Niyonzima
Ligi Kuu

Haruna Niyonzima dobi mwenye makazi yake Jangwani!

Sambaza....

Mnamo tarehe 5/2/1990, Nchini Rwanda mitaa ya Gisenyi alizaliwa kijana mmoja mwenye sura ya busara na maarifa mengi, na kuitwa jina Haruna. Ilimchukua miaka 15 tu, kujigundua kuwa yeye ni Dobi mzuri tena mpiga pasi za aina yeyote pale tu anapopata kitendea kazi pendwa ambacho ni mpira(kandanda).

Mwaka 2005, Niyonzima alijiunga na timu ya Etincelles akiwa kinda wa miaka 15, kisha kutimkia Rayon Sport ambapo alizidi kuimarika kabla ya mwaka 2007, kutua APR ambapo alidumu mpaka mwaka 2011.

Mara Paaap!! Mabingwa wa Kihistoria nchini Tanzania Yanga, katika pita pita zao wakamuona Dobi huyu, hawakuchukua maelezo mengi, ‘Chap’ kwa haraka wakamdondosha katika ardhi ya Nyerere na kumtambulisha kama mchezaji wao rasmi mwaka 2011.

Haruna Niyonzima akiutenga mpira wa kona.

Kilichofuata hapo ni historia, hakuna mwanaYanga asiyemjua, hakuna mchezaji wa timu pinzani asiemuhofia, wote walikua wakimuona tu, wanajua  leo kasheshe ipo pale katika eneo la dimba la katikati.
Kwa mafanikio makubwa na Burudani isiyo na kifani Niyonzima alidumu ndani ya Yanga kwa miaka 6 mfululizo huku akikata kiu ya mashabiki wa soka nchini haswaa.

Mwaka 2017, Tanzania Ilizizima, magazeti yalijaa, redio zilirindima, luninga ziling’aa na vijiweni kahawa zilinywewa saana yote kwa yote ikiwa ni kuzungumzia tukio la kijana huyu mwenye Damu ya Yanga kumwaga wino wa kuwatumikia Watani wao wa jadi Simba!.

Hapa ndipo majonzi kwa Yanga yalimwagika huku wale wa Simba huko vijiweni wakiagiza vinywaji kwa furaha, yaani ilikua shangwe wakiamini muunganiko wake na kina Jonas Mkude, Said Ndemla na Mo Ibrahim wapinzani wangepata mateso bila chuki uwanjani. Lakini ikawa tofauti.

Haruna Niyonzima akiitumikia Simba msimu wa mwaka 2018/2019.

Akiwa Simba mambo hayakwenda sawa kutokana na sababu tofauti tofauti za kimpira. Mkataba wake ulivyomalizika mwaka 2019 alirejea kwao Rwanda kujiunga na kikosi cha A.S kigali kabla ya mwaka huu maboss wapya wa Yanga GSM kumrejeshea na jeezi yake namba nane pale Jangwani.

Wajuzi wa mambo hunena kua ‘Hakuna Awali Mbovu’ naam! Niyonzima huyu wa Yanga moto wake ni ule ule kama aliokuwa nao kabla hajaiacha jezi za kijani na Njano.
Anapiga pasi za aina yeyote uzijuazo wewe, Mbwembwe zote anachanganya mithili ya kachumbali la mpemba kwenye Pilau, bila ya kukosea kila lengo lake hutimia.

Haruna Niyonzima akipiga mpira mbele ya nahodha wa Simba Mohamed Hussein.

Asikwambie mtu kitu babu, Haruna Hakizimana Fadhili Niyonzima ni moja kati ya Wapiga pasi mahili waliozaliwa miaka ya tisini ambao wataimbwa Vizazi na vizazi kutokana na Umaridadi wao Dimbani.

Umri ni namba tu, Imani yetu ni kwamba tutaendelea kumshudia Haruna Niyonzima (Dobi) akipiga pasi za Yanga kwa Umahiri wa hali ya juu huku mbwembwe na Ufundi ukichagiza Ubora wake kiwanjani.

Sambaza....