Sambaza....

Tarehe 22/08/2017 niliamka na mawazo sana, mawazo ambayo yalitokana na mimi kuona furaha ambayo walikuwa nayo Watanzania baada ya kutangazwa Emmanuel Amunike kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars.

>>>Tunawekeza ubora wa paa la Taifa stars na kusahau msingi wake.

Kocha ambaye alicheza kwa mafanikio makubwa enzi za uchezaji wake. Alicheza vilabu vikubwa duniani. Miguu yake ilifanikiwa kukanya nyasi za Nou Camp huku ngozi yake ikifanikiwa kufunikwa na jezi ya Barcelona na mikono yake iligusana na mikono ya Ronaldo De Lima.

Waliishi pamoja katika ardhi ya Barcelona, walicheza pamoja, walifurahia pamoja na kutaniana sana katika vyumba vya kubadilishia nguo. Kwa kifupi Emmanuel Amunike ana alama zake ambazo aliziweka kipindi alipokuwa mchezaji.

Alama ambazo zilimpa heshima kubwa sana katika ulimwengu wa mpira ndiyo maana hata tuliposikia Emmanuel Amunike ametangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania tulifurahia sana.

Tuliona nuru ikiwa imekaribia kwenye giza ambalo tumeishi kwa muda mrefu. Nafsi zetu zilianza kuwa na matumaini kubwa huyu ndiye ambaye atatuongoza kufika sehemu ambayo tunatamani kufika.

Sehemu ambayo tumeiota kwa kipindi kirefu, kibaya zaidi tumekuwa tukiiota tukiwa kitandani tumelala, shuka letu likiwa limefunika ngozi yetu gubigubi.

Neno udhubutu wa kuzifikia ndoto zetu limekuwa halipo karibu sana na sisi. Tumekuwa watu wa mipango mingi sana, watu ambao tunaongea sana bila kufanya vitendo ambavyo vinaweza kutufikisha sehemu ambayo tunaitamani.

Mara nyingi tunapenda sana lifti na kuzipuuzia hatua za kufikia maendeleo, tunaamini katika kupata kitu kwa urahisi bila kuruhusu ngozi zetu kutiririkwa na jasho!.

Ndiyo maana kila wimbo ambao tunaimbiwa huwa hatuuisikii kabisa hata kuuelewa hatatuki kuuelewa tunaamini sehemu ambayo haiaminiki kabisa.

Tunaamini sehemu ambayo haijaandaliwa kuaminika ndiyo maana tunapata matokeo ambayo yanatuvunja mioyo yetu kila uchwao.

Ni lini tuliwaandaa hawa wachezaji tulionao kwa sasa kwenye timu yetu ya Taifa?, yani wametoka katika mkondo upi mzuri wa mpira ?, mkondo ambao unamfanya mchezaji kujifunza misingi ya mpira akiwa na umri mdogo?.

Ni wachezaji wangapi waliopo katika kikosi cha timu ya Taifa waliojifunza misingi ya mpira wakiwa na umri mdogo ?, hapana shaka hakuna na wengi wao wameanza kufundishwa misingi ya mpira wakiwa na umri wa miaka 17.

Umri ambao katika nchi za wenzetu mchezaji wa umri huu anapigana kupanda katika timu ya wakubwa kwa ajili ya kucheza ligi kuu!, lakini kwetu sisi ndiyo umri ambao tunawafundisha misingi ya mpira.

Tunapenda sana kuukimbia ukweli na kujificha kwenye vichaka vya kujifariji. Tutajificha kwenye kuchaka cha Emmanuel Amunike , tutamkebehi sana, tutamlaumu sana na kumuona hafai lakini ukweli unabaki pale pale kuwa njia sahihi ya mpira tumeshaikimbia na hatutaki kabisa kuifuata.

Njia ambayo tulitakiwa tuwe na vituo vya kuibua, kulea na kukuza vipaji ambavyo ni bora na vyenye makocha bora ambao wangetusaidia kuzalisha wachezaji imara ambao wangetengeza Taifa Stars imara.

Mbwana Samatta (Kushoto) na Ulimwengu (Kulia)

Njia ambayo ingetufanya tuwe na mradi wa kuzalisha makocha wengi sana ambao wangetumika katika kuibua vipaji vipya na kuwawezesha kuvilea.

Tuna idadi ndogo sana ya makocha nchini na hata hawa waliopo hawatumiki ipasavyo katika kuinua vipaji vya wachezaji wetu, kwa mazingira haya unategemea kuna kipi kipya ambacho tunaweza kukifanya ?

Ni vigumu sana kufika sehemu ambayo tunatamani kufika wakati hatujaamua kufika, ndiyo maana waswahili waliwahi kusema ukitaka kuruka agana na nyonga.

Sisi nyonga zetu hatujaziandaa kuruka na hii ni labda kwa sababu ya ugumu wa nyonga zetu tulizo nazo na hatutaki kabisa kuzilainisha ndiyo maana hata ligi yetu kuu hatujaamua kuifanya kuwa ligi bora na imara.

Tunaiendesha katika mazingira ambayo siyo bora, mazingira ambayo hayatengenezi uimara wa ligi yetu. Naamini ligi imara siku zote hujenga timu ya Taifa imara. Ligi yetu ni mbovu tunategemea timu ya Taifa imara ?

Ni ngumu sana kupata kitu imara katika mazingira ambayo waamuzi wa ligi yetu ni wabovu, hatuwezi kupata kitu imara katika mazingira ambayo hatujaamua ligi yetu kuifanya iwe ya kibiashara.

Ndiyo maana ligi haina mdhamini, timu hazina wadhamini kitu ambacho kinapunguza ushindani ndani ya viwanja.

Tuna wachezaji wangapi ambao wanacheza ligi imara za kulipwa ?, ni wachache sana, hata hawa tulionao wanacheza katika ligi za kawaida sana ni Simon Msuva, Abdi Banda na Mbwana Samatta pekee ndiyo wanacheza kwenye ligi zenye ushindani.

Tuna mpango upi wa kuongeza idadi ya wachezaji wa kulipwa kwenye ligi imara duniani ?. Tunatengeneza mawakala wa kutusaidia kwenye hili?, tunaushirikiano na vituo vya kulelea vipaji vya nje ili tuwe tunapeleka vijana wetu kwa ajili ya kulelea vipaji vyetu?

Kwa hakika tuna mengi hatujaamua kuyafanya na tunajidanganya kwa kujifariji uongo kuwa tuko tayari kwa safari ta kuelekea Afcon wakati miguu yetu bado iko kitandani na haijaamua kupiga hatua ya kwenda mbele!


Sambaza....