Sambaza....

Kabla hata hajavaa jezi ya Simba alikuwa tayari mfalme! , Mfalme wa burudani uwanjani, Mfalme ambaye wengi walikuwa wanaamini kuwa alikuwa katika eneo ambalo siyo sahihi.

Hata msemaji wa Simba, Haji Manara alikuwa anaamini kabisa kuwa Haruna Niyonzima alikuwa hafai kabisa kuchezea Yanga.

Aina ya mchezo wa Yanga ulikuwa hauendani sana na aina ya mchezo ambao Haruna Niyonzima aliokuwa nao!, wengi walioona Yanga siyo sehemu sahihi kabisa.

Lakini pamoja na kuwa sehemu ambayo ilionekana siyo sahihi kwake alifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kutoa burudani kwa mashabiki wa mpira wa miguu.

Burudani ambayo ilimpa hatimiliki ya kumiliki mioyo ya mashabiki wengi wa mpira wa miguu. Kila miguu yake ilipokuwa inakanyanga Katika nyasi za viwanja vyetu ndivyo ambavyo alifanikiwa kujisogeza katikati ya mioyo ya mashabiki wengi.

Alifanikiwa haswaa kujipenyeza kwenye mioyo ya mashabiki wengi, akawa kipenzi kikubwa cha mashabiki wengi wa mpira hapa Tanzania. Akawa mfalme halali katika falme za mioyo yetu.

Aliitawala vilivyo mioyo yetu!, tukafurahia utawala wake kwa sababu hakukuwa na uonevu wowote kwenye utawala wake. Kwenye utawala wake alihakikisha kila moyo ulikuwa unatoa tabasamu kutokana na aina ya mpira wake.

Alikuwa Mfalme halali wa mioyo yetu na alijua vilivyo kiufurahisha mioyo yetu. Wengi walimtaka atoke Yanga na aende Simba, sehemu ambayo iliaminika kuwa ina aina ya mpira ambao ulikuwa unaendana na mpira wake.

Msimu jana alifanikiwa kubadilisha makazi, akatoka katika mitaa ya Jangwani na kuingia katika mbuga ya msimbazi, mbuga ambayo ilikuwa halali kwa makazi ya klabu ya Simba.

Mashabiki wa Simba walifurahi sana kwa sababu waliona burudani ambayo walikuwa wanaitamani kwa muda mrefu walikuwa wamesogezewa karibu kabisa, yani sebuleni kwao.

Lakini mashabiki wa Yanga waliumia sana kwa sababu walikuwa wanaondolewa burudani ambayo ilikuwa inaonekana kwao kwa muda mrefu na ilikuwa inawafurahisha haswaa.

Wakaona huo ndiyo muda wa mwisho kwao wao kufurahia utamu wa miguu ya Haruna Niyonzima. Na mahasimu wao walikuwa wamefanikiwa kuwapiga sehemu ambayo ilikuwa inauma.

Haruna Niyonzima alikuja kwa mategemeo makubwa sana katika timu ya Simba!, mategemeo ambayo yalikuwa yamebeba furaha za waliowengi.

Mategemeo ambayo yalikuwa yanatarajiwa kuonekana ndani ya uwanja. Walitamani ligi ianze ili wafurahie kitu ambacho walikuwa hawana kwa muda mrefu. Kitu ambacho mahasimu wao walikuwa nacho kwa muda mrefu.

Ligi ilifika, wengi wakawa wanashauku kubwa ya kumuona Haruna Niyonzima akiwa na jezi ya timu ya Simba. Ngao ya jamii ndiyo ilikuwa mechi ya kwanza kwa Haruna Niyonzima kucheza.

Tena alicheza dhidi ya timu yake ya zamani ya Yanga. Jezi namba nane ndiyo ilikuwa imefunika mgongo wa Haruna Niyonzima. Wengi walitegemea makubwa sana.

Inawezekana presha kubwa ya mchezo ilisababisha kuficha uwezo mkubwa wa Haruna Niyonzima kwa wakati huo. Hakufanya vizuri ukilinganisha na mategemeo makubwa ya waliowengi.

Nafsi zetu ziliamini katika muda, tuliamini katika kumpa muda, ndicho kitu ambacho tulikifanya. Tuliamua kumpa muda Haruna Niyonzima. Lakini kadri ambavyo tulivyokuwa tunampa muda ndivyo ambavyo alikuwa anazidi kujiweka mbali na uwanja.

Kutokuelewana kwake na viongozi wa Simba kulimfanya asionekane kwenye viwanja. Hakucheza sana, hivo ile burudani ambayo wengi walikuwa wanaitegemea hawakuipata.

Hadi msimu uliopita ulipoisha hakuna kikubwa ambacho Haruna Niyonzima alikifanya!, ligi ikaisha bila ile kiu ya mashabiki wa Simba kukatwa.

Msimu huu ukaanza, hali ikawa ile ile, Haruna Niyonzima akawa anatumia muda mwingi sana Rwanda kuliko kwenye kituo chake cha kazi, Tanzania.

 

Kwenye Simba Day kuna kitu kilionekana, kitu ambacho kilinishtua, kitu ambacho kilinifanya nikitazame kwa umakini zaidi.

Macho yako yaliona burudani katika miguu ya Chama, burudani ambayo wengi walikuwa wanaitaka katika miguu ya Haruna Niyonzima lakini ilipatikana ghafla kwenye miguu ya Chama.

Taratibu nafsi yangu ilizungumza kuwa mashabiki wa Simba wanaenda kumsahau Haruna Niyonzima. Nilijipa muda ili kukamilisha kitu ambacho nilikiona Siku ile.

Kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo naona ukweli wa nafsi yangu ulivyokuwa unazungumza na Mimi. Huyu ana burudani kubwa sana kwenye miguu yake.

Burudani ambayo tulikuwa tunaitaka kutoka katika miguu ya Haruna Niyonzima, lakini akatunyima kabisa. Leo hii Chama anatupa.

Leo hii Chama anaanza taratibu kujipenyeza kwenye mioyo ya mashabiki wa Simba.Ule Ufalme ambao walikuwa wamemwandalia Haruna Niyonzima naona kiti chake kinasogezwa kwa Chama.

Hapana shaka huyu Chama ndiye anayekuja kuua Ufalme wa Haruna Niyonzima, Ufalme wa burudani bora ya mpira wa miguu, na kadri Haruna Niyonzima anavyokaa kwenye benchi ndivyo kaburi lake linavyochimbwa.

 

Sambaza....