Niyonzima
Ligi Kuu

Derby iliyotawaliwa na wageni!

Sambaza....

Ni mchezo wa raundi ya pili tena kati ya Yanga na Simba baada ya mchezo wa kwanza kuisha kwa sare ya mabao mawili kwa mawili katika uwanja wa Taifa. Safari hii ni March 8 wababe hawa wanakutana.

Kuelekea mchezo huu tambo za mashabiki zimeshika hatamu huku kila shabiki akitamba kutokana na uwezo wa wachezaji wao. Mashabiki wa Simba wamekua wakitaja nyota wao wanaoamini watawapaa ushindi huku hali ikiwa sawa kwa Yanga pia.

Katika wachezaji nyota wanaoimbwa na mashabiki asilimia kubwa ni nyota wa kigeni huku wazawa wakiwa hawana nafasi katika midomo ya wapenda soka hao. Kwa kiasi kikubwa “Derby” imeonekana kutawaliwa na wachezaji wa kigeni kutokana na jinsi wanavyofanya vizuri katika michezo mingi ya Ligi Kuu Bara.

Tovuti yako pendwa ya Kandanda inakuletea baadhi ya nyota wa kigeni wanaofanya vizuri huku pia wakiwa wachezaji pendwa kwa mashabiki wao.

Benard Morrison – Yanga sc 

Benard Morrison amefanikiwa kuingia mapena kabisa katika mioyo ya mashabiki wa Yanga kutokana na vitu vya msingi na visivyo vya msingi anavyofanya uwanjani. Mashabiki wa  Yanga wanaamini kabisa atakua chachu ya ushindi huku akitegemewa kumpa kazi beki wa Simba Shomary Kapombe.

Haruna Niyonzima – Yanga sc.

Haishangazi mashabiki wa Yanga kuamini katika uwezo mkubwa wa Mnyarwanda huyo na hii ni kutokana na uzoefu mkubwa alionao pamoja na kucheza mechi nyingi za watani. Haruna anategemewa na mashabiki wa Yanga kuweza kuwapa furaha haswa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao kwa washambuliaji.

David Molinga – Yanga Sc.

Mashabiki wa Yanga wamekua 50 kwa 50 kuukubali uwezo wa Mcongo huyo lakini uwezo hafifu unaoonyeshwa na mshambuliaji wao Yikpe mashabiki wa Yanga wamejikuta wakibaki na tumaini pekee kwake. Uwezo mkubwa wa David Molinga katika kupiga mipira iliyokufa ndio unafanya mashabiki wa Yanga kuwapa presha mashabiki wa Simba.

Luis Miquissone – Simba sc.

“Konde Boy” amejikuta akiwa katika midomo ya mashabiki wa Simba baada ya michezo michache aliyocheza akiwa na jezi ya Simba. Chenga za maudhi, mashuti na kasi ndivyo vinavyowafanya mashabiki wa Simba kuwatishia wapinzani wao March 8.

Cleotus Chama

Cleotus Chama  – Simba sc.

Hakuna kitu mashabiki wa Simba wanafurahia kama miguu ya Chama akiwa uwanjani haswa uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi na chenga. Mashabiki wa Simba wanaamini Chama ndie atakakua kiini cha ushindi katika mchezo wao dhidi ya Yanga.

Meddie Kagere – Simba sc

Mnyarwanda huyu katika msimu huu amepungua kasi katika ufungaji tofauti na msimu uliopita lakini hilo halizuii kwa yeye kutajwa na mashabiki wakiamini ndie atakawapa ushindi katika mchezo huo. Meddie mpaka sasa ndie galacha wa magoli katika VPL akiwa na magoli 14.

Deo Kanda.

Alifunga goli katika mchezo wa kwanza dhidi ya Yanga halafu akapata majeruhi lakini sasa amerudi tena na anategemewa kuwepo March 8. Deo Kanda amekua akisifika kwa kasi na maarifa akiwa na mpira na hivyo kuwafanya mashabiki wa Simba kuendelea kujivunia uwezo wa winga huyo.

Hao ni baadhi tu ya nyota wanaotarajiwa kuwapa furaha mashabiki wao lakini pia wapo wengine kama Papy Tshishimbi na Lamine Morro kwa upande wa Yanga. Pia kuna Francis Kahata na Sharaf Shiboub.

Sambaza....