kuonekana limeathirika kwa kiasi kikubwa lakini na idara mbalimbali zina wachezaji muhimu ambao wapo wodini.

George Lwandamina amefikia hatua ya kumtumia Said Juma “Makapu” kama beki wa katikati kutokana na wachezaji wa eneo hilo kubadilishana vipindi vya kupata majeraha. Said Juma “Makapu” alionekana kama mtu ambaye angeziba nafasi ya Kamusoko aliyekuwa majeruhi, lakini akarudishwa eneo la beki wa kati.

Image result for george lwandamina images

Kuna kipindi Yanga ilifikisha wachezaji kumi na moja wodini, tena wachezaji nyota ambao ni nguzo ya timu

Lakini George Lwandamina hakutetereka aliendelea kukimbia na jeshi dogo ambalo alilitia ujasiri mkubwa kwenye mioyo yao.

Ikafikia hatua vijana waliokuwa Serengeti Boys mwaka jana kupewa nafasi, na kila walipokuwa wanapewa nafasi walionesha kutomwangusha mwalimu.

Ndiyo maana hata Ramadhani Kabwili alifungwa goli moja tu alipoaminiwa kwenye michezo minne.

Alionesha ukomavu na uimara tofauti na umri wake, hii ni kutokana na sumu ambayo aliwekewa na George Lwandamina.

Sumu ambayo ilimwezesha Akilimali kufanikiwa kuhusika kwenye goli kwa kutoa pasi ya mwisho dakika moja tu baada ya kuingia.

Sumu ambayo ilimfanya Edward Mwakaluka “Makka” kuwa mtawala wa dimba kila mechi ambayo alipewa nafasi na George Lwandamina.

Kila mchezaji ana njaa na hasira ya mafanikio kila akipewa nafasi, timu inacheza kwa umoja na ushirikiano.

Haijalishi mpira wanaocheza ( wakuvutia au usio wa kuvutia) kwao wao kupata matokeo ndicho kitu cha muhimu.

Na hiki ndicho kitu kikubwa kinachoonekana kwenye miili ya wachezaji wote na George Lwandamina amefanikiwa kukiweka ndani ya wachezaji.

Hali ambayo inawafanya wapigane bila kujali njia wanazoipita , wanapita njia ngumu sana kiuchumi na kitabibu lakini wameshikamana ndiyo maana katika michezo sita iliyopita imeshinda yote, ikiwa ni timu pekee iliyoshinda michezo sita iliyopita kwenye ligi kuu.

Tunaweza tusiwe na macho ya kumuona George Lwandamina kipindi hiki kwa sababu anakimbia akiwa amajipaka tope mwili mzima hivo ni ngumu kumtambua ndiyo maana wengi wetu tumeshindwa kumsifia na kumpongeza kwenye hili.

 

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x