Sambaza....

Shirikisho la kandanda nchini ‘TFF’ limetoa ufafanuzi kufuatia Klabu ya soka ya JKT Tanzania kulalamikia mchezo wao ujao wa ligi dhidi ya Yanga SC kupigwa uwanja wa Taifa badala ya Mkwakwani jijini Tanga kama inavyofahamika.

Akitoa ufafanuzi huo, Afisa habari wa TFF Clifford Mario Ndimbo amesema kwa mujibu wa barua ya JKT Tanzania ya Oktoba 15, 2018 ilielekeza wazi kuwa mechi zao za nyumbani dhidi ya timu za Simba na Yanga zitapigwa katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, lakini Bodi ya ligi ikatoa maelekezo kuwa mchezo namba 251 kati ya JKT Tanzania na Yanga utachezwa February 9, 2019.

“Kwa hiyo mchezo unaofuata ambao utachezwa Dar es Salaam hauna mkanganyiko wowote, ni mchezo ambao Yanga yeye ndiye mwenyeji wa mchezo huo na ndio maana unachezewa Dar, kwenye uwanja wa Taifa,”

“Mchezo ambao JKT Tanzania wao ni wenyeji upo pale pale utachezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani lakini utachezwa February 9, 2019 ukiwa kama mchezo namba 251 mchezo wa kiporo,” Ndimbo amefafanua.

Ikumbukwe jana klabu ya JKT Tanzania  kupitia kwa katibu mkuu Abdul Nyumba iliomba ufafanuzi kuhusiana na suala lao baada ya kuwepo kwa sintofahamu kuwa mchezo wao ambao awali ulipangwa kupigwa Mkwakwani umerudishwa jijini Dar, kwenye uwanja wa Taifa.

Sambaza....