Sambaza....

Nilianza kujitambua vizuri kwenye masuala ya mpira wa miguu kipindi cha Jack Lyod Chamwangana, Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.

Kipindi cha marehemu Jack Lyod Chamangwana ndicho kipindi ambacho nilikuwa nafauatilia vizuri sana mpira wetu.

Ilikuwa tofauti na mwanzoni ambapo nilikuwa mpenzi tu, lakini sikuwa mfuasi haswaa wa mpira wetu. Kwa kifupi nilikuwa mkubwa kipindi hicho.

Kipindi ambacho Jack Chamangwana akiwa kocha wa Yanga. Klabu ambayo inachangamoto nyingi sana kuanzia kuiongoza mpaka kuichezea.

Ndiyo klabu ambayo inaumiza kichwa sana. Ndiyo klabu ambayo neno “Amani” huwa linakaa kwa muda mfupi sana.

Huwezi kutegemea amani ikae kwa muda mrefu ndani ya klabu ya Yanga. Wao wameshazoea haya maisha na wao wanayaona ya kawaida sana.

Kuna kipindi inapotoweka huathiri mpaka timu. Kuna wakati wachezaji hushindwa hata kupata mshahara kutokana na migogoro ya uongozi.

Vyote hivi nilivishuhudia kipindi cha Jack Chamangwana. Klabu ilikuwa na migogoro sana. Viongozi walikuwa hawaelewani wao kwa wao.

Marehemu Chamangwana (Kushoto)

Timu ikawa imetelekezwa, ikawa kama mtoto ya Yatima. Timu ikakosa baba na mama. Lakini ilipata msamaria mwema ambaye alikaaa nayo vizuri.

Msamaria ambaye aliwafanya wachezaji wazibe masikio ili wasisikie chochote kinachoendelea kwa viongozi wao.

Msamaria huyu hakuwa kiongozi wa Yanga ila alikuwa kocha wa Yanga. Kocha ambaye alijebeba majukumu yote ya uongozi.

Kuna wakati wachezaji walipokuwa wanalia njaa yeye ndiye aliyetoa pesa yake mfukoni ili awanunulie chakula.

Hakuruhusu kabisa kipindi kigumu cha Yanga kiathiri matokeo ya Yanga uwanjani. Kipindi kile kinafanana sana na kipindi hiki.

Kipindi ambacho Yanga inapitia wakati mgumu sana. Inapitia magumu mengi sana kwenye uchumi lakini inaongoza ligi kuu ya Tanzania bara!.

Timu ina morali kubwa sana ingawa wachezaji wake wanaweza kukaa miezi miwili bila kulipwa mshahara, lakini wakiingia uwanjani huonesha njaa ya kupata matokeo.

Njaa hii haijaanzia kwa wachezaji au viongozi imeanzia kwa kocha wao Mwinyi Zahera. Huyu ndiye mwenyekiti wa Yanga, huyu ndiye katibu, msemaji na kocha wa klabu ya Yanga.

Na cha mwisho kabisa huyu ndiye shabiki wa kwanza wa Yanga. Anaipenda sana Yanga. Anapita na Yanga kipindi kigumu sana lakini mapenzi yake kwa Yanga hayajawahi kupungua hata kidogo.

Hayuko tayari kumuona mchezaji akilia njaa, yeye ndiye atakayefanya kila awezalo kutuliza njaa ya wachezaji.

Anawapenda sana wachezaji wake, anawajali sana wachezaji wake kitu ambacho kinamfanya awe shabiki mkubwa wa Yanga..

Na hii ndiyo siri kubwa ambayo Yanga wanayo kwenye mbio za ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara. Usije ukashangaa wakalibeba kombe hili.

Kwa sababu tu wachezaji wanajihisi deni kwa kocha Mwinyi Zahera. Wanaona kabisa wanadeni kubwa ambalo wanatakiwa kumlipa Mwinyi Zahera.

Na sehemu pekee ya kumlipa ni ndani ya uwanja , ndiyo maana wanapigana sana kila siku ili timu ipate matokeo na wasimwangushe shabiki namba moja wa Yanga kwa sasa Mwinyi Zahera.

Mkondo huu wa kuwa na makocha ambao huja kuwa mashabiki wa kubwa wa Yanga ni wa kawaida sana kwa Yanga.

Nimekuambia tangu nianze kuwa mfuasi haswaa wa mpira niliwahi kushuhudia Jack Chamangwana akiwa shabiki mkubwa wa Yanga.

Leo hii kuna Mwinyi Zahera, lakini kabla yake kuna wengi walipita na kukiri kwa midomo yao kuwa ni mashabiki wa Yanga.

Zahera, Kocha wa Yanga

Unamkumbuka Maxio Maximo?, kocha ambaye alikuja kuleta msisimko mpya wa mpira wa miguu nchini akiwa na Taifa Stars?.

Tukaipenda tena Taifa Stars, mahaba ambayo yalisababisha kuanza kuiamini tena, tulinunua sana jezi za Stars.

Hata wanawake wetu walianza kuupenda mpira. Ikawa kawaida sana kukutana na mwanamke kwenye uwanja wa Taifa. Kitu ambacho kilikuwa siyo utamaduni wetu.

Hii ni kwa sababu ya Maxio Maximo. Mbrazil ambaye aliwahi kupata nafasi ya kuifundisha Yanga. Alikuwa kipindi cha neema sana lakini alidumbukia kuwa shabiki wa Yanga.

Azam Fc wanaye kocha Hans Van Pljuim muda huu lakini wanajua kabisa ana kadi ya Yanga. Ni mwanachama wa Yanga.

Aliipata kipindi akiwa Yanga. Alikuja pia kipindi cha neema kama ilivyokuwa kwa kocha Maxio Maximo.

Ushawahi kujiuliza kwanini yote haya yanatokea?, jibu ni moja tu. Mashabiki wa Yanga sana mahaba kweli. Mahaba ambayo huwafanya wengi nao wadumbukie kwenye huba.

Na kujikuta wanaipenda Yanga. Mashabiki wa Yanga wanaipenda sana timu iwe wakati wa njaa au wakati wa neema, huwa na timu nyakati zote.

Hans Pluijm akionyesha kadi ya Yanga

Hata timu ikienda mkoani hupokelewa kwa kishindo sana. Mahaba haya huwalevya wengi na kujikuta wanaishabikia timu wakati ni makocha.

Hata mtangulizi wa Mwinyi Zahera, George Lwandamina alidumbukia kwenye huba sema viongozi ndiyo waliosababisha aondoke.

Alikuwa tayari kutembea na timu kipindi kigumu. Aliwajali sana wachezaji wake. Hukuweza kumsikia akilalamika.

Aliwafanya wachezaji wacheze kwa ajili ya mashabiki na siyo kwa ajili ya viongozi. Hii ni moja ya bahati kubwa sana ambayo Yanga hubahatika kuwa nayo.

Sambaza....